Mapigano makali yanaendelea karibu na makazi ya kiongozi wa Libya Kanali Muammar Gaddafi baada ya waasi kudhibiti sehemu kubwa ya mji wa Tripoli siku ya Jumapili.
Usiku wote kulikuwa na umati wa watu wakishangilia katika bustani ya Green Square, awali eneo hilo lilikuwa likiwakilisha sura ya maandamano ya watu wanaomuunga mkono Gaddafi.Waasi walikumbana na upinzani mdogo walipoingia kutokea mashariki, kusini na magharibi.
Msemaji wa waasi anasema majeshi ya Gaddafi bado yanadhibiti asilimia 15-20% ya Tripoli.
Waasi pia walisema wamemkamata mtoto wa kiume wa Kanali Gaddafi Saif al-Islam, lakini hakujawa na taarifa aliko Kanali.
Vifaru viliibuka kutoka kwenye makazi ya Daddafi Bab al-Azizia mapema Jumatatu asubuhi na kuanza kufyatua risasi, msemaji wa waasi alisema.
Milio ya risasi imekuwa ikisikika kwa muda mrefu katika eneo hilo.
Viongozi wan chi za Magharibi wameipokea hatua ya waasi na kumtaka Kanali Gaddafi kuondoka.
China imesema itashirikiana na serikali yoyote ambayo itakuwa ni chaguo la watu wa Libya.
Bendera zachanwachanwa
Mwandishi wa BBC mjini Tripoli , Rana Jawad, ambaye ameshindwa kuripoti waziwazi kuanzia mwezi Machi, anasema watu katika maeneo jirani mashariki mwa Tripoli waliamshwa na Imam wa msikiti wa wenyeji akiimba wimbo wa Taifa wa kabla ya utawala wa Gaddafi.
Kuna dalili kuwa mwisho unakaribia na waasi wamefanikiwa kupata kile walichokuwa wakikitaka, mwandishi wa BBC anasema.
Katika bustani ya Green Square – ambayo itarejea kuitwa jina lake la zamani kabla ya utawala wa Gaddafi la Martyrs' Square – watu wanaowaunga mkono waasi walichana bendera za kijani za serikali ya Gaddafi na kukanyaga picha za Kanali Gaddafi.
"Wakati wa kuupinga utawala wa Gaddafi sasa umefikia kilele. Tripoli inaanguka kutoka mikononi mwa dikteta. " alisema Rais wa Marekani Barack Obama katika taarifa.
Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron, ambaye amesitisha likizo yake kusimamia kikao Baraza la Usalama la Taifa alisema ni wazi " sasa mwisho wa Gaddafi umekaribia."
Bw Cameron alisema kiongozi wa Libya "amefanya uhalifu dhidi ya watu wa Libya na lazima aondoke sasa kuepusha mateso zaidi kwa watu wake ".
Mahakama ya Uhalifu wa Kimataifa mjini The Hague inafanya majadiliano kumhamisha Saif al-Gaddafi kwa mashtaka ya uhalifu wa kivita. Mahakama hiyo pia inatafuta kumkamata Kanali Gaddafi na mkuu wake wa Usalama, Abdullah al-Sanussi.
Mtoto mwingine wa Gaddafi Muhammad, alizungumza kwa simu kupitia Televisheni ya al-Jazeera wakati waasi walipoizunguka nyumba yake. Milio ya risasi ilisikika kabla ya mawasiliano kukatika.
Duru za kidiplomasia zimeliambia shirika la habari la AFP kuwa Kanali Gaddafi anaweza kuwa bado yuko Bab al-Azizia. Hajaonekana hadaharani tangu mwezi Mai, ingawa amekuwa akitoa ujumbe wa radio kutoka maeneo yasiyojulikana.
Picha za televisheni zilionyesha raia wa Libya wakipiga magoti na ardhini kushukuru kwa kile walichokiita "siku iliyobarikiwa".
Uongozi wa waasi, Baraza la Mpito la Taifa (NTC) umetangaza kuhamisha makao yake makuu ya harakati kwenda Tripoli kutoka mashariki mwa mji wa Benghazi ambao umekuwa mikononi mwa waasi tangu siku za mwanzo ya machafuko ya kisiasa.
Ufaransa inasema kiongozi wa NTC, Mustafa Mohammed Abdul Jalil,anatarajiwa kwenda Paris wiki ijayo kwa ajiliya mkutano wa "Kundi la Kimataifa" la nchi zinazohusika na mstakabali wa Libya.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni