Moshi. Mkurugenzi Mkuu wa zamani wa Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB), Leslie Omari, amehukumiwa kifungo cha miaka saba jela baada ya kupatikana hatia katika tuhuma zinazoangukia katika makosa ya vitendo vya ufisadi.
Mbali na kifungo hicho, Mahakama pia imemwamuru mshtakiwa kuilipa Benki ya Exim Sh330 milioni, ambazo kampuni yake binafsi ya African Consulting Group (ACGL), ilikopa kwa kutumia dhamana ya jengo la makao makuu ya TCB.
Leslie Omari
Hukumu hiyo iliyokuwa ikivuta hisia za ndugu, jamaa na marafiki wakiwamo watumishi wa TCB, ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Kobelo, huku mkurugenzi huyo akiwa haamini kilichotokea.
Hata hivyo, Hakimu Kobelo alimwachia huru mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo, Shaddy Kyambile ambaye wakati makosa hayo yakitendeka mwaka 2003, alikuwa Mkurugenzi wa Fedha wa Bodi ya Kahawa yenye makao yake makuu mjini Moshi.
Hakimu Kobelo alisema anakubaliana na utetezi wa Kyambile kuwa alielekezwa na bosi wake (Omari) kusaini nyaraka za kuidhinisha hati za Jengo la Kahawa, ili zitumike kama dhamana kuikopesha ACGL.
Mkurugenzi huyo mkuu wa zamani, ni miongoni mwa wanahisa wa ACGL, akimiliki asilimia 25 ya hisa.
“Mshtakiwa wa pili alisaini nyaraka kwa maelekezo ya bosi wake (Omari) ambaye alimwambia uamuzi wa kuidhamini ACGL ulishapitishwa na bodi ya wakurugenzi wakati si kweli,”alisema.
Akichambua ushahidi huo, hakimu huyo alisema utetezi wa Kyambile unaungwa mkono na maelezo ya kukiri ambayo Omari aliyaandika akisema yeye ndiye aliyemtaka Kyambile kusaini hati hizo.
Kyambile aliyekuwa akitetewa na wakili mashuhuri wa mjini Moshi, Godwin Sandi kwa sasa ni Mkurugenzi wa Fedha wa Mamlaka ya Uendelezaji Bonde la Ngorongoro (NCAA).
Akichambua ushahidi uliomtia hatiani mkurugenzi huyo, Hakimu Kobelo alisema ushahidi umethibitisha kuwa ni mhusika mkuu wa ACGL na alikuwa miongoni mwa watia saini benki.
Alifafanua kuwa mahakama imemtia hatiani mkurugenzi huyo mkuu kwa makosa mawili moja likiwa ni la matumizi mabaya ya ofisi na lingine la kutumia madaraka yake kujipatia manufaa.
“Japokuwa kwenye utetezi wake (Omari), alikana saini zake na mwandiko wake katika nyaraka mbalimbali, lakini teknolojia ya kisasa, imethibitisha kuwa ni saini yake na mwandiko ni wake,” alisema Hakimu Kobelo alisema katika shtaka la tatu, mshtakiwa atatumikia kifungo cha miaka mitatu na shtaka la nne atatumikia kifungo cha miaka minne. Hata hivyo, Hakimu alisema kwa kuwa vifungo hivyo viwili vitatumikiwa kwa pamoja, basi mshitakiwa atatumikia kifungo cha miaka minne jela na kuilipa Exim Bank Sh330 milioni ambazo ACGL ilizokopa. Kabla ya hukumu hiyo, Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru),Maghela Ndimbo aliiomba Mahakama itoe adhabu kali iwe fundisho kwa watumishi wengine wa umma wanaotumia vibaya madakara yao katika utumishi wa umma. Pia aliiomba Mahakama hiyo imwamuru mshtakiwa kuilipa Benki ya Exim mkopo ambao ACGL ilikopa mwaka 2003 ambao hadi kufikia mwaka 2009 umefikia Sh729.4 milioni pamoja na riba. Kabla ya hukumu hiyo, wakili aliyekuwa akimtetea mkurugenzi huyo, Elikunda Kipoko, aliiomba Mahakama impungizie adhabu mteja wake kutokana na umri, na ni baba anayetegemewa na familia. Baada ya hukumu hiyo, ndugu, jamaa na marafiki wa mshtakiwa aliyeachiwa huru, walijitokeza na kumbkumbatia kwa furaha. Kwa upande wake, Omari hakuaini kilichotokea na hivyo akalazimika kumuuliza wakili wake “Sikuelewa hivi hakimu amesema nini kuhusu mimi.’ Akiwa kizimbani baada ya hakimu tamka kuwa ametiwa hatiani, mkurugenzi huyo wa zamani wa TCB, alishika kichwa kuashiria kutoamini kwake kauli hiyo. Hukumu hiyo imeonyesha kutetemesha watu na hasa ndani ya Bodi ya kahawa Tanzania ambako baadhi ya watu walikuwa wakipiga simu mjini Moshi kutaka kujua kilichokea katika Mahakama ya Hakimu Mkazi.
Chanzo; Gazeti la Mwananchi
Chanzo; Gazeti la Mwananchi