Jumapili, 16 Juni 2013

DK. HOSSEAH WA TAKUKURU AFUNGUKA, ASEMA TAKUKURU INATENGWA NA SERIKALI.


Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hoseah 

Dodoma. Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hoseah, amefunguka na kueleza sababu za taasisi yake kushindwa kuwakamata walarushwa wakubwa kwa kuwa Serikali imemfunga mikono.
Akitoa majumuisho katika Mkutano Mkuu wa Chama cha Wabunge Wanaopambana na Rushwa nchini (APNAC) jana, Dk Hoseah alisema kuwa Serikali imeitenga Takukuru na kuwafanya waishi kama yatima.
Huku akishangiliwa na idadi kubwa ya wabunge, mkurugenzi huyo alisema kuwa amekuwa akishangazwa na lawama ambazo amekuwa akibebeshwa kila wakati kuwa ameshindwa kumaliza rushwa wakati bila kuziangalia sheria.
“Mnanipa lawama kila wakati, lakini huwezi kuanzisha chombo kama Takukuru halafu ukamfunga mikono mhusika, na mimi mmenifunga mikono nifanyeje jamani? Alihoji na kuongeza:
“Hata katika rasimu ya Katiba bado mmetutenga kama watoto yatima, wenzetu wote mmewaweka tena hata CAG mmesema kuwa mamlaka yake akiteuliwa basi asiingiliwe wala kuhojiwa…mamlaka gani mtu asihojiwe jamani, mimi nikiuliza Takukuru mnasema subirini Serikali ya Tanganyika.”
Gazeti la Guardian la Uingereza la Jumapili ya Desemba 19, 2010, lilitoa taarifa ya siri kuhusu wala rushwa wakubwa kulindwa Tanzania. Gazeti hilo lilichapisha taarifa za mtandao wa WikiLeaks uliokuwa ukimilikiwa na mwandishi wa habari wa Australia, Julian Paul Assange, ukimnukuu Dk Hoseah.
Dk Hoseah alinukuliwa na WikiLeaks akimueleza mwanadiplomasia wa Marekani aitwaye Purnell Delly, Julai 14 jijini Dar es Salaam mwaka 2007 kuhusu uwezo na nia ya Rais Kikwete katika kushughulikia ufisadi.
Alidai Rais Jakaya Kikwete alikuwa anakwamisha kuchunguzwa kwa vigogo wa Serikali wanaotuhumiwa kwa vitendo vya rushwa, na pia anahofia maisha yake kama mkuu wa Takukuru. Hata hivyo, Dk Hoseah kwanza alikiri kukutana na ofisa huyo ofisini kwake Julai 2007, lakini alikanusha kuzungumza kuwa Rais Kikwete alikuwa hataki sheria ichukue mkondo wake katika kuwachunguza vigogo wanaotuhumiwa kwa rushwa.
Atoa ushauri kwa Serikali
Kwa mara ya kwanza jana kiongozi huyo aliitolea uvivu Serikali kuwa imekuwa ikichangia mambo mengi katika rushwa ikiwamo usiri mkubwa katika rasilimali za nchi.
“Lazima Serikali iwe wazi, huwezi kuwaficha wananchi rasilimali zao eti ni siri kwa sababu ya sera mbovu, tunawaambia wananchi watanufaika na mirabaha ya asilimia tatu hiyo siyo sahihi jamani ndiyo maana tunashindwa kutoa majibu kwa wananchi wetu hilo ni tatizo jingine linalosababisha mambo ya rushwa,”alisema na kuongeza: “Siyo kila jambo ambalo serikali inapewa ushauri ni baya.”
Alipinga kitendo cha viongozi kuwa na kigugumizi katika uwajibikaji na akataka itungwe sheria kali ya kutaka kiongozi awajibike mara anapokuwa ametuhumiwa kwa jambo lolote aachie ngazi na kupisha uchunguzi kama ilivyo kwa nchi zingine.
Credits; Gazeti la Mwananchi

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni