Kampuni inayojishughulisha na uchakachuaji wa mchanga uliobakizwa baada ya kuondoa dhahabu ijulikanayo kwa jina moja tu la MANJANJO iliyopo maeneo ya mlima Ikungu wilayani Nachingwea mkoani Lindi inalalamikiwa na wanakijiji kuwa inachafua mazingira pale dawa aina ya CYNADE inayotumika kukamata dhahabu katika hali ya kimiminika inapoingia katika vyanzo vya maji hasa wakati huu wa mvua za masika. Hali hii imezua sintofahamu kwa uongozi wa kijiji na wanakijiji halikadhalika na kupelekea wananchi kutaka Kampuni hiyo ifukuzwe kabisa eneo hilo.
Mambobado ilipata nafasi ya kutembelea eneo la mgodi ikiambatana na uongozi wa serikali ya wilaya na wawakilishi wa uongozi wa kijiji cha Ikungu ili kujionea hali halisi baada ya madai kuwa baadhi ya mbuzi walikufa baada ya kunywa maji yaliyochanganyika na dawa yenye sumu mara baada ya mkutano na wanakijiji na serikali yao ambayo wajumbe asilimia 90 walitangaza kujiuzulu nyadhifa zao kwa vile serikali haisikilizi kilio chao wakati wanaathirika na sumu. Tukiongea na mkemia wa kampuni hiyo alisema kuwa madai kuwa mbuzi wamekufa na dawa kuingia kwenye mkondo wa maji si kweli ila ni chuki za kisiasa kati ya wanakijiji kwa kulishana maneno ya uwongo ili waichukie kampuni yao.
Aliendelea kusema kuwa wao huvundika udongo uliotumika na wachimbaji wengine kama picha ya juu inavyoonesha na baadae huchanganya na maji yenye dawa iitwayo CYNADE katika mashimo maalumu yaliyojengewa kwa simenti pembeni ambapo dhahabu isiyoonekana kwa macho hujichanganya na maji yenye dawa na kuingia eneo maalumu kama inavyoonekana picha hii ya juu ambapo baadae huchangayika na makaa ya mawe na kukusanywa katika viroba na kupelekwa Mwanza kwa ajili ya kuchomwa ili kupata dhahabu halisi.
Hapa ndipo dhahabu huchanganyika na makaa ya mawe na kuopolewa tayari kwenda kuchomwa Mwanza ili kutenganisha makaa na dhahabu, baadae maji yenye dawa iliyopoa hurudishwa tena kwenye mzunguko wa kwanza na kuongezwa dawa tena iwapo imepungua. Mtaalamu alisema maji haya yaliyotumika hawayaachii ila wanayatumia tena na hayana madhara isipokuwa katika hatua ya mwanzo kabla hayajatumika, aliyashika maji haya na kunawa ingawa alisema yana madhara iwapo yataingia machoni, mdomoni au kwenye vinyweleo ambapo huduma ya kwanza itatakiwa ili kuzuia madhara.
Hapa ni maji yaliyojichuja toka kwenye udongo uliotumika na kuchanganyika na maji ya mvua ambapo walionekana vyura ndani yake wakicheza kwa maana kuwa hayana sumu, pamoja na hayo hakuna maji yanayoachiwa kuingia kwenye mkondo wa maji. Watalamu wa mazingira wametaarifiwa pamoja na wale wa madini ili waje kutatua mgogoro huu, Afisa Afya pia ametoa maelekezo ya nini kifanyike ili kuboresha miundombinu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni