Jumatano, 24 Aprili 2013

SURVIVAL FOR CASHEWNUT TRADE; WAKULIMA WA KOROSHO WILAYA YA LIWALE WAFANYA VURUGU KUBWA KUDAI MAKATO YAO YA MALIPO YA PILI YA KOROSHO HAPO JANA.

Kanisa la Katoliki Liwale(picha HansP)
Wakulima wa zao la korosho wa Wilaya ya Liwale Mkoa wa Lindi jana kuamkia leo wamefanya vurugu kubwa ya kufunga barabara kwa magogo na kuchoma moto baadhi ya ofisi za vyama vya ushirika wa mazao baada ya kufadhaishwa nakulipwa malipo pungufu katika shilingi mia sita wanazodai kama malipo ya pili kwa kila kilo ya korosho waliyouza msimu wa 2012/2013.
Madhira haya yasipodhibitiwa kwa haraka yanaweza kuhamia wilaya zingine za Kilwa, Rwangwa na Nachingwea kwa vile kuna tatizo kama hilo la Liwale. Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Lindi ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kilwa amefunga safari mchana huu kuelekea wilayani Liwale kujaribu kupata ufumbuzi wa tatizo hilo.
Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Lindi kinalaumiwa kufanya biashara ya kuuza korosho kwa mnada kwa bei ndogo pasipo kuwashirikisha  wadau wake ambao ni vyama vya msingi vya ushirika vilivyopo mkoani hapa.

Alhamisi, 18 Aprili 2013

KATUNI TOKA KWA MASOUD KIPANYA; BORA BUNGE LIJADILIWE BILA KUONESHWA AU KUSIKILIZWA MOJA KWA MOJA NA VYOMBO VYA HABARI ILI WATOTO WETU WASIJIFUNZE MATUSI.


Credits; Gazeti la Mwananchi 19/04/2013

VIJEMBE TOKA BUNGENI JANA;MH. RAGE AMWAMBIA MH. LISSU AKASOME UPYA SHAHADA YAKE YA SHERIA NI BAADA YA KUKATAA TAARIFA YA LISSU JUU YA UHURU WA MAJADILIANO BUNGENI.

(Picha Maktaba)
Mh. Lissu jana alitolewa nje ya Bunge kwa nguvu kwa amri ya Naibu Spika Mh. Job Ndugai alipoonekana kuingilia Hotuba ya Mh. Mwigulu Nchemba jana aliyekuwa anashangaa habari ya udini imetoka wapi siku hizi baada ya miaka mingi ya utulivu chini ya utawala wa CCM!!!? Kiujumla hali ya utovu wa nidhamu imeendelea kutawala Bunge letu licha ya meza kuu kujitahidi kuidhibiti hali hiyo bila mafanikio, ni wakati wa wananchi kujitahidi kufuatilia matangazo ya vipindi vya Bunge ili tuchambue busara za Wabunge wetu hasa tukiangalia wapo kwa maslahi ya Watanzania au ya kwao binafsi!!?

Jumatano, 17 Aprili 2013

WAKULIMA WA KOROSHO WASAHAULIWA

Dodoma. Serikali jana ilipata kigugumizi kueleza kama itakuwa tayari kuwalipa ruzuku wakulima wa korosho kutokana na mtikisiko wa uchumi ulioikumba dunia.


Akijibu swali bungeni Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Adam Malima alisema ni wajibu wa Serikali kupambana na walanguzi na wanyonyaji kwa kuwasaidia wakulima wadogo wasidhulumiwe.

Katika swali lake la nyongeza, Mbunge wa Lindi Mjini, Salum Barwany (CUF) alitaka kujua kama Serikali itakuwa tayari kuwalipa ruzuku wakulima wa korosho kama ilivyofanya kwa watu wa kada nyingine wakiwemo wafugaji.

Kwa upande wake, Mbunge wa Kilwa Kusini, Seleman Bungara (Cuf) alihoji kama Serikali itakuwa tayari kuviagiza vyama vya ushirika vya msingi, kuacha kukopa mazao ya wakulima kupitia mfumo wa stakabadhi ghalani na badala yake, viwalipe wakulima fedha zao.

“Na je, Serikali ipo tayari kuwaachia wakulima wa korosho na ufuta wauze mazao yao kwenye soko wapendalo badala ya kuwalazimisha wauze kwenye vyama vya ushirika tena kwa kukopesha,” alihoji Bundara.

Malima alisema Serikali kupitia sera ya soko huria, ina wajibu wa kuandaa mazingira ya kuwawezesha wakulima wa mazao ya korosho, ufuta na mazao mengine, kutumia taasisi zao ikiwemo vyama vya ushirika ambavyo vipo karibu nao ili wafaidike navyo.

Pia alitetea mfumo wa stakabadhi ghalani kuwa una faida kubwa kwa wakulima na kwamba ulibuniwa kwa lengo la kuondoa mfumo sugu wa kukandamiza wakulima.

Malori yakiwa katika foleni ya kupakia Korosho huko Nachingwea Lindi jana, hata hivyo wakulima wa zao hili wamekata tamaa ya kuendelea na kilimo cha zao hilo kutokana na ucheleweshaji wa malipo yao, hadi sasa hawajalipwa malipo ya pili  ya msimu uliopita ingawa korosho zinasombwa.(Picha na HansP)
Habari kwa hisani ya gazeti la Mwananchi.

PICHA YA LEO; SWIMMING POOL YA KIENYEJI, MTOTO OMARI AKIOGELEA KATIKA KISIMA CHA NYUMBANI KWAO NACHINGWEA JANA.

HAKI YA KUCHEZA KWA WATOTO;Kisima hiki ni zege iliyojengwa mithili ya pipa nusu kwa ajili ya hifadhi ya maji ya akiba lakini mtoto huyu alionekana kufurahia maji haya kama yupo ufukweni, alichezea maji haya chini ya usimamizi wa wazazi wake kwa usalama zaidi.

Jumapili, 7 Aprili 2013

ONA BARUA HII KWENDA KWA MAKENGEZA; ETI RUSHWA SI ADUI WA HAKI NAAHIDI KURUSHA NA KURUSHWA NA RUSHWA.

Huu mjadala wa Katiba umeanza kusisimua kweli.  Laiti tungekuwa na muda zaidi, nadhani tungejifunza mengi.  Hebu ona barua hii.
Wewe Makengeza,
Wewe kwa kweli unakuwa kipofu.  Katika kulilia mavi ya kale unashindwa kuona mazuri yaliyopo.    Si binadamu tu wanaobadilika kulingana na wakati, hata nchi inapaswa kufanya hivyo, bila unafiki, bila kificho.
Hebu tuchukue mfano wa katiba yetu iliyopitwa na wakati.  Yaani bado inatangaza kwamba tunafuata siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.  Nani anadanganyika na uongo huo?  Labda vijana ambao wanafikiri Azimio la Arusha linahusu ujenzi wa barabara mjini na kwamba ujamaa maana yake ni kusaidiana kukwapua yanayokwapulika.  
Ujamaa ni hujumaaa!  Bila kusahau kwamba kujitegemea ni kutafuta wafadhili na mafedhuli wengi iwezekanavyo kutoka nje.   Haisaidii!
Kwa hiyo, si vizuri kuendelea kuwa na maneno tata ndani ya katiba.  Lazima kuwa na dira ya kutuongoza na hata kututongoza tukubali kujitoa na kujitosa katika maendeleo ya nchi yetu changa ya macho.
Ndiyo.  Hebu angalia uchaguzi unavyoendelea kwa sasa kupata wajumbe wa mabaraza ya kata.  Ni wajumbe tu wa mabaraza ya kata wenye lengo la kutoa mawazo kuhusu katiba yetu iweje.   Lakini badala ya watu kujinadi kwamba wana mawazo haya au yale kuhusu katiba, wanatwangana ngumi kwa misingi ya makundi ndani ya chama hiki au kile.
Waliofanikiwa kuchaguliwa kwenye ngazi ya mtaa wanadaiwa rushwa ili wapite kwenye ngazi ya kata na kadhalika.   Bila kuhonga, hata nafasi ya kuchangia Katiba Mpya huwezi kupata.
Kwa hiyo, waliofikiria kwamba Katiba ni suala la kuwatafuta watu wenye mawazo chanya ili kuwa na Katiba ambayo itatulinda sisi wa kizazi hiki pamoja na vizazi vijavyo vyote wanajidanganya.   Au tuseme kwamba wanaogombea nafasi hizo za kuingia kwenye mabaraza ya kata wameelewa kitu cha msingi sana kuliko wasomi wote wanaobwatia nadharia.  Mchakato wa katiba ndiyo dira ya Katiba.  
Bila rushwa, nchi yetu haiwezi kuendelea.  Naamini kwamba wananchi wote wameelewa hivyo ndiyo maana wanaendelea kubariki mtindo huu wa kupata wajumbe na mambo mengine yote ndani ya jamii yao.  Msingi huo ni wazi pia.  Nikilinyamazia jambo fulani maana yake nimelikubali.
Kwa hiyo napenda kutangaza kwamba katika misingi ya taifa inayoorodheshwa ndani ya Katiba, itangazwe rasmi kwamba ‘Tanzania ni nchi ya rushwa na kujitafutia’.   Kwa njia hiyo,  tunakuwa mfano bora wa uwazi na ukweli na pia tunaweza kuwashughulikia watu wahafidhina kama wewe mnaotaka kurudisha nyuma maendeleo ya nchi.  
Hebu tutafakari kidogo.  Juzi, nilipanda daladala kwenda vijijini. Wakati tunaanza safari jamaa mmoja alikuwa anamcheka mwimbaji maarufu eti analalamika kwamba wimbo wake hauchezwi na kituo cha redio kwa kuwa hajatoa hela.
‘Hajui methali isemayo ‘Penya udhia tia rupia’!
Wenzake wote wakamuunga mkono.  
‘Kabisa.  Hajui kwamba hii ni Tanzania?’
‘Si ndiyo.  Hebu ona kama kuna mtu aliyemwunga mkono?  Kimyaaaa!  Mfumo ni mfumo Bwana.’
Wakati huo, tulikuwa tumekaribia kwenye mwembe mkubwa.  Dereva akamwambia konda ampatie elfu mbili sadaka ya leo.  Waliokuwemo kwenye basi wakaanza kucheka tena.
‘Heee!  Kumbe tumeshafika Mwembehongo.’
Ikabidi niulize kulikoni.   Wakanieleza kwamba hapa wanakaa wale wauguzi wa njia na kuchukua sadaka yao kwa kila gari lipitalo.
‘Sasa kwa nini mnaruhusu hali hii iendelee?  Si mtoe taarifa.’
Wakaniangalia kana kwamba nimetoka kwenye sayari nyingine.
‘Hii ni Tanzania Bwana.  We vipi?’
‘Kwani hii ndiyo maana ya Utanzania?’
‘Sasa.  Wale wasomi wenzio wanakwapua mabilioni, wewe umefanya nini? Lakini ukiona mdogo naye anajaribu kujitutumua unabisha.  Huna uzalendo wewe.’
‘Mmmh!  Kukubali kutoa hongo ndiyo uzalendo?
‘Tumeshakuambia kwamba hii ni Tanzania.  Ndiyo desturi zetu.’
‘Lakini huoni kwamba desturi hii inaua.  Angalia lile jengo lilivyoanguka.’
‘Bado bwana huelewi.  Kwanza si kosa la mtu aliyehongwa.  We ngoja tu wiki mbili kama utasikia kesi hii tena.  Ni kosa la majengo yenyewe.  Mbona majengo mengi sana yamejengwa kwa mtindo huu, lakini hayaanguki.  Nakuambia lile jengo limekosa uzalendo kabisa.  Limeanguka ili lituaibishe mbele ya dunia.’
mbali kama jengo moja linaporomoka.  
‘Kweli kabia.  Kama tungefuata sheria unavyotaka wewe, mangapi yasingeporomoshwa. Watu watakosa maghorofa hivihivi kwa sababu tu jengo moja limekosa uzalendo.’
Basi zima likakauka kucheka. Hata dereva alisahau kwamba breki zake hazifanyi kazi kidogo tuingie mtaroni.
‘We Bwana hebu shika adabu huko.  Unataka kukosa uzalendo na wewe kwa kusababisha ajali.’
‘Jamani breki zangu …’
‘Kwani kuna mabasi mangapi ambayo hayana breki.  Hebu tufikishe haraka.’
‘Ndiyo.  Umetoa sadaka huko usije ukatutoa kafara pia.’
‘Hapana.’
‘Basi nyamaza.   Huu Mwembehongo si kazi ya mwuguzi mmoja.  Ni mfumo mzima kuanzia juu hadi chini.  Wewe si unataka atoe taarifa.  Atoe kwa nani?  Kwa bosi wake?  Asipomkatia bosi wake mshiko wa kutosha, atashtuka anaongoza mabaiskeli huko Katavi ndanindani.  Kila mtu yumo kwenye mfumo.  Hii Tanzania Bwana.’
Papohapo nilielewa.  Tuache nadharia ya mambo ya haki na nini sijui.  Lazima tukubali hali halisi.  Hii ni nchi ya rushwa na Kujitafutia.   Ndiyo dira ya taifa letu.  Iwapo imefikia hali ha watu kutoa na kupokea rushwa ili waweze kutoa maoni kuhusu katiba, basi hawana budi kufagilia rushwa kwenye katiba yenyewe.
Baada ya hapo itakuwa rahisi sana kusahihisha mambo.  Kwa kuwa tutakuwa tumetamka hali halisi ya maoni ya walio wengi,  tutaweza kushughulikia wanaokwamisha.
Kwanza tunapaswa kuiga mfano mzuri wa hawa wauguzi wetu wa lami.  Mtu asipokusanya sadaka ya kujitosheleza mwenyewe pamoja na mabosi wake, anapelekwa kuliko na kulia na kusaga meno.  Vizuri sana.  Hivyo, baada ya kupitisha katiba kwamba hii ni nchi ya rushwa na kujitafutia, yeyote ambaye hatumii nafasi yake kwa ajili ya kujineemesha pamoja na mabosi wake anaweza kushtakiwa kwa kwenda kinyume cha katiba.   Katibua katiba!  Anatishia kufumua mfumo.
Vinginevyo tunaweza kuamua kuchukua hatua ndogondogo kwanza.  Kwa mfano katika sheria ya uchaguzi, inaweza kuandikwa kwamba:
Kila mgombea ana wajibu wa kutoa rushwa
Wakati wa uchaguzi ni wakati wa wananchi kuneemeka angalau kidogo, ndipo waweze kuona manufaa ya dira ya taifa ya rushwa na kujitafutia.  Ni muhimu waone hivi wazidi kusema kwamba ‘Hii ni Tanzania’ kwa kujivunia, si kwa kinyongo na unyonge.  Anapohongwa na kila mgombea, atakumbuka ladha ya pilao kwa miaka kadhaa ijayo. Tena napendekeza uchaguzi ufanyike kila miaka mitatu ili kuhakikishwa kwamba hasahau.  
Kulingana na sheria hiyo, mtu yeyote anayetambulikwa kwamba hajatoa rushwa vya kutosha (na viwango vitapangwa!) anaweza kuwekewa pingamizi na kufutwa kama mgombea au iwapo, kwa bahati mbaya alichaguliwa bila kuhonga vya kutosha, ushindi wake unaweza kufutwa na mahakama kwa mujibu wa sheria hii mpya ya uchaguzi.   
Sheria hii itatusaidia sana.  Kwanza itaondoa ulazima wa kugawa pesa sehemu za ajabu kama chooni.  Kwa nini tunashusha hadhi ya wagombea na mawakala wao?   Kwa nini wasifanye waziwazi kabisa?  Pili hatutasumbuliwa tena na waheshimiwa wanaojidai samaki wasafi ndani ya tenga lenye mnuko.  Wanuke wote, au tuseme, kutokana na sheria hii, wanukie wote kwa pamoja.
Tukishatengeneza vizuri hapo juu, viwango vitapangwa kwa kila aina ya uchaguzi, hadi viranja wa shule, uongozi wa SACCOS na VICOBA, na kadhalika.  Jumuiya za dini zijue kwamba hawana budi kufuata mkondo huo. Sote tujue kwamba ‘Rushwa ni rafiki wa haki.  Kwa maendeleo ya taifa langu, sitakataa kurusha wala kurushwa.
Chanzo; Gazeti la Mwananchi

Jumatatu, 1 Aprili 2013

BINTI ALIYEUAWA AKITOKA DISCO HUKO NACHINGWEA AMEZIKWA KIJIJINI KWAO NAIPANGA.

Mwili wa marehemu Mariam ukiwa umehifadhiwa baada ya kugunduliwa asubuhi nje mbele ya Kanisa la Assemblies of God Nachingwea.
Bint ajulikanae kwa jina la Mariam amezikwa jumatatu iliyopita kijijini kwao Naipanga baada ya uchunguzi wa Madaktari katika Hospitali ya Nachingwea kubaini kuwa alikabwa na kusababisha kushindwa kupumua hivyo kupoteza maisha, hata hivyo kabala ya kuuawa aliingiliwa kwa kubakwa na wauaji hao na inasadikiwa marehemu alikuwa anatokea Disco katika Ukumbi wa NR ambapo mashindano ya Dansi mia mia yalikuwa yanaendelea hadi yalipohitimishwa juzi. Mkononi alikutwa na alama ya muhuri wa Ukumbi wa NR ambao wote wanaoingia hapo hupigwa muhuri huo kama alama badala ya tiketi.
Polisi wanendelea na uchunguzi wa dhahama hiyo ikiwa ni pamoja na kuwashikilia wasichana wawili ambao ni maswahiba na marehemu Mariam, Mungu aiweke pema roho ya Marehemu Mariam, Amin.

SERIKALI YATANGAZA NAFASI 1100 ZA AJIRA IDARA MBALIMBALI.

Serikali kupitia Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imetangaza nafasi za kazi 1,134 katika sekta mbalimbali za ofisi za umma.

Bendera yaTanzania

Kwa mujibu wa Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Xavier Daudi nafasi hizo za kazi ambazo zinapatikana katika tovuti ya Sekretarieti ya Ajira ya www.ajira.go.tz ni kwa ajili ya waajiri mbalimbali wa ofisi za umma.

Katibu alifafanua kuwa nafasi 949 ni kwa ajili ya waajiri walioainishwa katika ofisi za wizara, halmashauri na nyingine 185 ni za taasisi na wakala mbalimbali za Serikali.

Aidha, amewataka waombaji wote wa fursa za ajira kufungua matangazo yote mawili ya kazi na kuzingatia masharti ya Matangazo yote kama yalivyo katika lugha ya Kiingereza na Kiswahili kabla ya kutuma maombi yao Aprili 9, 2013.

Daudi alifafanua kuwa waajiri ambao watatoa ajira hizo ni makatibu wakuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Fedha, Wizara ya Mambo ya Nje ya Nchi na Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Wizara ya Maendeleo Jinsia na Watoto, Wizara ya Kazi na Ajira na Ofisa Mtendaji Mkuu Wakala wa Vipimo.

Wengine ni Makatibu wakuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Nishati na Madini, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Wizara ya Ardhi Nyumba na Makazi, Wizara ya Maji na Katibu Ofisi ya Rais Maadili.

Wengine ni Makatibu Tawala wa Mikoa ya Kagera, Iringa, Ruvuma, Mbeya, Mwanza, Shinyanga, Manyara, Dar es Salaam, Morogoro, Geita, Pwani, Mara, Kilimanjaro, Lindi, Singida, Tabora, Tanga, Katavi na Arusha; pamoja na wakurugenzi wa halmashauri za majiji na manispaa Mwanza, Iringa, Songea, Shinyanga, Morogoro, Singida, Kigoma/ Ujiji na Temeke.

Nafasi nyingine ni kwa ajili ya wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya Mufindi, Kyela, Rungwe, Mbeya, Chunya, Biharamulo, Bukoba, Muleba, Namtumbo, Songea, Morogoro, Makete, Mkuranga, Mbinga, Tunduru, Ukerewe, Sengerema, Ilemela, Busega, Maswa na Meatu.

Nyingine ni Wilaya za Shinyanga, Kishapu, Kilosa, Msalala, Rufiji, Rorya, Ruangwa, Lushoto, Mkinga, Mpanda, Monduli, Ngorongoro, Kigoma, Nachingwea, Rombo, Same, Singida, Urambo, Tabora, Babati, Mbulu, Simanjiro na Kiteto.

Pia zimo Wilaya za Handeni, Pangani, Kibondo, Chamwino Mtwara, Nanyumbu, Mpwapwa, Kongwa na Tandahimba pamoja na halmashauri za miji ya Njombe na Kibaha. Nafasi nyingine ni za Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita) na Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa).

Nafasi hizo zilizotangazwa zimegawanyika katika kada zifuatazo; Mchambuzi Mifumo ya Kompyuta daraja la II – (nafasi 10), Ofisa Vipimo II – nafasi 6, Mpima Ardhi, daraja la II (nafasi 26), Mhandisi daraja la II – Ufundi Umeme – Nafasi 9, Ofisa Mipango Miji daraja la II– nafasi 13 na Mhandisi daraja la II - Ujenzi (Nafasi 16).

Pia wanahitajika wahandisi daraja la II - Maji (Nafasi 13), Ofisa Misitu daraja la II (nafasi 7), Ofisa wa Sheria daraja la II – nafasi 3, Mtakwimu daraja la II – nafasi 8 na nyingine mbalimbali.
Credits; Gazeti la Mwananchi