Jumanne, 24 Aprili 2012

ARCADO NTAGAZWA AFIKISHWA KISUTU JANA KWA TUHUMA ZA UTAPELI

WAZIRI wa zamani wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Arcado Ntagazwa (65), amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kujibu mashitaka ya kujipatia mali ya Sh milioni 74 kwa njia ya udanganyifu.

Arcado Ntagazwa.

Katika kesi hiyo iliyosomwa mahakamani hapo jana, Ntagazwa anashitakiwa pamoja na mtu anayedaiwa kuwa ni mtoto wake, Dk. Webhale Ntagazwa (29) na Seneta Julius Miselya (60).

Baada ya kusomewa mashitaka na kuyakana, waliachiwa kwa dhamana isipokuwa Miselya ambaye hakuwa ametimiza masharti ya dhamana kwa wakati huo.

Wakisomewa mashitaka yao jana mbele ya Hakimu Liud Chamshama, Mwendesha Mashitaka Wakili wa Serikali, Ladislaus Komanya alidai kuwa Ntagazwa na wenzake hao walijipatia mali hiyo kwa udanganyifu.

Walidaiwa kuwa Oktoba 22, 2009 maeneo ya Mikoroshini Msasani katika Wilaya ya Kinondoni, washitakiwa kwa nia ya udanganyifu walijipatia kofia 5,000 na fulana 5,000 kutoka kwa Noel Severe zenye thamani ya Sh milioni 74.

Ilidaiwa na Komanya kuwa washitakiwa hao walimdanganya Severe kuwa bidhaa hizo wangezilipa baada ya mwezi mmoja tangu kupewa mzigo huo, jambo ambalo hawakulitekeleza.

Washitakiwa hao walikana mashitaka yao na wakili wa Ntagazwa, Alex Mgongolwa aliomba dhamana kwa wateja wake akidai kuwa Ntagazwa ni mtu anayeaminika, kwa kuwa alipata kuwa Waziri na Mbunge kwa muda mrefu.

Wakili wa Serikali hakuwa na pingamizi kwa washitakiwa kupewa dhamana kwa sababu mashitaka wanayokabiliwa nayo yanadhaminika kisheria.

Hakimu Chamshama naye hakuwa na pingamizi, hivyo kutoa dhamana kwa washitakiwa kwa masharti ya kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika, watakaosaini hati ya dhamana ya Sh milioni tano.

Washitakiwa walitakiwa kutoa Sh milioni 12 taslimu au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani hiyo, kutotoka nje ya mkoa wa Dar es Salaam bila ruhusa ya Mahakama na kukabidhi mahakamani hapo hati zao za kusafiria

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni