Jumanne, 2 Julai 2013

OBAMA AHITIMISHA ZIARA YAKE AFRIKA, AWAAGA WATANZANIA NA KUAHIDI NEEMA KIBAO.



Rais Obama akiwaaga watanzania waliofika katika Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
  • Rais Obama alikuwa nchini katika ziara ya kikazi ya siku mbili ambapo ametaja vipaumbele vinne vya Marekani kwa Tanzania, ambavyo vinajumuisha miradi mbalimbali ya umeme, miundombinu ya barabara, maji na programu za kielimu kwa  vijana kwa lengo la kuongeza ajira.
Dar es Salaam. Rais wa Marekani Barack Obama amehitimisha ziara yake ya Afrika mapema leo, kwa kutembelea mradi wa uzalishaji umeme wa Symbion Ubungo, jijini Dar es Salaam.
Katika hotuba yake Ubungo, Rais Obama alielezea jinsi mkakati wa serikali yake wa kuhakikisha Afrika inapata umeme utakavyoboresha maisha ya wakazi wa bara hili.
Mapema leo asubuhi, Rais Obama aliungana na Rais wa zamani wa Marekani George Bush kuweka shada la maua kuwakumbuka wahanga wa shambulizi la kigaidi la ubalozi wa Marekani mwaka 1998.
Katika ziara yake ya siku mbili iliyoanza jana nchini Tanzania, Rais Obama amesisitiza umuhimu wa kuboshesha mahusiano ya kibiashara kati ya Afrika na Marekani. 
Wakati wa ziara yake, Obama aliahidi kutilia mkazo vipaumbele vinne vya Marekani kwa Tanzania.
Marekani itaisaidia serikali ya Kikwete kuboresha miradi mbalimbali ya umeme, miundombinu ya barabara, maji na programu za kielimu kwa  vijana kwa lengo la kuongeza ajira.
Jijini Dar es salama, Barabara za Ally Hassan Mwinyi, Mandela, Sam Nujoma na ile ya Morogoro zilifungwa kwa muda kuanzia majira ya saa tatu asubuhi huku maelfu ya wananchi wakitanda barabarani kwa lengo la kumuaga rais huyo.
Mara baada ya kufika katika  uwanja wa Ndege Rais Obama na Mkewe walitumia  muda mfupi kuagana na mwenyeji wao Rais Kikwete na mkewe ikiwa ni pamoja na kuwaaga mamia ya viongozi waliofika uwanjani hapo.
Mikakati ya Marekani Afrika
Kiongozi huyo aliwasili Dar es Salaam jana mchana ikiwa ni nchi ya mwisho katika ziara yake barani Afrika ikitanguliwa na Senegal na Afrika Kusini.
Akizungumza na waandishi wa habari pamoja na Rais Jakaya Kikwete Ikulu, Rais Obama alisema aliainisha mambo hayo wakati alipozungumza na mwenyeji wake huyo.
Alisema katika mazungumzo hayo, waligusia mradi mkubwa wa umeme uitwao Power Afrika wenye lengo la kuongeza kiwango cha umeme kinachozalishwa nchini na barani Afrika ili kupata umeme nafuu na wa uhakika utakaochagiza kuongeza uzalishaji na kukuza ajira.
Chanzo; Gazeti la Mwananchi

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni