Jumapili, 3 Machi 2013

FATOU BENSOUDA ATEMBELEA TANZANIA, NI MWENDESHA MSHTAKA MKUU WA ICC



Rais Jakaya Kikwete akiwa katika picha ya pamoja na Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Uhalifu wa Kimataifa (ICC), Fatou Bensouda alipofika Ikulu jijini Dar es Salaam 
Na Fidelis Butahe
Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Uhalifu wa Kimataifa (ICC), Fatou Bensouda, ametua nchini jana na kufanya mazungumzo na Rais Jakaya Kikwete, Ikulu Dar es Salaam.

Hatua hiyo ya ICC imekuja ikiwa ni miezi sita tangu Serikali ya Tanzania ilipopelekwa katika mahakama hiyo, iliyoko The Hague,  Uholanzi kwa madai ya kukiuka haki za binadamu.

Malalamiko hayo maalumu yalipelekwa ICC na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Septemba 28 mwaka jana, baada ya kutokea kwa mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Daudi Mwangosi na watu wengine 23.

Taarifa ya LHRC ilieleza kuwa pamoja na watu hao kuuawa, Serikali ilishindwa kuwachukulia hatua wahusika.

Mbali na kuishtaki Serikali ICC, kituo hicho cha Sheria na Haki za Binadamu pia kilipeleka mashtaka kwenye Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu.



Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho, Dk Hellen Kijo-Bisimba, alisema kuwa walifungua mashtaka hayo ili kuzitaka mamlaka hizo za kimataifa kufanya uchunguzi na kuichukulia hatua stahiki za kisheria dhidi ya Serikali ya Tanzania.

Jana Rais Jakaya Kikwete alikutana na Bensouda na kufanya mazungumzo na baadaye walipiga picha za pamoja nje ya Viwanja vya Ikulu,  akiwa pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angellah Kairuki na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Eliezer Feleshi.

Katika maelezo yake Bisimba alisema: “Tumepeleka mashtaka 24 ICC tangu Septemba 28 mwaka huu, ambayo yanahitajika kufanyiwa uchunguzi na kuchukua hatua kali dhidi ya Serikali ya Tanzania ambayo imekuwa ikiwalinda viongozi wake wanaokiuka haki za binadamu.”

“Tunatarajia kuona uwajibikaji wa viongozi wote wa Serikali na vyombo vya dola waliohusika kwa njia yoyote ile. Hatua hizo au uwajibikaji huo ni pamoja na kujiuzulu, kuachishwa kazi na kufikishwa Mahakamani,” aliongeza Dk Bisimba.

Gazeti hili lilipomtafuta Jaji Werema kuzungumzia ujio wa Bensouda alisema kuwa Mwendesha Mashtaka huyo alikuwa mgeni wa Rais Kikwete, hivyo hawezi kueleza kilichozungumzwa.

“Alikuwa mgeni wa Rais, lakini kubwa nililolisikia ni kwamba alikuja kusalimia kwa sababu tangu alipoteuliwa hakuwahi kuja Tanzania,” alisema Werema.

Kama ilivyokuwa kwa Werema, naye Feleshi  alikwepa kuzungumzia ujio huo wa Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC, huku akisema jambo hilo linaweza kutolewa ufafanuzi na Ikulu.
Kwa Hisani ya Gazeti la Mwananchi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni