Jumapili, 19 Februari 2012

JAJI MKUU AASA MAHAKIMU WAACHE TABIA YA KUHAIRISHA KESI

MAHAKIMU nchini wametakiwa kuacha utamaduni wa kuahirisha kesi bila sababu za msingi hali inayoleta manung'uniko kati ya mshitakiwa na mdai haki.

Aidha mawakili na wanasheria nao wameaswa kuacha tabia ya kujali maslahi kwa wateja wao
bali waangalie jinsi ya kuwasaidia kupata haki badala ya kuwatetea huku wakijua
wateja wao hawatafanikiwa.

Hayo yalisemwa jana na Jaji Mkuu wa Tanzania, Othman Chande wakati alipokuwa
akifungua mkutano wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) unaofanyika mkoani
Arusha kwa siku mbili.

Alisema kwenye Mahakama kuna utamaduni kwa baadhi ya Mahakimu kuahirisha kesi bila
sababu za msingi na kuongeza kuwa kwa kufanya hivyo kunaleta malalamiko kati ya
mtuhumiwa na aliyefungua kesi hali inayopelekea wananchi kukosa imani na Mahakama.

Pia alisema si busara kwa mawakili ambao ni maofisa wa Mahakama kujali fedha kwa
wateja wao huku wakijua haki itatendeka na kuwaasa kuacha tamaa za fedha badala
yake watoe huduma kwa wananchi ambao wanahitaji msaada wa kisheria pasipo kuwa na
fedha.

"Acheni tabia ya kutaka fedha huku mkijua wateja wenu hawatafanikiwa katika kesi
inayowakabili pia na Mahakimu acheni tabia ya kuahirisha kesi bila ya kuwa na sababu
za msingi."

Aliongeza kuwa baadhi ya wananchi hawana uwezo wa kawaida kupata mawakili wa
kuwatetea kutokana na fedha lakini kisheria inatakiwa mawakili kujitolea kuwasaidia
washitakiwa kwenye kesi zao, hivyo wawe na moyo wa huruma na si kuangalia maslahi
yao binafsi.

Naye Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Francis Stola aliiomba Serikali
kutenga fedha kwa wakati za mashauri ya kesi za uchaguzi na yale ya dharura ili kesi
hizo ziweze kuamuliwa kwa wakati badala ya kupoteza muda.

Pia alisema wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maktaba, vitabu vya sheria
pamoja na tatizo la rushwa kwa baadhi ya wanasheria ambao wanatia doa taaluma hiyo
na kusisitiza kuwa taaluma hiyo ni muhimu katika kusaidia jamii mbalimbali

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni