Waziri wa Elimu Dk. Shukuru Kawambwa.
SERIKALI mwaka huu itaanza kulipa posho ya kujikimu ya Sh. 500,000 walimu watakaopangiwa na kuripoti katika maeneo yenye mazingira magumu ikiwa ni sehemu ya motisha kwao.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, aliliambia Bunge juzi kwamba utaratibu maalumu utafanyika kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi, kuainisha na kutambua maeneo yenye mazingira magumu nchini kote.
Dk. Kawambwa aliyasema hayo wakati akijibu hoja za wabunge kabla ya kupitishwa kwa Makadirio ya Matumizi ya Wizara yake, Sh bilioni 659.29 kwa mwaka huu wa fedha; Sh. bilioni 71.76 za matumizi ya kawaida; Sh. bilioni 34.43 mishahara na Sh bilioni 37.33 matumizi mengineyo.
Chini ya mpango huo wa kutoa motisha kwa walimu, Dk Kawambwa alisema nyumba 1,200 zenye uwezo wa kuchukua familia mbili kila moja, zitajengwa katika maeneo hayo ambayo hata hivyo hakutaja vigezo vitakavyotumika kuyatambua.
Alisema lengo ni walimu hao wafikie kwenye nyumba za heshima ili wapate ari ya kufanya kazi. Majibu ya Waziri yalitokana na hoja za wabunge ambao wengi wao walizungumzia suala la maslahi ya walimu huku wengine wakiitaka Serikali itafute ufumbuzi wa tatizo la baadhi yao kukataa kuripoti katika baadhi ya maeneo.
Akiendelea kutaja mikakati ya kuboresha taaluma ya ualimu, Waziri Kawambwa alisema pia Serikali imepandisha posho ya wanavyuo vya ualimu wanaokwenda kufanya mafunzo kwa vitendo kutoka Sh. 800 hadi Sh 2,000 kwa siku. Alisema posho hiyo itaendelea kurekebishwa kulingana na mahitaji.
Katika hatua nyingine, alisema Serikali itaunda bodi itakayokuwa na mamlaka ya kusimamia taaluma ya ualimu kama ilivyo kwa taaluma zingine nchini. Alisema chombo hicho, kitawajibika kusimamia taaluma na maadili ya walimu.
Ingawa Kawambwa hakusema ni lini chombo hicho kitaanzishwa, alisema kama ilivyo kwa madaktari, wahandisi na taaluma nyingine zenye bodi maalumu za usimamizi, kwa walimu, bodi hiyo itawezesha wanataaluma hao pia kuwa chini ya chombo chao.
Akizungumzia changamoto iliyotolewa na wabunge kuhusu kuimarisha Idara ya Ukaguzi, Waziri alisema Serikali inafanyia kazi ushauri huo hususan unaotaka iwepo mamlaka au wakala anayejitegemea kwa ajili ya kuendesha kitengo hicho. Alisema wameshajadili suala hilo mara nyingi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni