Jumamosi, 10 Machi 2012

WANANCHI NA WANAHARAKATI WAPINGA MGOMO WA MADAKTARI.

DAKTARI mstaafu, Dk. Nyamaroko Khalfani, amebeza kitendo cha madaktari nchini kugoma, akisema daktari wa kweli na aliyekula kiapo cha kazi hiyo, hawezi kugoma, labda iwe kwa maslahi binafsi.

Dk. Khalfani aliyestaafu mwaka 2002 alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari wakati Kamati ya Wanaharakati Wazalendo ilipotoa tamko kuhusu maandamano yanayotarajiwa kufanyika kesho Dar es Salaam, kupinga mgomo huo.

Kutokana na kufahamu uzito wa kiapo cha madaktari, alisema anaungana na wanaharakati hao kupinga mgomo huo kwani ni kinyume na wajibu wa kitaaluma.

“Mimi ni daktari, nimefanya kazi sana Tarime Vijijini; kwa kweli si rahisi kwa taaluma yetu kugoma, ila kwa sababu ya maslahi binafsi ndiyo maana madaktari wa sasa wanagoma…daktari halisi na aliyekula kiapo cha kazi, si rahisi kugoma kama wanavyofanya hawa,” alisema.

Alisema madaktari wengi sasa ni vijana ambao wako kimaslahi zaidi kuliko kuzingatia wajibu na taaluma inavyowataka na ndiyo maana wanajiangalia badala ya kuangalia haki za wagonjwa ambao wanahitaji huduma ya tiba kutoka kwa wataalamu hao.

“Nawashutumu kwa hatua yao hiyo, kwani si jambo zuri na linaweza kuja kuvunja kabisa hali ya amani na usalama wa Taifa … jambo la msingi warudi kwanza kazini kuhudumia wagonjwa wakati madai yao yakishughulikiwa na Serikali ambayo imeshaonesha nia ya kufanya hivyo,” alisema Dk Khalfani.

Katibu wa Kamati hiyo, Salum Hapi, alisema maandamano hayo yataanzia Manzese Bakhresa hadi viwanja vya Jangwani na yatashirikisha wananchi wazalendo, wakiwamo wagonjwa.



Alisema madaktari hao wamesomeshwa kwa kodi za wananchi wakiwamo wagonjwa, hivyo ni wajibu wao kulipa fadhila hizo, kwa kuwapa huduma bora wananchi na kwamba kugoma kuwatibu ni kuwasaliti na ni kinyume cha viapo vyao vya kazi.

“Hatua yao ya kugoma ni unyama, tunawataka madaktari wamwogope Mungu na kutii viapo vyao na kuheshimu Watanzania waliowasomesha kwa kodi zao, kwa kurejea kazini…kama kuna mambo ya msingi ya taaluma yao yashughulikiwe kwa mazungumzo bila kuathiri wala kuhatarisha maisha ya Watanzania,” alisema.

Mkurugenzi wa Kamati hiyo ambaye pia ni Balozi wa Amani nchini, Risasi Mwaulanga, alisema kwa hali ya kiungwana, watu wanaoheshimu Dola wangepaswa kutoa fursa kwa Dola kushughulikia mapendekezo yao, ili yafanyiwe kazi badala ya kuibuka na madai mapya wakitaka mawaziri wajiuzulu.

Madaktari hao walianza mgomo mkubwa wa nchini nzima Jumatano kwa lengo la kushinikiza kujiuzulu kwa Waziri wa Afya, Dk. Haji Mponda na Naibu wake, Dk. Lucy Nkya, kama moja ya masharti ya kuendeleza mazungumzo na Serikali juu ya madai yao mbalimbali ya maslahi.

Morogoro Kiongozi wa Kituo cha Sauti ya Uponyaji, Nabii Joshua Aram, alisema watu wasio na hatia wanaopoteza uhai kwa kukosa huduma za tiba, damu zao zinalia mbele za Mungu na kwamba ili kuepuka laana ya Mungu kwa madaktari, hawana budi kurejea katika meza ya mazungumzo na Serikali ili kutafuta suluhu ya madai yao.

Alisema Watanzania wengi wanatambua hali ya uchumi wa nchi ilivyo, wakiwamo madaktari na kwamba Serikali yoyote iliyochaguliwa na watu hupenda kuendesha mambo kwa maslahi ya watu wake na kutokana na hali hiyo, madaktari wanapaswa kuwa wavumilivu katika kudai maslahi yao.

Aram alikuwa akizungunza na waandishi wa habari ambapo aliongeza kwamba ingawa madaktari hao wana madai ya msingi, lakini uamuzi waliochukua ni hatari kwa jamii ambayo inateseka sasa. Alisema nchi inaendeshwa kwa misingi ya utawala wa sheria na Mungu anataka madaktari wakubali kutumikia watu.

“Wenzetu hawa wasiangalie maslahi yao pekee ... watazame pia maslahi ya Taifa katika nyanja zingine,” alisema na kuongeza: “Mimi nafikiri tumwombe Mungu mfumo wa nchi yetu urudi katika hali yake, maadili yarejee, tutafute utatuzi wa matatizo yetu kwa njia ya mazungumzo,” alisisitiza Nabii Joshua

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni