Ijumaa, 6 Aprili 2012

ALIYEKUWA MBUNGE WA ARUSHA MJINI BW. LEMA HAIAMINI MAHAKAMA!!? IKULU YASEMA KAULI YAKE NI YA KIPUUZI.


Bendera ya Rais wa Tanzania

Na Mwandishi Wetu
 Ikulu ya Tanzania imesema kuwa kauli aliyoitoa aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema muda mfupi baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha juu ya kuihusisha Ikulu na Rais Jakaya Kikwete katika kesi hiyo ni ya kipuuzi.
IKULU
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari kutoka Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, imesema Rais Kikwete wala Ikulu haijawahi kuingilia kesi yake kwa namna yoyote ile, na wala haijawahi kutokea hata kwa kesi zingine zozote.
“Kwa hakika, haijapata kutokea Kikwete, tokea alipoingia madarakani, Desemba 21, 2005, akaingilia, kwa namna yoyote ile, mwenendo wa kesi yoyote ile katika Mahakama yoyote na ya ngazi yoyote katika Tanzania. Na wala hakusudii kufanya hivyo wakati wote wa muda wake uliobakia wa uongozi,” ilisema Ikulu katika taarifa hiyo.
Aidha imeainisha kuwa si kazi ya Rais kutoa hukumu ama kuelekeza namna ya kutoa hukumu katika kesi zilizoko Mahakamani. Rais hana madaraka wala mamlaka hayo.
Katika mahojiano yake leo, Alhamisi, Aprili 5, 2012, na Redio One, ikiwa ni kauli yake ya kwanza baada ya Mahakama Kuu ya Arusha kutangaza kumvua ubunge, aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, amedai kuwa Jaji Gabriel Rwakibalira imetokana na maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete na Ikulu.
“Kauli hii ya Lema ni upuuzi. Sio Rais Kikwete wala Ikulu imeingilia kati kesi yake kwa namna yoyote ile, iwe ni kwa kupiga simu ama kuzungumza na Jaji Rwakibalira…Siyo kazi ya Rais kutoa hukumu ama kuelekeza namna ya kutoa hukumu katika kesi zilizoko Mahakamani. Rais hana madaraka wala mamlaka hayo,” imefafanua taarifa hiyo.
Imeongeza kuwa kauli ya Lema ni ukosefu mkubwa wa adabu na heshima kwa Mahakama ambao ni muhimili huru usioingiliwa na Serikali ama na Muhimili mwingine katika maamuzi yake. Lema amekuwa kiongozi kwa muda sasa, hivyo ni lazima atambue jambo hili kubwa na muhimu katika mfumo mzima wa utawala wa nchi yetu.
“Ni jambo lisilokuwa na mshiko wala tija, na kwa kweli ni bahati mbaya, kwamba Lema anajaribu kuingiza mambo yasiyohusika katika jambo la dhahiri kabisa kuwa ni la kisheria ambalo msingi ni hoja na maelezo mahakamani.
Lema asitafute visingizio kwa yaliyomfika kwa sababu hakuna mtu mwingine wa kumbebea msalaba huu. Badala ya kutafuta mchawi asiyekuwepo, ni vyema Lema angekaa chini na kuangalia ni sababu zipi za kisheria zilizomfanya ashindwe na kama ameridhika kuwa hakutendewa haki akate rufani kwa mujibu wa sheria na taratibu. Tunaomba wananchi wampuuze. Ameshindwa kesi kwa makosa yake aliyofanya hana mtu wa kumlaumu bali ajilaumu mwenyewe.” Imeeleza taarifa

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni