Jumanne, 23 Oktoba 2012

SHEIKH FARID HADI AFIKISHWA MAHAKAMANI JANA.

Shekhe Farid wa Uamsho kizimbani

Written by Khatib Suleiman, Zanzibar
 
BAADA ya uvumi wa kutoweka na kusababisha ghasia visiwani hapa na kisha kuonekana, jana kiongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu(JUMIKI) maarufu kama Uamsho, Shekhe Farid Hadi Ahmed na wenzake saba walifikishwa mahakamani kwa tuhuma za uchochezi na kusababisha fujo.
Hata hivyo, Mahakama ya Mwanakwerekwe ilikataa kutoa dhamana kwa viongozi hao hadi keshokutwa shauri lao litakaposikilizwa katika mahakama hiyo, kwa madai kwamba uchunguzi zaidi unahitajika katika matukio hayo.
Shekhe Farid na viongozi hao saba, walifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Mjini saa nne asubuhi katika msafara wa magari sita ya Polisi. Wengine waliofikishwa katika Mahakama ya Mwanakwerekwe ni kiongozi mwandamizi wa Uamsho, Shekhe Azan Khalid Hamdani (43), Mussa Juma Issa (37), Suleiman Juma (50), Hassan Bakari Suleiman (39), Mselem Ali Mselem (52) na Khamis S. Khamis.
Akisoma mashitaka yanayowakabili washitakiwa hao, Mwendesha Mashitaka wa Serikali Mohamed Ame, alidai washitakiwa hao walikwenda kinyume na kifungu 45(a) na (b) cha Sheria ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar namba 6 ya mwaka 2004.
Akifafanua, Ame alidai Agosti 17 saa 11 jioni Magogoni mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, washitakiwa hao wakiongoza Jumuiya ya Uamsho walitoa matamko ya uchochezi yanayoashiria uvunjifu wa amani na kusababisha fujo na mtafaruku kwa Serikali katika sehemu ya mihadhara yao.
Wakili wa Washitakiwa, Abdalla Juma aliomba Hakimu kuwapa hati ya mashitaka na dhamana washitakiwa hao, kitendo ambacho kilipingwa na Wakili wa Serikali.
Awali Hakimu anayesikiliza kesi hiyo, Ame Msaraka Pinja alisema baada ya kupitia hoja za kila upande, Mahakama iliona isikurupuke kutoa dhamana ili kulifanyia kazi zaidi shauri hilo.
“Mahakama imepitia maombi yote mawili kutoka kwa upande wa mashitaka na Wakili wa washitakiwa na kuona isikurupuke na ni bora kulifanyia uchunguzi zaidi shauri la dhamana,” alisema Msaraka. Kabla ya hapo, wafuasi wa Uamsho walijazana katika eneo la mahakama hiyo ambapo ulinzi uliimarishwa katika maeneo mbalimbali, ikiwamo jirani na jengo hilo.
Aidha, ulinzi uliimarishwa pia katika maeneo na barabara zinazokwenda na kuingia katika Mahakama ya Wilaya ya Mwanakwerekwe kwa ajili ya kudhibiti fujo za wafuasi wa Uamsho. Hali ya usalama katika mji wa Unguja na maeneo mengine ya mitaa kwa sasa ni shwari huku vikosi vya SMZ vikifanya doria na kutawanya makundi mbalimbali ya vijana.
Kutoweka kwake Shekhe Farid alitoweka ghafla wiki iliyopita na kudaiwa na wafuasi wake kuwa alikuwa ametekwa na vyombo vya usalama jambo lililosababisha vurugu.
Katika vurugu hizo za Zanzibar, maskani mbili za CCM za Kisonge na Mwembeladu zilichomwa moto na pia baadhi ya wafuasi wa Uamsho kudaiwa kumwua Koplo Said Abdulrahman wa Polisi kwa kumkata mapanga.
Wakati hali ikiwa hivyo na kusababisha Polisi kuongeza ulinzi Zanzibar, Shekhe Farid aliibuka ghafla na kudai kuwa alikuwa ameshikiliwa na watu wasiojulikana ambao walikuwa wakimhoji kuhusu harakati za jumuiya hiyo lakini hawakumdhuru.
Hata hivyo Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa alisisitiza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama havikuwa vimemshikilia Shekhe Farid, alisema walilazimika kumkamata na viongozi wenzake ili kufahamu wapi alikuwa na kuthibitisha kama kweli alitekwa au la kabla ya kumfikisha mahakamani jana.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni