Jumamosi, 14 Julai 2012

ALIYEMTEKA NA KUMJERUHI DK. ULIMBOKA AFIKISHWA MAHAKAMANI.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Suleiman Kova

ADAIWA KUWA NI RAIA WA KENYA, ALIKODIWA
Waandishi Wetu,

RAIA wa Kenya, Joshua Mulundi (21) amekamatwa na polisi jijini Dar es Salaam na kupandishwa kizimbani kwa tuhuma za kumteka na kufanya jaribio la kumuua Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk Steven Ulimboka. Mtuhumiwa huyo alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana alasiri na kusomewa mashtaka mawili na Wakili wa Serikali, Ladslaus Komanya.

Wakili Komanya alidai mahakamani hapo kuwa Mulundi ambaye makazi yake ni Murang'a nchini Kenya kuwa, mnamo Juni 26, mwaka huu akiwa eneo la Leaders Club, jijini Dar es Salaam alimteka Dk Ulimboka.

Hata hivyo, kumetokea utata wa jina, umri wake na makazi ya mtuhumiwa huyo, kwani wakati hati ya mashtaka mahakamani inasema ni Joshua Mulundi mwenye umri wa miaka 21 na mkazi wa Murang’a nchini Kenya, taarifa ya Jeshi la Polisi imesema anaitwa Joshua Mahindi mwenye miaka 31 na mkazi wa Namanga nchini Kenya.

Katika shtaka la pili, Wakili Komanya alidai kuwa tarehe hiyohiyo mshtakiwa alifanya jaribio la kumsababishia kifo Dk Ulimboka kwa kumpiga katika eneo la Msitu wa Pande eneo la Tegeta jijini Dar es Salaam, kinyume cha sheria.

Hata hivyo, mshtakiwa huyo alikana mashtaka hayo akidai kuwa makosa aliyoshtakiwa nayo siyo sahihi.

Hakimu Mkazi, Agnes Mchome alimwambia kuwa hatakiwi kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo, isipokuwa Mahakama Kuu pekee.

Hakimu Mchome aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 5,2012 itakapotajwa tena mahakamani hapo.
Taarifa ya Polisi
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi mshtakiwa huyo anajulikana kwa jina la Joshua Muhindi (31), mkazi wa Namanga nchini Kenya. Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Suleiman Kova aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa mshtakiwa huyo alikamatwa Juni 29 mwaka huu katika Kanisa la Ufufuo na Uzima lililoko Kawe baada ya taarifa kutoka kwa wasamaria wema.

Alisema raia huyo mwenye kitambulisho cha utaifa namba 29166938 kilichotolewa Oktoba 11, 2010 katika Wilaya ya Nyeri nchini Kenya, pia anamiliki hati ya dharura ya kusafiria yenye namba 0123431 iliyotolewa Juni 14, mwaka huu Namanga Kenya.
Kwa mujibu wa Kova, baada ya kuhojiwa na polisi, raia huyo alisema alikuja nchini Juni 23, mwaka huu kwa ajili ya kufanya tukio lililotokea Juni 25 mwaka huu na kwamba alijulishwa kuwa yeye na wenzake 12 ndiyo walipangwa kutekeleza tukio hilo.

Alisema raia huyo na wenzake walikuja nchini kwa ajili ya kumdhuru Dk Ulimboka, baada ya kukodiwa na mtu ambaye hakumtaja jina ambaye anaamini ni mtumishi wa Serikali.

“Baada ya kuhojiwa alidai kuwa yeye ndiye aliyehusika kumteka Dk Ulimboka na wenzake na baada ya utekaji huo wenzake waliondoka,” alisema Kova na kuongeza:

“Alisema walikuja kutekeleza tukio hilo kwa lengo la kujua ni nani anayemshawishi Dk Ulimboka na alipelekwa na mwenyeji wake asiyemtambua hadi katika hoteli moja katikati ya jiji.”

Alisema mtuhumiwa huyo na wenzake 12 wako kwenye kikundi kijulikanacho kama Gun Star chenye makao yake Iwiru Wilaya ya Thika nchini Kenya na kwamba kinaongozwa na mtu mmoja ajulikanaye kama Silencer akisaidiwa na Paft.
Alisema pia, mtuhumiwa huyo alidai kuwa, wamekuwa wakijihusisha na matumizi ya silaha na kwamba wamekuwa wakifanya matukio mengi ya kihalifu nchini Kenya.

Alisema baada ya utekaji huo, Juni 29 mwaka huu raia huyo alikwenda katika Kanisa la Ufufuo na Uzima lililoko Kawe kwa nia ya kutaka kuonana na kiongozi wa kanisa hilo Mchungaji Gwajima, lakini hakufanikiwa badala yake alionana na msaidizi wake ajulikanaye kama Joseph Marwa Kiriba.

“Alipoonana naye alimweleza kuwa yeye ni mwanachama wa Kikundi cha ‘Umafia’ na kwamba hukodiwa kufanya matukio ya kihalifu Kenya na nje ya mipaka,” Kamanda Kova alisema.

“Alikwenda katika kanisa hilo kwa ajili ya kufanya toba maana aliona alifanya kitendo cha kinyama hivyo aliona arudi ili akapate toba,” alisema.

Alisema jeshi hilo bado linaendelea na uchunguzi kwa ajili ya kuwatafuta watu wengine waliohusika na utekaji huo.
Katika hatua nyingine, jeshi hilo pia limewakamata watu wanane ambao wanadaiwa kuhusika na uvamizi wa mashamba katika eneo la Kawe.

Maandamano ya madaktari yazuia
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limepiga marufuku maandamano ya madaktari yaliyopangwa kufanyika Jumatatu ijayo kushinikiza mambo kadhaa ikiwamo kuundwa tume huru ya kuchunguza kutekwa, kuteswa na kutupwa katika Msitu wa Pande kwa Kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Steven Ulimboka.

Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Suleman Kova aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa maandamano hayo hayatafanyika kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo za kiusalama.

Alisema wamesitisha maandamano hayo kwa sababu madai ya madaktari tayari yameshashughulikiwa na Serikali.
“Tumesitisha maandamano kwa sababu tunahofia kunaweza kutokea uvunjifu wa amani maana Waislamu nao walipanga kuandamana kesho (leo),” alisema Kova.

Msimamo wa madaktari

Kauli hiyo ya Kova ilitolewa saa chache baada ya kikao cha zaidi ya madaktari 400 waliokutana katika mkutano wa dharura ulioitishwa na Chama cha Madaktari (MAT), ambako waliridhia kufanyika kwa maandamano hayo.
Katibu wa (MAT) Dk Rodrick Kabangila alisema katika kikao hicho, madaktari hao walipokea taarifa ya MAT iliyoeleza hatua zilizochukuliwa na Serikali dhidi ya wenzao waliofukuzwa.

“Madaktari wamepokea taarifa za wenzao kufanyiwa vitendo vya unyanyasaji, ikiwamo kufukuzwa katika makazi yao kwa kutumia Polisi wa Kutuliza Ghasia (FFU), kunyimwa chakula, posho na kuelezea kuwa vitendo hivyo ni vya unyanyasaji na uonevu dhidi ya taalamu na udaktari wenyewe,” alisema Dk Kabangila.

Dk Kabangila alisema kuwa, kufuatia hatua hiyo madaktari hao wamepitisha azimio la kufanya maandamano ya amani ambayo yanatarajia kushirikisha madaktari zaidi ya 800 hadi 1,000 na kutoa wito kwa wananchi wenye mapenzi mema na taaluma hiyo, kushiriki wakiwa na vitambaa vyeupe.

Akizungumzia msimamo wa polisi kuyazuia maandamano hayo, Dk Kabangila alisema uongozi wa madaktari utakutana kujadili tamko hilo la polisi.

“Tumepata barua inayozuia maandamano yetu. Barua hii imetoa sababu ambazo ni tofauti na sisi tulichoomba. Sisi (MAT) ndio tulioomba maandamano kwa ajili ya kuonyesha hisia zetu juu ya vitendo wanavyofanyiwa madaktari,” alisema Dk Kabangila.
Habari hii imeandaliwa na Geofrey Nyang’oro, Nora Damian na James Magai


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni