Jumanne, 7 Februari 2012

WAZIRI ATIMULIWA NA NYOKA KANISANI.

Mh. Aggrey Mwanri kushoto akiwa na Askofu Thomas Laizer(Picha na Maktaba)
NAIBU Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Aggrey Mwanri, juzi
alitimua mbio kunusuru maisha yake na waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini, Usharika wa Sanya Juu, mtaa wa Kilingi.

Hali hiyo ilitokea baada ya tukio la nyoka kutoka kusikojulikana kuingia kanisani humo huku Naibu Waziri akijiandaa kuendesha harambee ya ujenzi wa Kanisa hilo. Tukio hilo lilitokea katika ibada ya saa nne iliyokuwa ikiongozwa na Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini, Dk. Martin Shao, ambayo pia ilikuwa ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi huo.

Mwanri aliyekuwa mgeni rasmi kwa ajili ya kuendesha harambee hiyo ya Kanisa la Kilingi, akiwa na mkewe meza kuu, aliwashangaza waumini alipokimbia akiwa amenyanyua mikono juu. Kutokana na kuibuka kwa nyoka huyo, waumini walikimbizana na kiumbe huyo kwa mawe na viti bila kujali kama walikuwa ibadani, huku Askofu na wachungaji wengine wakiendelea kusali na waumini kutakiwa kurejesha utulivu katika ibada.

Hata hivyo, jitihada za waumini za kumkimbiza nyoka huyo kutaka kumwua hazikufanikiwa, baada ya kutoweka asionekane tena, jambo lililoacha simulizi la ni kwa jinsi gani alifika mahali hapo. Awali mgeni rasmi wa harambee hiyo, alikuwa awe Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, lakini kutokana na kubanwa na shughuli za sherehe za maadhimisho ya miaka 35 ya kuzaliwa CCM, alishindwa kufika.

'Habarileo' lilishuhudia Mwanri ambaye pia ni Mbunge wa Siha akikimbia huku akitamka maneno ya “shindwa kwa Jina la Yesu wewe shetani, shetani shindwa kwa Jina la Yesu,” huku wageni wengine waalikwa wakianguka chini wakijiokoa.



Akizungumza na 'Habarileo', Mwanri alisema tukio hilo ni la kushangaza zaidi, kwani nyoka huyo alipita nyuma ya watu wote, lakini hakuonekana hadi katika meza yake huku akiwa amenyanyua kichwa chake na kutema sumu.

“Inashangaza sana kwani lazima ujiulize alifikafikaje hapo mbele, wakati nyuma yangu kulikuwa na watu wengi...alikuwa na hasira sana, kwani alikuwa tayari kung'ata, kwa kweli hadi sasa mimi sielewi ni mambo gani haya,” alisema Mwanri. Hata hivyo hakuna madhara makubwa yaliyotokea mbali na mhamaniko uliowapata waumini hao. Nyoka huyo hakuweza kutambuliwa aina yake kutokana na mtafaruku huo

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni