Msimamo huo ulionesha kuwa mgomo uliokuwapo ni wa kujaribu kutengeneza mazingira ya uhaba wa nishati hiyo kwa kuchelewesha utoaji wake kwa sababu mbalimbali.
Katika maghala ya kampuni zinazosambaza mafuta zilizoko Kurasini, Dar es Salaam, gazeti hili lilishuhudia kampuni mbili ambazo licha ya kuagizwa na Serikali kusambaza bidhaa yake ya petroli lakini hazikutii agizo hilo.
Kampuni ya Engen na BP maghala yake hayakuwa na hekaheka za magari kama ilivyokuwa kwenye maghala ya kampuni zingine, ambako jana malori yalijazana kusomba bidhaa hiyo.
Gazeti hili lilitaka kujua sababu ya Engen kutotoa huduma, lakini walinzi waliokuwa getini walimwonesha mwandishi jina la Duncan Malashika, kuwa ndiye atazungumza na wanahabari juu ya suala hilo.
“Sisi watu wa Utawala wametuachia jina hili, kuwa mkija wanahabari, tuwaeleze kuwa huyo ndiye Meneja wa Kampuni na amekuja nchini na ataitisha kikao cha wanahabari,” alisema askari aliyekuwa getini.
Kwa upande wa kampuni ya BP Tanzania Limited ambayo ni mbia wa Serikali ya Tanzania yenye hisa asilimia 51, licha ya kuwapo malori ya petroli za kampuni hiyo, lakini hadi saa nane mchana hakukuwa na gari ambalo lilikuwa limetoka na mzigo.
Hakuna Ofisa wa Kampuni hiyo aliyekuwa tayari kuzungumza, huku walinzi wa kampuni hiyo wakidai kuwa wahusika walikuwa kwenye kikao na wakatoa namba ya simu ya mhusika ambaye hata ilipopigwa haikupatikana.
Kwa upande wa maghala ya Oil Com, magari yalikuwa yanapakia mzigo na kutoka, lakini mengi yalionekana ni ambayo yanapeleka mzigo nje ya nchi. Baadhi ya madereva wa magari yanayosambaza mafuta nchini ambao wananunua bidhaa hiyo kutoka Oil Com walilalamika kuwa tangu Alhamisi wiki jana wako hapo lakini hawajapata mzigo.
“Leo wanatoa mafuta lakini wanatoa kipaumbele kwa magari yanayopeleka mzigo nje, mimi niko hapa tangu Alhamisi sijapata mzigo,” alisema Hemed Said ambaye ametoka Singida.
Malalamiko kama hayo pia yalitolewa na dereva Ramadhan Ali aliyetoka Mbeya ambaye alisema Oil Com licha ya kutoa mzigo, lakini magari yanayosambaza mzigo ndani ya nchi si mengi yanayopewa mzigo.
Lakini kwa upande wa maghala ya GBP, Orxy na CamelOil, magari yote ya ndani na nje yalikuwa yanatoa mzigo hali iliyoonesha kuwa hawakuwa na tatizo. Mkurugenzi Mtendaji wa CamelOil, Abdallah Nahd, alisema walianza kutoa huduma hiyo tangu saa 12 asubuhi jana.
Nahd alisema walisitisha kutoa huduma hiyo baada ya kutofautiana kwa kiasi fulani na Serikali, lakini kutokana na hatua iliyofikiwa, walisitisha mgomo kwa kuwa wako chini ya Serikali, hivyo hawana mamlaka yoyote.
Alisema kutokana na hali hiyo, walianza kutoa mafuta hayo ambapo kwa muda huo alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari (saa 8.30 mchana), zaidi ya malori 100 yalikuwa yamepakia na kuondoka na mafuta.
Hali ilivyokuwa vituoni Magari na watu wengi waliokuwa na vidumu, bado walionekana wakigombea kupata mafuta hayo katika baadhi ya vituo vilivyoanza kuuza.
Baadhi ya vituo vililazimika kuomba ulinzi wa polisi ambao walisimamia uuzaji wa huku wengi wakipewa masharti ya kununua lita zisizozidi tano ili angalau kila mtu apate.
Gazeti hili lilipita katika kituo cha CamelOil Manzese na kukuta msongamano huo uliowalazimu walinzi wa kituo hicho kuingilia kati na kuweka utaratibu wa kuuziwa.
Kituo cha OilCom cha Big Brother Manzese, hali ilikuwa mbaya zaidi na kusababisha msongamano wa magari hadi eneo la barabara ya Morogoro na kusababisha foleni kutokana na eneo hilo kuwa makutano na barabara ya Mabibo. GAPCO eneo la Posta Mpya, magari mengi yalikuwa kwenye foleni yakisubiri kupata huduma hiyo.
Vituo ambavyo jana vilianza kutoa huduma ni vya kampuni za CamelOil, Orxy, Gapco, Lake Oil, Kobil na baadhi ya vile vya OilCom ambavyo watu wenye vidumu walijazana huku foleni za magari nazo zikiongezeka.
Kutokana na nishati ya mafuta kuendelea kuwa haba, baadhi ya vijana ambao walikuwa wanauza mafuta hayo uchochoroni, waliyauza kwa Sh 4,000 badala ya Sh 2004 kwa lita.
Mwandishi wa habari hizi, alishuhudia wafanyabiashara wa bodaboda wakinunua mafuta hayo katika eneo la Kipawa kando ya kituo cha mafuta cha OilCom. “Sisi tutaendelea kuwa na mafuta hayo si unaona tuko kando ya kituo, tunajua namna ya kuyapata,” alisema muuzaji wa mafuta hayo.
Mgomo huo unatokana na hatua ya Serikali kupitia kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) kutangaza kushusha bei hiyo baada ya Serikali kuondoa baadhi ya tozo na kodi kwa bidhaa hizo.
Katika agizo la Ewura, bei ya petroli kwa bei elekezi ni Sh 2,004 wakati dizeli ni Sh 1,911 na mafuta ya taa bei kikomo ni Sh 1,890. Bei hizo zinatokana na Serikali kupunguza zaidi ya Sh 200 kwa lita. Hatua hiyo ya Serikali iligomewa na wafanyabiashara wa mafuta na wengi wao kuamua kufunga vituo vya kuuzia mafuta kwa kisingizio kuwa hawana bidhaa hiyo muhimu kwa uchumi wa Taifa.
Mkuu wa Mawasiliano wa Ewura, Titus Kaguo alipoulizwa kuhusu hali ya jana, alisema walikuwa bado wanafanya tathmini kujua ni nani wanaendeleza nmgomo ili hatua zichukuliwe. Kuhusu mafuta yaliyiodaiwa kuwa yanapelekwa nje, alisema si kweli kwani mafuta yaliyotolewa jana ambayo aliyatolea mchanganuo yalikuwa ni yaliyowekwa vinasaba ili yauzwe ndani ya nchi.
Mchanganuo Kwa mujibu wa Kaguo, hadi saa 10 jioni, tayari jumla ya lita 5,401,600 za mafuta mbalimbali jamii ya petroli zilishapakuliwa kutoka maghalani na kupelekwa katika vituo mbalimbali vya kuuza kwa reja reja. Alisema hadi wakati huo, lita 1,821,600 za petroli zilishapakiwa.
Alisema lita 3,309,500 za dizeli zilipakuliwa huku matumizi ya siku yakiwa ni lita milioni tatu, wakati huo za mafuta ya taa zikiwa ni lita 270,500 na matumizi ya siku yakiwa lita 615,000.
Kwa mujibu wa mchanganuo huo, kampuni ya BP ilichukua mafuta lita 402,000 za dizeli na petroli lita 48,000; CamelOil lita 416,500 za petroli na 629,000 dizeli. 0ilCom ilichukua lita 382,000 za dizeli na 353,000 za petroli, huku Total ikiwa na lita 163,000 za dizeli na 0ryx lita 91,000 za dizeli na lita 44,000 za petroli. Mchanganuo huo ulionesha pia kwamba kampuni ya Gulf Bulk ilikuwa na lita 272,000 za dizeli na 86,000 za petroli wakati Engen ikichukua lita 175,000 za dizeli na 64,000 za petroli.
Kampuni ya MGS International ilichukua mafuta lita 116,000 za petroli na 232,000 za mafuta ya taa wakati NatOil ilichukua lita 79,000za dizeli, 55,000 za petroli na 4,000 za mafuta ya taa. LakeOil ilikuwa na lita 279,000 za dizeli na 65,000 za dizeli huku Gapco wakiwa na lita 418,100 za petroli, 348,000 za dizeli na 34,500 za mafuta ya taa na Kobil ikiwa na lita 37,000 za petroli na 431,000 za dizeli.
Harakati za kupata mafuta.
Camel Oil
Kampuni ya Hass ilichukua lita 37,000 za petroli na lita 431,000 za dizeli. Wakati huo huo, Kaguo alisema meli mbili za mafuta zilikuwa zimetia nanga bandarini Dar es Salaam, ambapo moja ilipakua lita milioni 15 za dizeli na nyingine hadi jana alasiri ilikuwa ikiendelea kupakua lita milioni 16 za dizeli na milioni 19 za mafuta ya ndege
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni