Jumamosi, 29 Septemba 2012

JALADA KESI YA VIGOGO JKT LIPO KWA DPP.

James Magai
JALADA la kesi ya maofisa wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wanaokabiliwa na mashtaka ya matumizi mabaya ya ofisi za umma, limekwama kwa Mkurugenzi wa Mashtaka.Kesi dhidi ya maofisa hao saba waandamizi wa JKT, iko katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa SUMA JKT ambaye ni mmoja wa washtakiwa Kanali Ayoub Mwakang'ata kulia mwenye suti nyeupe.

Maofisa hao ni pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Uzalishaji Mali la jeshi hilo (Suma JKT), Kanali  Ayoub Emu Mwakang’ata na Mkuu wa Miradi, Luten Kanali Felix Andrew Samillani.
Wengine ni  Luteni Kanali Mkochi Chacha Kichogo, Luteni Kanali Paul Andrew Mayavi , Meja Peter Mabulla Lushika, Sajenti John Andrew Laizer na Meja Yohana Leonard Nyuchi.
Kesi hiyo ilitarajiwa kuanza kusikilizwa jana, katika hatua za awali ambapo washtakiwa wangesomewa maelezo kuhusu mashtaka yanayowakabili.

Hata hivyo ilikwama kutokana na kutokuwapo kwa jalada lao mahakamani.
Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Tabu Mzee, alidai kuwa jala la kesi hiyo bado liko kwa DPP, na akaomba mahakama ipange tarehe nyingine ya kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali.

Hakimu Aloyce Katemana alikubaliana na ombi hilo na kupanga maelezo hayo yasomwe  Oktoba 26 mwaka huu.
Hii ni mara ya pili kwa vigogo hao wa JKT kushindwa kusomewa mashtaka kutokana na jalada la kesi yao kuitwa na DPP.
Awali, mahakama ilipanga washtakiwa hao wasomewe maelezo hayo  Agosti 30 mwaka huu, lakini ilishindikana kutokana na jalada la kesi kuitishwa na DPP.

Hatua hiyo ilimlazimisha mwendesha mashtaka huyo wa Takukuru kuomba kesi ipangiwe nyingine na mahakama ikapanga jana.

Washtakiwa hao walipandishwa kizimbani  Julai 2 mwaka huu na kusomewa mashtaka saba yakiwemo ya kula njama na kuhamisha zaidi ya Sh3 bilioni kinyume cha sheria.

Mwendesha Mashtaka wa Takukuru, Donasian Kessy akisaidiana na Ben Lincoln, alida kuwa washtakiwa walitenda makosa hayo kwa nyakati tofauti.
Kessy alidai kuwa walitenda makosa hayo wakati wakipitisha uamuzi wa ununuzi wa magari na vifaa vya ujenzi chakavu, kula njama na kuhamisha mabilioni ya fedha kinyume cha masharti ya kifungu cha 156 cha kanuni za Fedha za Umma za mwaka 2001.

Akifafanua mashtaka hayo, katika shtaka la kwanza, Kessy alidai kuwa Machi 5, 2009 washtakiwa wote wakiwa ni wajumbe wa Bodi ya Zabuni ya Suma JKT, kwa makusudi walitumia vibaya madaraka yao kwa kupitisha uamuzi wa kununua magari ya mtumba na vifaa vya ujenzi vilivyotumika.

Alidai kuwa walitenda hayo bila mamlaka ya Bodi ya Wakurugenzi wa Takopa. Takopa ni muungano wa kampuni mbili za ujenzi ya Korea  zilizoingia ubia na  Suma JKT

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni