SERIKALI imewalipa madai yao yote madaktari waliokuwa wakifanya mazoezi kwa vitendo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Sehemu ya moja ya majengo ya Hospitali ya Rufaa MuhimbiliFedha zilizolipwa ni jumla ya Sh milioni 826. Lakini pia imewataka madaktari wanachama wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa kiapo na kuachana na uanaharakati.
Aidha, imewataka madaktari bingwa 51 ambao hawajaripoti katika vituo vyao vya kazi katika hospitali za rufaa za mikoa na manispaa za Dar es Salaam, kufanya hivyo mara moja, wakitambua kuwa walisomeshwa na fedha za walipa kodi.
MAT pia imetakiwa kutambua kuwa uanachama katika chama hicho ni wa hiari na kwamba Mganga Mkuu nchini, Deo Mtasiwa, hataondolewa katika wadhifa huo kama madaktari hao wanavyotaka.
Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Lucy Nkya, alisema hayo jana Dar es Salaam wakati akizungumzia suala la madaktari walio katika mazoezi ya uboreshaji wa taaluma kwa vitendo Muhimbili.
Alisema hivi karibuni wataalamu 195 waliokuwa mazoezini Muhimbili waliamua kutoendelea na ratiba zao za mazoezi kwa vitendo hadi watakapolipwa posho zao za Novemba na Desemba mwaka jana. Wamelipwa jumla ya Sh milioni 826.
“Tatizo lilitokea baada ya kuchelewa kutolewa kwa fedha za posho kwa wataalamu wa sekta ya afya, Wizara ilihakikisha fedha zinapatikana haraka na wakati huo huo ikiwasiliana na wawakilishi wa wataalamu hao na uongozi wa taasisi walizokuwa wakifanyia mazoezi kuhusu jitihada zinazofanywa kutatua tatizo hilo,” alisema Dk. Nkya.
Aidha, alisema pamoja na Wizara kuwahakikishia wataalamu hao kuwa suala hilo limepatiwa ufumbuzi, bado walishikilia msimamo wa kutorudi vituoni mpaka wapokee fedha, kitendo ambacho hakikuwa cha kiungwana.
Dk. Nkya alisema baada ya hali hiyo, Wizara ilipeleka wataalamu 51 waliokuwa wakisubiri kuanza mafunzo Januari mwaka huu, ili kuchukua nafasi za wataalamu waliokataa kurejea, ili kuzuia athari ambazo zingeweza kujitokeza kwa wagonjwa. Wataalamu 60 hawakushiriki mgomo huo.
Alisema kitendo cha wataalamu hao kutoendelea na mazoezi kilisababisha uongozi wa Muhimbili kuwaandikia barua za kuwarudisha wizarani ambako ndiko ombi la kuitaka hospitali hiyo kuwapa nafasi za mazoezi lilitoka.
Aliongeza kwamba wataalamu hao wanapokuwa kwenye mazoezi huwa chini ya Wizara na ndiyo sababu Muhimbili iliwarudisha wizarani.
Dk. Nkya alisema pamoja na kulipa madai yote, Wizara ilifanya tathmini ya suala hilo na kubaini kuwa pamoja na mambo mengine, kuwapo kwa idadi kubwa ya wataalamu mazoezini, hakulingani na uwezo wa Muhimbili wa kuwapa fursa ya kufanya kazi kwa ukamilifu.
“Ili kuhakikisha wataalamu hao wanafikia malengo ya mazoezi, Wizara imeamua kuwapanga katika hospitali mbalimbali za Dar es Salaam ikiwa ni pamoja na Muhimbili, Temeke, Mwananyamala, Aga Khan, Amana na Lugalo, kwa kuzingatia uwezo wa hospitali hizo, hadi juzi idadi ya wataalamu 195 walikuwa wamepewa barua na kuripoti katika vituo walivyopangwa,” alisema Dk. Nkya.
Alifafanua, kuwa ya Muhimbili ilipokea 134,Temeke 12, Amana 19, Mwananyamala 16, Lugalo saba na Aga Khan saba pia.
Kuhusu tamko la MAT la kutoa saa 72 kwa Serikali kuwarejesha madaktari hao Muhimbili, alisema waraka huo haujawasilishwa wizarani bali waliusoma katika vyombo vya habari na kufafanua kuwa madaktari hao hawakufukuzwa, ila wamepangwa upya.
Kuhusu madaktari bingwa, alisema mwaka jana Serikali iliwapa uhamisho 61 kutokana na kupandishwa hadhi kwa hospitali za mikoa yote, manispaa tatu za Dar es Salaam na 10 za mashirika ya dini kuwa za rufaa na mikoa.
Alisema hospitali hizo zilipandishwa hadhi ili zitoe huduma za ubingwa na kupunguza upelekaji wa wagonjwa wanaohitaji huduma hizo kwenye hospitali za kanda na za kitaifa na pia kusogeza huduma karibu na wananchi, hivyo kuwataka watii mwito huo wakitambua kuwa walisomeshwa kwa kodi za wananchi.
Kuhusu kuwavua uanachama wa MAT baadhi ya viongozi wa Wizara, walisema ni hiari kwa daktari kuwa mwanachama wa chama hicho na hawalazimishwi ila hutakiwa kutekeleza majukumu yao bila kuvunja kiapo na kutochezea uhai wa binadamu.
Mgomo huo wa madaktari ulianza mwezi huu kwa lengo la kuishinikiza Serikali iwalipe malimbikizo ya stahiki zao
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni