Jumatano, 17 Aprili 2013

WAKULIMA WA KOROSHO WASAHAULIWA

Dodoma. Serikali jana ilipata kigugumizi kueleza kama itakuwa tayari kuwalipa ruzuku wakulima wa korosho kutokana na mtikisiko wa uchumi ulioikumba dunia.


Akijibu swali bungeni Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima alisema ni wajibu wa Serikali kupambana na walanguzi na wanyonyaji kwa kuwasaidia wakulima wadogo wasidhulumiwe.

Katika swali lake la nyongeza, Mbunge wa Lindi Mjini, Salum Barwany (CUF) alitaka kujua kama Serikali itakuwa tayari kuwalipa ruzuku wakulima wa korosho kama ilivyofanya kwa watu wa kada nyingine wakiwemo wafugaji.

Kwa upande wake, Mbunge wa Kilwa Kusini, Seleman Bungara (Cuf) alihoji kama Serikali itakuwa tayari kuviagiza vyama vya ushirika vya msingi, kuacha kukopa mazao ya wakulima kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani na badala yake, viwalipe wakulima fedha zao.

“Na je, Serikali ipo tayari kuwaachia wakulima wa korosho na ufuta wauze mazao yao kwenye soko wapendalo badala ya kuwalazimisha wauze kwenye vyama vya ushirika tena kwa kukopesha,” alihoji Bundara.

Malima alisema Serikali kupitia sera ya soko huria, ina wajibu wa kuandaa mazingira ya kuwawezesha wakulima wa mazao ya korosho, ufuta na mazao mengine, kutumia taasisi zao ikiwemo vyama vya ushirika ambavyo vipo karibu nao ili wafaidike navyo.

Pia alitetea mfumo wa stakabadhi ghalani kuwa una faida kubwa kwa wakulima na kwamba ulibuniwa kwa lengo la kuondoa mfumo sugu wa kukandamiza wakulima.

Malori yakiwa katika foleni ya kupakia Korosho huko Nachingwea Lindi jana, hata hivyo wakulima wa zao hili wamekata tamaa ya kuendelea na kilimo cha zao hilo kutokana na ucheleweshaji wa malipo yao, hadi sasa hawajalipwa malipo ya pili  ya msimu uliopita ingawa korosho zinasombwa.(Picha na HansP)
Habari kwa hisani ya gazeti la Mwananchi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni