Ijumaa, 15 Julai 2011

ALIYEMUUA KAKA WA RAIS KARZAI ATUNDIKWA SOKONI BAADA YA KUUWAWA.

Kisasi cha Kumuua Kaka wa Rais, Maiti Yatundikwa Sokoni


Maiti ya Sardar Muhammad ikiwa imetundikwa
Friday, July 15, 2011 3:43 AMMaiti ya mzee wa Afghanistan ambaye aliuliwa baada ya kumuua kwa kumpiga risasi kaka yake rais wa Afghanistan,Hamid Karzai, ilitundikwa sokoni kama kisasi kwa mauaji aliyoyafanya.
Sardar Muhammad alikuwa mtu aliyeaminika sana kwenye familia ya rais wa Afghanistan, Hamid Karzai.

Sardar kutokana na ukaribu wake kwa kaka yake na rais Karzai, bwana Ahmad Wali Karzai, alikuwa miongoni mwa wazee wa kikabila ambao walikuwa wakikutana na Wali Karzai muda wowote ule kujadili masuala mbalimbali.

Siku ya jumanne, Sardar mwenye umri wa miaka 40, alifika kwenye nyumba ya Wali Karzai pamoja na wazee wengine na alikuwa na faili ambalo alimtaka Wali Karzai aliangalie.

Walienda chumba cha pili wakiwa peke yao ili waweze kuliangalia faili hilo lakini hazikupata dakika nyingi Sardar alichomoa bastola yake na kumpiga risasi mbili Wali Karzai.

Walinzi wa Wali Karzai waliwahi kufika kwenye chumba hicho na kumuua kwa kumpiga risasi Sardar ambaye alikuwa akijiandaa kumpiga risasi ya tatu bwana Wali Karzai.

Walinzi hao kwa hasira na kulipa kisasi cha kuuliwa kwa bosi wao, waliitundika maiti ya Sardar kwenye mojawapo ya majengo yaliyopo kwenye soko lililopo katikati ya mji wa Kandahar. Maiti hiyo iliachwa ikining'ia hapo juu ya ukuta kwa zaidi ya dakika 20 kabla ya kuondolewa.

Jana yalikuwa mazishi ya Wali Karzai ambayo yaliongozwa na rais wa Afghanistan, Hamid Karzai.

Maelfu ya watu walijitokeza kumzika Wali Karzai lakini mazishi yake yaliingia dosari wakati mtu mmoja alipojilipua ndani ya msikiti na kuwaua watu watatu akiwemo mmoja wa maimamu wakuu wa Afghanistan, watu wengine 15 walijeruhiwa.

Taarifa zaidi zilisema kwamba mwanaume huyo aliingia msikitini wakati wa sala ya kuisalia maiti akiwa amevaa kilemba ambacho ndani yake alificha bomu alilolitumia kujilipua.

Taarifa hizo ziliongeza kuwa mwanaume huyo alifanikiwa kuingia na bomu hilo msikitini kwa kujiingiza na kujifanya yupo katika msafara mmoja na maimamu kwakuwa maimamu huwa hawasachiwi.

"Huwa tunawaheshimu watu wanaovaa vilemba, hatukukisachi kilemba chake kutokana na heshima zetu kwa watu wanaovaa vilemba, ameisaliti heshima hii kwa kuficha bomu kwenye kilemba", alisema Afisa Usalama mkuu wa Kandahar, Jenerali Mohammed Naim Momin.

Naye rais wa Afghanistan, Hamid Karzai akiombeleza kifo cha kaka yake aliwataka Waafghanistan waache kuwaua ndugu zao.

"Ni rahisi kuua na kila mtu anaweza, lakini mwanaume wa kweli ni yule anayeokoa maisha ya watu", alisema rais Karzai

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni