Jumamosi, 13 Agosti 2011

EWURA YAIFUNGIA KAMPUNI YA BP KWA UKAIDI WA KUACHA MGOMO WA KUUZA MAFUTA.

KILE kilichokuwa kikisubiriwa na wananchi wengi, hatimaye jana kilitimia kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Maji na Nishati (Ewura) kusitisha leseni ya biashara ya kampuni ya mafuta ya BP kwa miezi mitatu.

Hatua hiyo ilitangazwa jana Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Haruna Masebu, kutokana na kampuni hiyo kukaidi agizo la Serikali la kuitaka kuuza mafuta jamii ya petroli kuanzia juzi jioni.


Sambamba na hatua hiyo, kampuni zingine tatu za mafuta zimepewa onyo kali zisirudie tabia iendayo kinyume na sheria za nchi na kuziagiza ziuze mafuta kwa watu wote bila ubaguzi.

“Amri hii itafuatiliwa kwa karibu na ikibainika wamekiuka, hatua kali zaidi zitachukuliwa dhidi yao mara moja,” alisema Masebu na kuzitaja kampuni hizo kuwa ni Oilcom (T), Camel
Oil (T) na Engen Petroleum (T).

Hata hivyo, BP ambayo inaelezewa kuwa na ubia na Serikali, imepata unafuu kwamba itaendelea kuuza mafuta ya ndege ambayo Ewura haina mamlaka ya kusimamia bei zake.

Lakini pia itaruhusiwa kuuza mafuta yake yote ya petroli, dizeli na ya taa yaliyopo kwenye maghala yake kwa wafanyabiashara wengine wa jumla, kama wanataka kwa usimamizi wa
Ewura, ili kuzuia kutoharibika kwa mafuta hayo katika kipindi hicho cha miezi mitatu ambapo haitaruhusiwa kufanya biashara ya mafuta ya jumla.

“Hata hivyo, vituo vyote vya rejareja vyenye nembo ya BP vitaruhusiwa kuuza mafuta kwa kuyanunua kwa wafanyabiashara wengine wa jumla na si kwa BP,” alisema Masebu alipozungumza na waandishi wa habari.

Akifafanua kuhusu hatua hizo, Masebu alisema baada ya kutangaza bei mpya zilizoanza Agosti 3, kampuni zilianza mgomo baridi wa kuuza mafuta kutoka kwenye maghala yake.

“Hata hivyo mgomo huo haukufahamika sana kutokana na kutokea wakati kukiwa na siku za mapumziko ya muda mrefu kuanzia Agosti 6 hadi 8.

“Baada ya kugundua hilo, Bodi ya Wakurugenzi ya Ewura ilikaa Agosti 9 na kutoa agizo la kisheria kwa kampuni nne zilizoonekana kuwa vinara wa mgomo huo; BP, Oilcom, Camel Oil na Engen Petroleum,” alisema.

Kwa mujibu wa agizo hilo, kampuni hizo kuanza kuuza mafuta mara moja, kuacha mara moja vitendo vinavyozuia uuzwaji mafuta na kutoa maelezo kwa maandishi katika muda wa saa 24 kwa kuvunja Sheria ya Petroli ya Mwaka 2008 kifungu 24 (1).

“Baada ya agizo kutolewa, kesho yake kampuni zote zilianza kuuza mafuta kwenye maghala ambapo siku ya kwanza Agosti 10 ziliuzwa lita 8,535,700 kutoka kwenye maghala hayo.

“Hata hivyo, pamoja na kuuzwa kwa mafuta kwa wingi, bado BP ilionekana kukaidi amri halali ya Ewura kwa kuzingatia Sheria ya Petroli ya Mwaka 2008, kifungu 24 (1) kwa kutouza mafuta kwenye vituo vyake vyote,” alifafanua Mkurugenzi Mkuu wa Ewura.

Chimbuko Juni 22, Serikali kupitia Waziri wa Fedha wakati akihitimisha Hotuba ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2011/12, ilitoa maagizo kwa Ewura kuchukua hatua za kupunguza bei za mafuta kwa maeneo mengi.

Maeneo yaliyozingatiwa yalikuwa ni ya ukokotoaji wa thamani ya shilingi kwa kuioanisha na dola ya Marekani na kuondoa au kupunguza wigo wa asilimia 7.5 ambayo kampuni ziliruhusiwa kuwekewa ili kufidia baadhi ya gharama; Mengine ni kupitia upya misingi ya ukokotoaji wa viwango vya tozo za taasisi za umma kwa lengo la kubaki na tozo stahili na kwa viwango stahili bila kuathiri majukumu ya udhibiti na usimamizi yanayofanywa na taasisi hizo, lakini pia kupunguza tozo za kampuni za mafuta, ikiwa ni pamoja na gharama za kibenki na upotevu wa mafuta yanayosafirishwa kwenye meli na gharama ya ukaguzi.

Julai 4, Ewura ilianza mchakato kwa kutoa matangazo kwenye vyombo vya habari kuhusu
kupunguza bei za mafuta.

Pia ikaandaa dokezo lililokuwa na vipengele kadhaa, ambavyo vitapunguzwa na kusambazwa kwa wadau wakiwamo wauzaji wa mafuta nchini.

Wadau walichangia dokezo hilo na kuwasilisha Ewura kwa maandishi na hatimaye mchakato wa utengenezaji wa kanuni mpya ambayo imepunguza bei za mafuta ulihitimishwa kwa kuitisha mkutano wa taftishi uliofanyika Julai 22, katika ukumbi wa Karimjee Wadau Mchakato wa kupata maoni ya wadau ulianza Julai 4 na kukamilika Julai 26 ambapo Masebu alisema kwa kawaida, mchakato huo ungechukua siku 81 lakini kutokana na unyeti wa suala hili, Mamlaka ililazimika kuufupisha hadi siku 23.

Wadau walioshirikishwa katika taftishi hiyo ni pamoja na kampuni za mafuta, Baraza la Watumiaji wa Huduma zinazodhibitiwa na EWURA (CCC), Baraza la Ushauri la Serikali, Taasisi za Umma kama vile TRA, TBS, WMA, TPDC, TPA, SUMATRA, na TIPER.

Maoni ya wadau yalipokewa na kuchambuliwa na timu ya wataalamu kutoka taasisi mbalimbali zikiwamo Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Fedha na Uchumi, Shirika la Maendeleo ya Mafuta Tanzania (TPDC), Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Ewura na katika mfumo mzima wa kufanikisha utayarishaji wa kanuni hii mpya, wadau wote walifahamishwa katika mchakato huu kuwa bei mpya zitatolewa Agosti mosi

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni