Jumatatu, 15 Agosti 2011

NCCR YASEMA ITAMUUNGA MKONO MGOMBEA MWENYE NGUVU IGUNGA.


Naibu katibu Mkuu wa Chama Cha CUF, Julius Mtatiro, akizungumza na waandishi wa habari, kuhusu chama hicho kuwa na mgombea katika uchaguzi mdogo wa bunge Jimbo la Igunga, mkoani Tabora jana.Kulia ni Naibu Katibu wa Jumuiya ya vijana Abubakari Kitogo. Mazungumzo hayo yalifanyika jijini Dar es Salaam.Picha na Said Powa
Waandishi wetu
KINYANG'IRO cha uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga kimezidi kushika kasi baada ya jumla ya wanachama 26 wa vyama tofauti vya siasa kuomba ridhaa ya kuchaguliwa kuviwakilisha kuwania kiti hicho kilichoachwa wazi na Rostam Aziz.

Idadi hiyo ya wanasiasa wanaowania kiti hicho inazidi kuongeza joto la kisiasa kuelekea uchaguzi huo ambao tayari vyama vya CCM na Chadema kila kimoja kimeanza kukishutumu kingine kutokana na kile kinachodaiwa ni kuwapo kwa mchezo mchafu kabla ya kampeni.

Kwa mujibu wa orodha rasmi ya wagombea wa vyama waliomba ridhaa hiyo, hadi jana walikuwa wamefikia 26 huku mchakato wa kuchukua fomu ndani ya vyama ukiwa katika hatua za mwisho.

Dazeni moja wajitokeza Chadema

Mkurugenzi wa Sera na Utafiti wa Chadema, Waitara Mwikabwe alisema wanachama waliojitokeza kuomba ridhaa ya chama hicho kuwania nafasi hiyo hadi jana walikuwa 12.

Alisema mchakato huo unaendelea mpaka saa 10:00 jioni ya Agosti 16, mwaka huu na baada ya hapo kamati teule itaendelea na kazi ya kuteua jina litakaloingia katika kinyang’anyiro hicho.

Mwikabwe aliwataja wanachama waliochukua fomu kuwa ni pamoja na Kajua Sebastian, Marco Amos, Kahema John, Buzinza Magego, Dickson Samson, Anwar Luhumbi, Erasto Tumbo, Joseph Mwandu, Juma Katigula, Frank Matto, Joseph Mapalala na Juma Chaha.

13 wajitokeza kuwania ridhaa ya CCM

Kwa upande wake, Katibu wa CCM wa Wilaya ya Igunda, Neema Adam alisema katika chama hicho waliojitokeza kuwania nafasi hiyo ni 13 na mchakato huo wa kuchukua fomu ulihitimishwa saa 10:00 jioni ya Agosti 13, mwaka huu.

Adam aliwataja wanachama hao waliojitokeza kuwania nafasi hiyo kuwa ni Amina Ally Said, Ngassa Nicolaus, Shams Feruzi, Adam Brown, Shell David, Dk Peter Daniel Kafumu, Makoba Mchenya, Joseph Ally Omary, Seif Hamis Gulamaly, Hamis Shaabani, Nathan Mboje, Hamadi Hemed Safari na Paul Ndohele.

Kwa utaratibu, mchakato wa kumpata mgombea wa CCM huanzia kwenye ngazi ya kata ambako wagombea hupigiwa kura na wanachama, kisha matokeo hupelekwa Kamati ya Siasa ya Wilaya ambayo hutoa alama pasipo kukata jina kisha hupeleka mapendekezo Kamati ya Siasa ya Mkoa ambayo nayo hupitia na kutoa mapendekezo kwenda Kamati Kuu (CC) chini ya Mwenyekiti Taifa kwa uamuzi wa mwisho.

CUF wamteua Mahona

Chama cha CUF chenyewe kimefikia hatua ya mwisho ya  mchakato baada ya kumtangaza Leopard Mahona (30), kuwa mgombea atakayewania ubunge jimbo hilo.

Akizungumza jijini Dares Salaam jana, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro alisema lengo la chama hicho ni kuchukua jimbo hilo lililoachwa wazi na Rostam.

Julai 14 mwaka huu, Rostam alitangaza kujivua nyadhifa mbili ya ubunge na ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), kutokana na kile alichodai kuwa ni siasa uchwara ndani ya chama chake.

Mtatiro alisema mgombea huyo ambaye ni mwenyeji wa Igunga alichuana na Rostam katika Uchaguzi Mkuu uliopita na kushika nafasi ya pili huku akidai kwamba ni kutokana na mshindani wake kutumia fedha nyingi.

“Anakubalika ndani ya jimbo hilo na anajua uongozi na ana kiu kubwa ya kuendelea kuwatetea wana Igunga ndiyo maana alipata zaidi ya kura 11,000 katika uchaguzi uliopita,” alisema Mtatiro.

Mtatiro alisema mgombea huyo ana stashahada ya elimu ya juu ya biashara na utawala na ana uzoefu mkubwa wa utendaji baada ya kufanya kazi katika mashirika mbalimbali ya kimataifa nchini. Alisema:: CUF inaingia Igunga na “Operesheni chagua Mahona.”

Alisema wananchi wa Igunga wanapaswa kuwa makini katika uchaguzi huo kwa kuwa ndiyo utakaotoa dira ya maisha yao katika kipindi kirefu kijacho.

Mtatiro alisema kitendo cha Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa kudai kuwa CUF kimezindua kampeni za chinichini na kuipa jina la ‘Liwalo na liwe’ ni kukinyong'onyeza na kusisitiza hakijawahi kufanya uzinduzi wowote wa kampeni ya uchaguzi wa Igunga tangu jimbo hilo liwe wazi.

“Kulizungumza tu linaweza kuonekana dogo, lakini ni jambo kubwa sana katika chama na kauli hiyo inatuvurugia heshima yetu kwa jamii,” alisema.

Kuhusu gharama za uchaguzi
Naibu Mkurugenzi wa Uchaguzi wa CUF, Shaweji Mketo alisema kwa mujibu wa Sheria ya Uchaguzi gharama za uchaguzi katika Jimbo la Igunda zinapaswa kutozidi Sh80milioni na siyo 40 kama ilivyoelezwa na Msajili.

Alisema ameshangazwa na kauli ya msajili kwamba gharama za uchaguzi wa jimbo hilo hazitakiwi kuzidi ya Sh40milioni, kwa chama chochote. Hata hivyo, hakuwa tayari kuzungumzia gharama walizoziandaa kwa ajili ya uchaguzi huo akisema watatumia kiasi kidogo tu cha fedha.

Sau yajitosa kuweka mgombea

Chama cha Sauti ya Umma (Sau) nacho kimeingia katika mbio za kuwania ubunge katika uchaguzi huo mdogo na tayari kimetamba kutwaa jimbo hilo baada ya kufanikiwa kuwateka baadhi ya viongozi wa vyama vingine na wanachama wake.

Meneja wa kampeni wa chama hicho Melckezedek Leseka alisema mpaka jana, walikuwa wamefanikiwa kuwahamishia viongozi wa vyama vya Chausta na UDP pamoja na wanachama wao wote katika chama chao.

Leseka alisema Sau kimefanikiwa kufungua matawi kwenye vijiji vyote na kwamba hawatishwi na vyama vingine vilivyoingia kwenye mbio hizo vya CUF, Chadema na CCM ambavyo alisema vimejaa ubabaishaji kwa kuhubiri udini, ukabila na ahadi nyingi za uongo.

Katibu wa Sau Wilaya ya Igunga, Shaabani Kirita alisema mpaka jana wanachama watano walikuwa wamejitokeza kuchukua fomu kwa ajili ya kuomba kuteuliwa kugombea nafasi hiyo ya Ubunge.

Aliwataja wanachama hao kuwa ni John Majid Magumu, Mwalimu Leonard Agustino, Sospeter Kabunguru, Sophia Ally na Joseph Mohamed Said.

Alisema Kama Kuu (CC) ya chama hicho itakutana Agosti 22, mwaka huu kuteua mgombea ambaye chama kitampitisha kubeba bendera yake.

NCCR kuunga mkono mwenye nguvu

Chama cha NCCR-Mageuzi, kimetangaza kuwa hakitasimamisha mgombea katika uchaguzi huo mdogo wa Igunga na badala yake kimesema kitamuunga mkono mgombea wa chama chochote cha upinzani.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa chama hicho, Samwel Ruhuza alisema ili wapinzani waweze kushinda ni lazima wakubali kushirikiana na kukubaliana kusimamisha mgombea mmoja tu katika jimbo hilo.

“NCCR tunaamini katika ushirikiano na tumekuwa tukifanya jambo hilo karibu kila uchaguzi…, nia yetu ni kuhakikisha  CCM haishindi,” alisema Ruhuza.

Sau, Chadema warushiana vijembe

Wakati NCCR kikitaka umoja wa vyama, Chadema na Sau vimeingia katika malumbano baada ya kushambuliana kwa maneno huku viongozi wake wakirushiana vijembe.

Mwenyekiti wa Sau, Paul Kyara aliwataka wananchi wa Jimbo la Igunga wasipoteze muda wao kukichagua Chadema kwenye uchaguzi ujao kutokana na kile alichodai kuwa kimejaa ubabe na ni kama kampuni inayolenga kuwanufaisha watu wachache.

Kyara ambaye aliwahi kuwa Mweka Hazina wa Chadema alidai kwamba Chadema ni chama cha kidikteta ambacho hakithamini viongozi wake na ndiyo maana kimekuwa kikiwafukuza na kuwanyang'anya uanachama, bila kujali maslahi ya wananchi waliowachagua.

Alikuwa akirejea hatua ya Chadema ya hivi karibuni kuwafukuza madiwani watano wa Arusha na kudai kwamba wapo mbioni kumfukuza Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda.

Hata hivyo, Mwikabe alijibu tuhuma hizo akisema chama chake ni makini hakiwezi kubishana na chama cha mfukoni kama Sau ambacho alidai kwamba kipo kwa ajili ya kuganga njaa.

"Jamani hiki chama ni cha kutafutia mlo hakina jipya kinataka umaarufu kupitia Chadema, waambieni sisi tupo kukabiliana na baba yao CCM wanayemtumikia siyo wao ambao tuna uhakika kwamba wapo kwa ajili ya kumsaidia bwana mkubwa wao CCM, njaa zitawaua," alisema Mwikabe.

Habari hii imeandikwa na Elizabeth Ernest, Fidelis Butahe, Dar Mustapha  Kapalata na John Dotto, Igunga

Chanzo; Gazeti la Mwananchi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni