Ijumaa, 15 Julai 2011

KODI MACHINGA COMPLEX YAPUNGUZWA HADI ELFU KUMI.

Machinga Complex

BODI ya Jengo la Machinga Complex, Ilala, imepunguza kodi ya pango kwa asilimia 84 kutoka Sh 60,000 kwa mwezi hadi Sh 10,000 ili kuwawezesha wapangaji kulipa kwa wakati.

Aidha, imetoa siku 14 kwa wafanyabiashara wote waliopewa vizimba, lakini hawajaweka bidhaa zao, kuanza kufanya biashara vinginevyo watanyang’anywa hivyo na kupewa wafanyabiashara wengine.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari a Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Godwin Mmbaga, amesema, wamefanya uamuzi huo kutokana na hali ya maisha ya sasa ili kuwawezesha wafanyabiashara hao kufanya biashara zao kwa faida.

Amesema, jengo hilo linalopokea wafanyabiashara 4,200 mpaka sasa, lina changamoto ambazo zinatakiwa kufanyiwa kazi ukiwemo ukubwa wa kodi ambayo wafanyabiashara hao wadogo wanatakiwa kulipa ikilinganishwa na uwezo wao.

Amesema, kiwango hicho cha fedha kitakuwa kikirejewa kila baada ya miezi mitatu kuzingatia hali ya uchumi na mafanikio ya biashara kwa wafanyabiashara hao.

Akizungumzia wafanyabiashara ambao hawajaingia katika jengo hilo, amesema baada ya siku hizo kwisha, watapita na kuhakiki wafanyabiashara ambao hawajaingiza bidhaa zao na maeneo ambayo yatakuwa wazi, watapewa wafanyabiashara wengine.

“Tunaamini si watu wote wenye vizimba wataingia maana wapo waliochukua vizimba kwa matarajio tofauti na kuna watu hata mikataba yao hawajaichukua mpaka leo,” alisema Mwenyekiti huyo.

Amesema, kuhusu suala la walemavu, Bodi hiyo itahakikisha wanapewa eneo la chini kwanza huku wakiendelea kuboresha miundombinu mingine.

Hata hivyo, amesema ni matarajio ya Bodi kwamba eneo hilo litajiendesha kwa faida zaidi na kuzingatia maslahi ya wafanyabiashara na wapangaji wa eneo hilo
CHANZO; MWANANCHI

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni