Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo LIBYA BBC. Onyesha machapisho yote
Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo LIBYA BBC. Onyesha machapisho yote

Jumanne, 23 Agosti 2011

KANALI GADAFFI BADO NGANGARI.

Mwanawe Gaddafi aapa kupambana na waasi

Saif al-Islam
Mwanawe Gaddafi Saif al-Islam
Mtoto wa kiume wa Kanali Muammar Gaddafi, Saif al-Islam, ambaye awali waasi walidai kuwa wamemkamata, amejitokeza katika hoteli moja inayoshikiliwa na wafuasi wa Kanali Gaddafi.
Mwandishi wa BBC Matthew Price amezungumza na Saif al-islam na kusema kuwa anaonekana kuwa mchangamfu na shauku kuu.
Saif al-Islam amesema waasi wameingia kwenye ''mtego'' mjini Tripoli na kwamba wanajeshi wanaomuunga mkoni Kanali Gaddafi walikuwa ''wamevunja uti wa mgogo wa waasi hao''.
Waasi wanaopigana kuudhibiti mji mkuu wa LibyaTripoli , wamerudishwa nyuma na wanajeshi wanaomuunga mkono Kanali Muammar Gaddafi.
Lakini wakati mapigano yanapoendelea katika maeneo mbalimbali ya mji, msafara wa waasi kutoka mashariki mwa nchi ulirudishwa nyuma.

Bado hajulikani alipo Kanali Gaddafi.

Jumapili iliyopita waasi walidai kuwa walikuwa wamemkamata Saif al-Islam, pamoja na familia yake.
Hata hivyo, bado Kanali Gaddafi hajulikani alipo. Nyumba yake inalindwa na wapiganaji wanaomtii.
Waasi hao walioingia mjini Tripoli jumamosi iliyopita walikaribishwa watu waliokuwa wakisheherekea katika bustani ya Green Square wakati walipowasili siku ya jumapili.
Waasi hao wamesema kuwa wameweka vizuizi katika sehemu mbalimbali za mji lakini wanakabiliwa na upinzani mkali katika baadhi ya maeneo.
Kamanda wa waasi amesema wanadhibiti asilimia 90 ya mji wa Tripoli.
Kiongozi wa Baraza la Mpito la kitaifa (NTC), Mustafa Abdel Jalil, amesema wakati wa ushindi halisi utakuwa pale watakapo mkamata Kanali Gaddafi.

Rais Obama apongeza watu wa Libya.

Rais Barrack Obama amewapongeza watu wa Libya kwa kile alichokitaja kama ''kujitolea mhanga kusipokuwa kwa kawaida''. Obama amesema watu wa Libya wanakaribia kupata kile wanachohitaji.
Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa, Ban Ki-Moon naye amewakumbusha wanachama wa Umoja huo kuwa, wanajukumu la kuheshimu mahakama ya kimataifa ya jinai, ambayo imetoa hati za kuwakamata Kanali Gaddafi, mtoto wake wa kiume Saif al Islam na mkuu wake wa idara ya ujasusi.
Baadhi ya viongozi wa waasi wanasema afadhali wafunguliwe mashtaka nchini Libya na sio katika mahakama ya kimataifa ya ICC, mjini The Hague

Jumatatu, 22 Agosti 2011

WAASI WA LIBYA WAPO NDANI YA TRIPOLI, KANALI HAJULIKANI ALIPO.

Waasi wa Libya wako Tripoli


Mapigano makali yanaendelea karibu na makazi ya kiongozi wa Libya Kanali Muammar Gaddafi baada ya waasi kudhibiti sehemu kubwa ya mji wa Tripoli siku ya Jumapili.
Usiku wote kulikuwa na umati wa watu wakishangilia katika bustani ya Green Square, awali eneo hilo lilikuwa likiwakilisha sura ya maandamano ya watu wanaomuunga mkono Gaddafi.
Waasi walikumbana na upinzani mdogo walipoingia kutokea mashariki, kusini na magharibi.
Msemaji wa waasi anasema majeshi ya Gaddafi bado yanadhibiti asilimia 15-20% ya Tripoli.
Waasi pia walisema wamemkamata mtoto wa kiume wa Kanali Gaddafi Saif al-Islam, lakini hakujawa na taarifa aliko Kanali.
Vifaru viliibuka kutoka kwenye makazi ya Daddafi Bab al-Azizia mapema Jumatatu asubuhi na kuanza kufyatua risasi, msemaji wa waasi alisema.
Milio ya risasi imekuwa ikisikika kwa muda mrefu katika eneo hilo.
Viongozi wan chi za Magharibi wameipokea hatua ya waasi na kumtaka Kanali Gaddafi kuondoka.
China imesema itashirikiana na serikali yoyote ambayo itakuwa ni chaguo la watu wa Libya.

Bendera zachanwachanwa


Mwandishi wa BBC mjini Tripoli , Rana Jawad, ambaye ameshindwa kuripoti waziwazi kuanzia mwezi Machi, anasema watu katika maeneo jirani mashariki mwa Tripoli waliamshwa na Imam wa msikiti wa wenyeji akiimba wimbo wa Taifa wa kabla ya utawala wa Gaddafi.
Kuna dalili kuwa mwisho unakaribia na waasi wamefanikiwa kupata kile walichokuwa wakikitaka, mwandishi wa BBC anasema.
Katika bustani ya Green Square – ambayo itarejea kuitwa jina lake la zamani kabla ya utawala wa Gaddafi la Martyrs' Square – watu wanaowaunga mkono waasi walichana bendera za kijani za serikali ya Gaddafi na kukanyaga picha za Kanali Gaddafi.
"Wakati wa kuupinga utawala wa Gaddafi sasa umefikia kilele. Tripoli inaanguka kutoka mikononi mwa dikteta. " alisema Rais wa Marekani Barack Obama katika taarifa.
Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron, ambaye amesitisha likizo yake kusimamia kikao Baraza la Usalama la Taifa alisema ni wazi " sasa mwisho wa Gaddafi umekaribia."
Bw Cameron alisema kiongozi wa Libya "amefanya uhalifu dhidi ya watu wa Libya na lazima aondoke sasa kuepusha mateso zaidi kwa watu wake ".
Mahakama ya Uhalifu wa Kimataifa mjini The Hague inafanya majadiliano kumhamisha Saif al-Gaddafi kwa mashtaka ya uhalifu wa kivita. Mahakama hiyo pia inatafuta kumkamata Kanali Gaddafi na mkuu wake wa Usalama, Abdullah al-Sanussi.
Mtoto mwingine wa Gaddafi Muhammad, alizungumza kwa simu kupitia Televisheni ya al-Jazeera wakati waasi walipoizunguka nyumba yake. Milio ya risasi ilisikika kabla ya mawasiliano kukatika.
Duru za kidiplomasia zimeliambia shirika la habari la AFP kuwa Kanali Gaddafi anaweza kuwa bado yuko Bab al-Azizia. Hajaonekana hadaharani tangu mwezi Mai, ingawa amekuwa akitoa ujumbe wa radio kutoka maeneo yasiyojulikana.
Picha za televisheni zilionyesha raia wa Libya wakipiga magoti na ardhini kushukuru kwa kile walichokiita "siku iliyobarikiwa".
Uongozi wa waasi, Baraza la Mpito la Taifa (NTC) umetangaza kuhamisha makao yake makuu ya harakati kwenda Tripoli kutoka mashariki mwa mji wa Benghazi ambao umekuwa mikononi mwa waasi tangu siku za mwanzo ya machafuko ya kisiasa.
Ufaransa inasema kiongozi wa NTC, Mustafa Mohammed Abdul Jalil,anatarajiwa kwenda Paris wiki ijayo kwa ajiliya mkutano wa "Kundi la Kimataifa" la nchi zinazohusika na mstakabali wa Libya.
Ramani

Jumapili, 21 Agosti 2011

MAPIGANO NA WAASI WA LIBYA YAFIKA MJI MKUU WA TRIPOLI.


Baada ya saa kadha za milio ya bunduki katika mji mkuu wa Libya, Tripoli, Kanali Muammar Gaddafi na mwanawe wa kiume wamesisitiza kwamba wana hakika watawashinda wapiganaji.

Katika matangazo yao Kanali Gaddafi alisema, wafuasi wake mjini Tripoli wamewafyeka wale aliowaita "panya" walioingia mjini. Na katika hotuba nyengine, mwanawe, Saif Al-Islam Gaddafi, alikana kusallim amri.

Saif al-Islam Gaddafi alisema:

"Hili swala la kusalimu amri, au kupepea bendera nyeupe, siyo jambo ambalo mtu yeyote anafaa kulizungumza, kwa sababu limekataliwa.

Huo siyo uamuzi wa Muammar Gaddafi au Saif al-Islam; ni uamuzi wa watu wa Libya."

Saif al-Islam alisema ripoti za vyombo vya habari, kwamba Kanali Gaddafi na majeshi yake yanakaribia kushindwa, ni za uongo.

Viongozi wa wapiganaji wanasema wafuasi wao mjini Tripoli, wameanzisha harakati na wanashirikiana na wapiganaji wanaokaribia mji kutoka karibu pande zote

Jumatatu, 13 Juni 2011

UJERUMANI YAWAUNGA MKONO WAASI WA LIBYA.

Ujerumani yawatambua waasi wa Libya

Ujerumani imetambua waasi wa Libya kama "Wawakilishi halali wa wananchi wa Libya".

"Tunataka Libya huru, ya amani na demokrasia bila ya kuwepo Muammar Gaddafi," Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Guido Westerwelle amesema katika ngome ya waasi mjini Benghazi.

Takriban mataifa kumi na mbili yametambua Baraza la mpito la Taifa.

Ujerumani ilishutumiwa kwa kukataa kuunga mkono azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, la kuruhusu majeshi ya Nato kulinda raia wa Libya.

Baraza hilo la mpito liliundwa na majeshi yaliyoanzisha upinzani dhidi ya utawala wa Kanali Gaddafi, Februari 16.

Baada ya miezi ya mapigano makali, Kanali Gaddafi amesalia na udhibiti wa mji mkuu Tripoli, huku waasi wakishikilia mji wa Benghazi na eneo kubwa la mashariki.

Akizungumza kwa pamoja na waziri wa mambo ya nje wa waasi, Ali Issawi, Bw Westerwelle amesema: "Tuna lengo moja: Libya bila Gaddafi.

"Baraza la taifa ndio wawakilishi halali wa watu wa Libya."

Wananchi wa Libya waliokuwa wakisikiliza, walipiga kofi baada ya tangazo hilo.

Afisa wa ngazi ya juu, makamu mwenyekiti wa baraza, Abdel Hafez Ghoga, amefurahishwa na uamuzi huo wa Ujerumani akisema ni "Hatua kubwa sana".

Wanasdiasa wa upinzani, wanahabari na wataalam wa sera za nje wa Ujerumani, walishutumu serikali kwa kutojiunga na mashambulizi ya Nato, na kuituhumu kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake ya kimataifa.

Jumanne, 31 Mei 2011

ZUMA AJITOSA KUMALIZA MGOGORO WA LIBYA.

Zuma kujaribu kutatua mzozo wa Libya

Jacob Zuma
Jacob Zuma
Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma amewasili mjini Tripoli kwa kile kinachoonekana kuwa juhudi za mwisho za kujaribu kutafuta suluhu ya kidiplomasia ya mzozo unaoendelea.
Haifahamiki kama ziara hiyo ambayo ni ya pili kwa Bw Zuma, itaangazia kumshawishi Kanali Muammar Gaddafi kuondoka madarakani.
Waasi wanaopigana na majeshi ya Gaddafi tangu mwezi Februari wamekataa kufanya mazungumzo hadi pale atakapoondoka kwenye uongozi.
Wakati huo huo chama cha Bwana Zuma cha African National Congress kimeshutumu mashambulio ya majeshi ya Nato mjini Libya.
"Tunaungana na bara hili na watu wote wanaopenda amani duniani katika kushtumu mashambulio ya anga yanayoendelea Libya yakifanywa na vikosi vya magharibi," chama cha ANC kimesema katika taarifa siku moja kabla ya ziara ya Zuma.
Shinikizo kutoka kwa jamii ya kimataifa zinaendelea dhidi ya Kanali Gaddafi, huku nchi zinazounda kundi la G8 zikitoa wito siku ya Ijumaa ya kumtaka aondoke na rais wa Urusi Dmitry Medvedev akisema siku ya Jumamosi kwamba hana tena haki ya kuwaongoza watu wa Libya.
Waasi wa Libya waliridhishwa na taarifa hiyo ya kundi la G8.
"Dunia nzima imekubaliana kwamba Kanali Gaddafi na utawala wake hawakupoteza tu uhalali wa kuongoza lakini pia heshima," alisema kiongozi wa waasi Mustafa Abdul Jalil katika taarifa

Jumapili, 29 Mei 2011

NATO YASHAMBULIA LIBYA MCHANA TOFAUTI NA MAZOEA YAO YA KUSHAMBULIA USIKU.

NATO imeshambulia nyumba ya Gaddafi

NATO inasema kuwa imeangamiza minara ya walinzi katika eneo la nyumba ya Kanali Gaddafi wa Libya mjini Tripoli, kwa mashambulio mawili yaliyofanywa na ndege za umoja huo wa kijeshi.
Watu wakizungumza karibu na jumba la Gaddafi la Babu al_aziziya baada ya kushambuliwa mwezi Aprili
Waandishi wa habari mjini Tripoli, wanasema shambulio moja lilofanywa mchana, lilivunja sehemu za ukuta unaozunguka jengo la jeshi la Bab al-Aziziya.
Msemaji wa NATO, alieleza kuwa shambulio hilo ni funzo kubwa kwa kiongozi wa Libya, kwamba hawezi tena kujificha nyuma ya kuta ndefu

Jumapili, 8 Mei 2011

MAJESHI YA GADAFFI YASHAMBULIA BANDARI YA MISRATA.

Mabomu mtawanyiko yanatumiwa Misrata


Majeshi ya Kanali Gaddafi wa Libya yametumia mabomu ya mtawanyiko, katika shambulio jengine katika mji wa bandari ya Misrata, ambao umezingirwa na jeshi hilo.

Bandari ya Misrata.
Msimamizi wa bandari alisema mabomu hayo yaliripuka chini ya lori na kujeruhi watu wawili.
Mwandishi wa BBC mjini Tripoli anasema, waandishi wana picha ambazo zinaonesha wazi mabomu yaliyojizika ardhini, yaliyofyatuliwa kutoka kombora linalorusha mabomu mtawanyiko, ambayo yamepigwa marufuku katika nchi nyingi.

Juma lilopita NATO ilitegua mabomu yaliyolengwa dhidi ya meli katika pwani ya Misrata.
Na mizinga iliyofyatuliwa na jeshi la Gaddafi nchini Libya, inaarifiwa kuwa imepiga ardhi ya Tunisia kwenye mji wa Dehiba, ulio mpakani.
Vita baina ya jeshi la wapiganaji na jeshi la Kanali Gaddafi vimezidi kuwa vikali katika juma lilopita, kwenye milima ya magharibi mwa Libya.