Jumamosi, 1 Septemba 2012

TWITE APOKELEWA KWA VISHINDO HUKO JANGWANI.

'Twite, twite, Rage, Rage'

Sosthenes Nyoni
'TWITE, Twite, Twite' kiitikio 'Rage, Rage, Rage' ndiyo wimbo  uliotawala jana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere wakati beki mpya wa Yanga, Mbuyu Twite alipowasili akitokea Rwanda.

Wimbo huo ulikuwa ukiimbwa na mamia ya mashabiki wa Yanga wake kwa waume waliofurika uwanjani hapo kwa ajili ya kumpokea beki huyo.

Kwa wiki kadhaa Twite aliteka hisia za mashabiki wa timu za Yanga na Simba ambazo ni baada ya beki huyo kusajiliwa na timu hizo kabla ya yeye mwenyewe kuikana Simba na kuamua kuichezea Yanga.

Kitendo hicho, kilisababisha kuzuka kwa malumbano baina ya viongozi wa klabu hizo mbili na kufuatiwa na tamko la Makamu mwenyekiti wa Simba, Godfrey Nyange Kaburu kusema kuwa watamkamata Twite na kumfikisha kwenye vyombo vya sheria  atakapokanyaga ardhi ya Tanzania.

Hata hivyo licha ya vitisho hivyo vya Kaburu, hakuna kiongozi yeyote wa Simba aliyeonekana uwanjani hapo kumsubiri beki huyo kwa ajili ya kumtia mikononi kama ilivyotarajiwa.

Mara baada ya kuwasili uwanjani hapo majira ya saa10.30 jioni, Twite alipokewa na viongozi wa Yanga wakiongozwa na katibu mkuu wa timu hiyo, Selestine Mwesigwa na alikabidhiwa jezi namba 4 yenye jina la Rage  kama ushindi dhidi ya wapinzani wao Simba.

Mara baada ya kukabidhiwa jezi hiyo, Twite alizungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa umati aliouhushuhudia uwanjani hapo ulimpa moyo wa kuona jinsi mashabiki wa Yanga wanavyomjali.

"Nimeshangaa sana kuona watu wengi kiasi hiki, hii inadhihirisha ni kiasi gani mashabiki wananijali, nami nasema sitawaangusha, jambo la muhimu ni ushirikiano tu kutoka kwao na uongozi mzima wa Yanga ili malengo yafikiwe,"alisema Twite

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni