Jumapili, 7 Aprili 2013

ONA BARUA HII KWENDA KWA MAKENGEZA; ETI RUSHWA SI ADUI WA HAKI NAAHIDI KURUSHA NA KURUSHWA NA RUSHWA.

Huu mjadala wa Katiba umeanza kusisimua kweli.  Laiti tungekuwa na muda zaidi, nadhani tungejifunza mengi.  Hebu ona barua hii.
Wewe Makengeza,
Wewe kwa kweli unakuwa kipofu.  Katika kulilia mavi ya kale unashindwa kuona mazuri yaliyopo.    Si binadamu tu wanaobadilika kulingana na wakati, hata nchi inapaswa kufanya hivyo, bila unafiki, bila kificho.
Hebu tuchukue mfano wa katiba yetu iliyopitwa na wakati.  Yaani bado inatangaza kwamba tunafuata siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.  Nani anadanganyika na uongo huo?  Labda vijana ambao wanafikiri Azimio la Arusha linahusu ujenzi wa barabara mjini na kwamba ujamaa maana yake ni kusaidiana kukwapua yanayokwapulika.  
Ujamaa ni hujumaaa!  Bila kusahau kwamba kujitegemea ni kutafuta wafadhili na mafedhuli wengi iwezekanavyo kutoka nje.   Haisaidii!
Kwa hiyo, si vizuri kuendelea kuwa na maneno tata ndani ya katiba.  Lazima kuwa na dira ya kutuongoza na hata kututongoza tukubali kujitoa na kujitosa katika maendeleo ya nchi yetu changa ya macho.
Ndiyo.  Hebu angalia uchaguzi unavyoendelea kwa sasa kupata wajumbe wa mabaraza ya kata.  Ni wajumbe tu wa mabaraza ya kata wenye lengo la kutoa mawazo kuhusu katiba yetu iweje.   Lakini badala ya watu kujinadi kwamba wana mawazo haya au yale kuhusu katiba, wanatwangana ngumi kwa misingi ya makundi ndani ya chama hiki au kile.
Waliofanikiwa kuchaguliwa kwenye ngazi ya mtaa wanadaiwa rushwa ili wapite kwenye ngazi ya kata na kadhalika.   Bila kuhonga, hata nafasi ya kuchangia Katiba Mpya huwezi kupata.
Kwa hiyo, waliofikiria kwamba Katiba ni suala la kuwatafuta watu wenye mawazo chanya ili kuwa na Katiba ambayo itatulinda sisi wa kizazi hiki pamoja na vizazi vijavyo vyote wanajidanganya.   Au tuseme kwamba wanaogombea nafasi hizo za kuingia kwenye mabaraza ya kata wameelewa kitu cha msingi sana kuliko wasomi wote wanaobwatia nadharia.  Mchakato wa katiba ndiyo dira ya Katiba.  
Bila rushwa, nchi yetu haiwezi kuendelea.  Naamini kwamba wananchi wote wameelewa hivyo ndiyo maana wanaendelea kubariki mtindo huu wa kupata wajumbe na mambo mengine yote ndani ya jamii yao.  Msingi huo ni wazi pia.  Nikilinyamazia jambo fulani maana yake nimelikubali.
Kwa hiyo napenda kutangaza kwamba katika misingi ya taifa inayoorodheshwa ndani ya Katiba, itangazwe rasmi kwamba ‘Tanzania ni nchi ya rushwa na kujitafutia’.   Kwa njia hiyo,  tunakuwa mfano bora wa uwazi na ukweli na pia tunaweza kuwashughulikia watu wahafidhina kama wewe mnaotaka kurudisha nyuma maendeleo ya nchi.  
Hebu tutafakari kidogo.  Juzi, nilipanda daladala kwenda vijijini. Wakati tunaanza safari jamaa mmoja alikuwa anamcheka mwimbaji maarufu eti analalamika kwamba wimbo wake hauchezwi na kituo cha redio kwa kuwa hajatoa hela.
‘Hajui methali isemayo ‘Penya udhia tia rupia’!
Wenzake wote wakamuunga mkono.  
‘Kabisa.  Hajui kwamba hii ni Tanzania?’
‘Si ndiyo.  Hebu ona kama kuna mtu aliyemwunga mkono?  Kimyaaaa!  Mfumo ni mfumo Bwana.’
Wakati huo, tulikuwa tumekaribia kwenye mwembe mkubwa.  Dereva akamwambia konda ampatie elfu mbili sadaka ya leo.  Waliokuwemo kwenye basi wakaanza kucheka tena.
‘Heee!  Kumbe tumeshafika Mwembehongo.’
Ikabidi niulize kulikoni.   Wakanieleza kwamba hapa wanakaa wale wauguzi wa njia na kuchukua sadaka yao kwa kila gari lipitalo.
‘Sasa kwa nini mnaruhusu hali hii iendelee?  Si mtoe taarifa.’
Wakaniangalia kana kwamba nimetoka kwenye sayari nyingine.
‘Hii ni Tanzania Bwana.  We vipi?’
‘Kwani hii ndiyo maana ya Utanzania?’
‘Sasa.  Wale wasomi wenzio wanakwapua mabilioni, wewe umefanya nini? Lakini ukiona mdogo naye anajaribu kujitutumua unabisha.  Huna uzalendo wewe.’
‘Mmmh!  Kukubali kutoa hongo ndiyo uzalendo?
‘Tumeshakuambia kwamba hii ni Tanzania.  Ndiyo desturi zetu.’
‘Lakini huoni kwamba desturi hii inaua.  Angalia lile jengo lilivyoanguka.’
‘Bado bwana huelewi.  Kwanza si kosa la mtu aliyehongwa.  We ngoja tu wiki mbili kama utasikia kesi hii tena.  Ni kosa la majengo yenyewe.  Mbona majengo mengi sana yamejengwa kwa mtindo huu, lakini hayaanguki.  Nakuambia lile jengo limekosa uzalendo kabisa.  Limeanguka ili lituaibishe mbele ya dunia.’
mbali kama jengo moja linaporomoka.  
‘Kweli kabia.  Kama tungefuata sheria unavyotaka wewe, mangapi yasingeporomoshwa. Watu watakosa maghorofa hivihivi kwa sababu tu jengo moja limekosa uzalendo.’
Basi zima likakauka kucheka. Hata dereva alisahau kwamba breki zake hazifanyi kazi kidogo tuingie mtaroni.
‘We Bwana hebu shika adabu huko.  Unataka kukosa uzalendo na wewe kwa kusababisha ajali.’
‘Jamani breki zangu …’
‘Kwani kuna mabasi mangapi ambayo hayana breki.  Hebu tufikishe haraka.’
‘Ndiyo.  Umetoa sadaka huko usije ukatutoa kafara pia.’
‘Hapana.’
‘Basi nyamaza.   Huu Mwembehongo si kazi ya mwuguzi mmoja.  Ni mfumo mzima kuanzia juu hadi chini.  Wewe si unataka atoe taarifa.  Atoe kwa nani?  Kwa bosi wake?  Asipomkatia bosi wake mshiko wa kutosha, atashtuka anaongoza mabaiskeli huko Katavi ndanindani.  Kila mtu yumo kwenye mfumo.  Hii Tanzania Bwana.’
Papohapo nilielewa.  Tuache nadharia ya mambo ya haki na nini sijui.  Lazima tukubali hali halisi.  Hii ni nchi ya rushwa na Kujitafutia.   Ndiyo dira ya taifa letu.  Iwapo imefikia hali ha watu kutoa na kupokea rushwa ili waweze kutoa maoni kuhusu katiba, basi hawana budi kufagilia rushwa kwenye katiba yenyewe.
Baada ya hapo itakuwa rahisi sana kusahihisha mambo.  Kwa kuwa tutakuwa tumetamka hali halisi ya maoni ya walio wengi,  tutaweza kushughulikia wanaokwamisha.
Kwanza tunapaswa kuiga mfano mzuri wa hawa wauguzi wetu wa lami.  Mtu asipokusanya sadaka ya kujitosheleza mwenyewe pamoja na mabosi wake, anapelekwa kuliko na kulia na kusaga meno.  Vizuri sana.  Hivyo, baada ya kupitisha katiba kwamba hii ni nchi ya rushwa na kujitafutia, yeyote ambaye hatumii nafasi yake kwa ajili ya kujineemesha pamoja na mabosi wake anaweza kushtakiwa kwa kwenda kinyume cha katiba.   Katibua katiba!  Anatishia kufumua mfumo.
Vinginevyo tunaweza kuamua kuchukua hatua ndogondogo kwanza.  Kwa mfano katika sheria ya uchaguzi, inaweza kuandikwa kwamba:
Kila mgombea ana wajibu wa kutoa rushwa
Wakati wa uchaguzi ni wakati wa wananchi kuneemeka angalau kidogo, ndipo waweze kuona manufaa ya dira ya taifa ya rushwa na kujitafutia.  Ni muhimu waone hivi wazidi kusema kwamba ‘Hii ni Tanzania’ kwa kujivunia, si kwa kinyongo na unyonge.  Anapohongwa na kila mgombea, atakumbuka ladha ya pilao kwa miaka kadhaa ijayo. Tena napendekeza uchaguzi ufanyike kila miaka mitatu ili kuhakikishwa kwamba hasahau.  
Kulingana na sheria hiyo, mtu yeyote anayetambulikwa kwamba hajatoa rushwa vya kutosha (na viwango vitapangwa!) anaweza kuwekewa pingamizi na kufutwa kama mgombea au iwapo, kwa bahati mbaya alichaguliwa bila kuhonga vya kutosha, ushindi wake unaweza kufutwa na mahakama kwa mujibu wa sheria hii mpya ya uchaguzi.   
Sheria hii itatusaidia sana.  Kwanza itaondoa ulazima wa kugawa pesa sehemu za ajabu kama chooni.  Kwa nini tunashusha hadhi ya wagombea na mawakala wao?   Kwa nini wasifanye waziwazi kabisa?  Pili hatutasumbuliwa tena na waheshimiwa wanaojidai samaki wasafi ndani ya tenga lenye mnuko.  Wanuke wote, au tuseme, kutokana na sheria hii, wanukie wote kwa pamoja.
Tukishatengeneza vizuri hapo juu, viwango vitapangwa kwa kila aina ya uchaguzi, hadi viranja wa shule, uongozi wa SACCOS na VICOBA, na kadhalika.  Jumuiya za dini zijue kwamba hawana budi kufuata mkondo huo. Sote tujue kwamba ‘Rushwa ni rafiki wa haki.  Kwa maendeleo ya taifa langu, sitakataa kurusha wala kurushwa.
Chanzo; Gazeti la Mwananchi

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni