Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo MICHEZO BBC. Onyesha machapisho yote
Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo MICHEZO BBC. Onyesha machapisho yote

Alhamisi, 11 Julai 2013

MKENYA WA KWANZA KUSAJILIWA LIGI KUU YA UINNGEREZA, NI WANYAMA.

Wanyama asajiliwa na Southampton

Victor Wanyama
Southampton imemsajili mcheza kiungo wa Celtic Victor Wanyama kwa kitita cha pauni milioni kumi na mbili na nusu.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21, ambaye alijiunga na Celtic kutoka kwa klabu ya Beerschot ya Ubelgiji mwaka wa 2011, amesaini mkataba wa miaka minne na Southampton.
Wanyama, kutoka Kenya, aliteuliwa kuwa mchezaji bora mchanga katika ligi ya Scottland mwaka uliopita na alifunga bao wakati wa mechi yao ya kuwania kombe la klabu bingwa barani ulaya dhidi ya Barcelona ambayo Celtic iliibuka na ushindi wa goli moja kwa bila.
Kiasi hicho ndicho cha juu zaidi kwa mchezaji yeyote kuuzwa nchini Scottland.
Wanyama vile vile amevunja rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kutoka Kenya kushiriki katika ligi kuu ya Premier ya England.
Kwingineko Swansea imekamilisha usajili wa Wilfreid Bonny kutoka kwa klabu ya Vitesse arnhem ya Uholanzi kwa kitita cha pauni milioni kumi na mbili kiwango ambacho ndicho kubwa zaidi kwa klabu hiyo kumnunua mchezaji yeyote.
Hata hivyo usajili huo utategemea ikiwa mchezaji huyo atapewa kibali cha kufanya kazi nchini England.
Bonny ambaye alikuwa amesaini mkataba wa miaka minne na klabu hiyo ya uholansi, alifunga magoli 21 baada ya kucheza mechi 30 msimu uliopita pekee.
Klabu ya Westham vile vile ilikuwa imewasilisha ombi la kutaka kumsajili mchezaji huyo kutoka Ivory Coast lakini Swansea ikafanikiwa kwa kutoa kiasi cha juu.

Jumatatu, 25 Februari 2013

MANCHESTER CITY WAIFUNGA CHELSEA 2-0

Man City yailemea Chelsea 

Wachezaji wa Manchester City
Mabingwa watetezi wa kombe hilo Manchester City wameandikisha ushindi mkubwa dhidi ya mabingwa wa ulaya Chelsea na hivyo kufufua matumaini yao ya kuhifadhi kombe hilo kwa mwaka wa pili, licha ya kukabiliwa na upinzani mkali kutoka wa vinara wa ligi hiyo kwa sasa Manchester United.
Mechi hiyo iliyokuwa na mashambulizi na kila aina ya vivutio baina ya timu hizo zinazomilikiwa na matajiri wawili tofauti,imemalizika kwa ushindi wa Man City wa mabao mawili kwa bila.
Mabao ya kipindi cha pili ya Yaya Toure na Carlos Tevez yalitosha kuizamisha Chelsea, na kufufua matumaini ya Man City, kutetea taji lao ambalo sasa linaonekana kuwa mikononi mwa majirani zao Manchster United wanaoongoza ligi wakiwa na tofauti ya point 12.
Mapema kipindi cha pili, Chelsea, walipata penati baada ya Demba BA, kuangushwa katika eneo la hatari na mlinda mlango wa Man City, Joe Hart, lakini penati iliyopigwa na nahodha wa Chelsea, Frank Lampard, ilipanguliwa Joe Hart na kuamsha mashambulizi zaidi ya Manchester City.
Wachezaji wa Newcastle
Yaya Toure kunako dakika ya 63 alipenyeza shuti la wastani pembeni mwa lango la Chelsea na kuwafanya Manchester City, kuongoza kwa bao moja kabla Chelsea, kufanya juhudi za kutaka kusawazisha lakini wakajikuta wanoangezwa bao la pili maraidadi kabisa lililofungwa na Carlos Tevez ambaye aliingia akitokea benchi,huku likiwa bao lake la kwanza baada ya mechi sita alizocheza bila kuifungia timu yake.
Kwingineko,katika mchezo mwingine wa leo, Newcastle wakiwa nyumbani,walitoka nyuma baada ya kufungwa bao la mapema na kuchomoza na ushindi wa mabao manne kwa mawili dhidi ya Southampton.
Mabao wa Newcastle yamefungwa na Musa Sisoko,Papis Demba Cisse,Yohan Cabaye aliyefungwa kwa mkwaju wa penati huku bao la nne watakatifu au Southampton wakijifunga.
Mabao ya Southampton yalifungwa na Morgan Scheneiderlin dakika tatu tu baada ya mchezo kuanza huku bao la pili likifungwa na Rickie Lambert.

Jumatatu, 15 Oktoba 2012

CAPE VERDE YAIHAIBISHA CAMEROON KWENYE KUWANIA KUFUZU MASHINDANO YA MATAIFA HURU YA AFRIKA.

Cameroon yabanduliwa nje

Wachezaji wa Cameroon
Wachezaji wa Cameroon
Cameroon leo imebanduliwa nje ya fainali za kuwania kombe la mataifa huru barani Afrika zitakazo andaliwa nchini Afrika Kusini, licha ya kushinda mechi yao ya raundi ya pili kwa mabao mawili kwa moja dhidi ya Cape Verde hii leo mjini Yaunde.
Cape Verde iliilaza Cameroon kwa mabao mawili kwa bila katika mechi yao ya raundi ya kwanza.
Kabla ya mechi hiyo Cameroon ilihitaji kuishina Cape Verde kwa zaidi ya magoli mawili ili kujikatia tikiti ya kushiriki katika fainali hizo.
Cape Verde ambayo imeorodheshwa nyuma ya Cameroon katika orodha ya timu bora ulimwenguni, imeandikisha historia kwa kufuzu kwa fainali hizo za kuwania kombe la mataifa huru barani Afrika kwa mara ya kwanza baada ya kuishinda Indomitable Lions kwa jumla la magoli matatu kwa mawili.
Katika mechi nyingine ya kufuzu, Ethiopia ilivaana na Sudan ambapo Ethiopia imeibuka na ushindi wa mabao mawili kwa bila.
Katika mechi ya raundi ya kwanza Sudan ilishinda kwa mabao matano kwa matatu.
Ethiopia sasa imefuzu kupitia sheria ya goli la ugenini baada ya timu hizo kufungana jumla ya magoli matano kwa matano.

Jumapili, 23 Septemba 2012

LIVERPOOL NA MAN U KUKWAANA NDANI YA OLD TRAFFORD.


Liverpool
Liverpool kucheza na Man United ugenini Old Trafford
Meneja wa klabu ya Liverpool, Brendan Rodgers, ana nia ya kuwashirikisha wachezaji wake wote mahiri katika pambano kubwa la Jumapili wakati klabu kitakapocheza katika uwanja wa ugenini wa Manchester United, Old Trafford.
Meneja huyo alifanya mabadiliko 11 siku ya Alhamisi, wakati timu yake ilipocheza dhidi ya klabu ya Young Boys, katika mechi ya ligi ya Europa, na kuiwezesha Liverpool kuondoka na ushindi.
Kati ya wachezaji waliopumzishwa wakati huo kwa misingi ya kucheza Old Trafford ni pamoja na Steven Gerrard, Luis Suarez na Joe Allen.
Man United, licha ya kutocheza vizuri sana msimu huu, walifanikiwa kuishinda Galatasaray ya Uturuki usiku wa Jumatano, na mbali na kushindwa na Everton katika mechi yao ya kufungua msimu, wameshinda mechi nyingine zote, licha ya mchezo wao wa kutovutia sana kufikia sasa.
Man U inatazamiwa pia kufanya mabadiliko kidogo katika kikosi ambacho kiliishinda Wigan, na Robin van Persie na Patrice Evra wanatazamiwa kushirikishwa katika pambano hilo la nyumbani.
Kuna mapambano mengi ya ligi kuu ya Premier ambayo mara kwa mara hutajwa kama ya kukata na shoka, lakini kati ya yote hayo, pambano la Jumapili kwa urahisi linapata sifa hizo.
Baadhi ya mashabiki wa soka nchini Uingereza wanasema uhasama kati ya Liverpool na Manchester United ulianza tangu nyakati za ujenzi wa mfereji uliokuza biashara za usafiri wa meli kutoka Liverpool hadi Manchester, na ukaanza kuzua uhasama kuanzia masuala ya kiuchumi hadi muziki, lakini zaidi kupita yote, ikawa ni uadui katika soka. Kwa hiyo, Liverpool inapocheza na Manchester United, basi hiyo ni mechi ya kusisimua sana nchini Uingereza

Jumapili, 9 Septemba 2012

FAINALI ZA AFRIKA 2013; ZAMBIA YAIFUNGA UGANDA 1-0.

Chipolopolo yailipua Cranes

Nahodha Christopher Katongo asherehekea goli.
Mabingwa wa Afrika Zambia wamewafunga Uganda bao 1-0 katika mechi iliyochezwa uwanja wa Levy Mwanawasa , mjini Ndola ,zambia, Jumamosi.
Hii ilikuwa mechi ya kuwania kufuzu kucheza fainali za kombe la Afrika za mwaka 2013, Afrika kusini.
Nahodha wa Chipolopolo Christopher Katongo alifunga goli kutokea katikati ya uwanja kipindi cha kwanza cha mchezo.
Mchezaji huyo anayesakata soka ya kulipwa nchini China alitumia mwanya wa kuzubaa kwa mabeki wa The Cranes kunasa mpira wa kurusha wa Davies Nkausu na kufurahisha mashabiki wapatao 40,000 waliohudhuria mechi hiyo.
Uganda, inasaka nafasi kwa mara ya kwanza kucheza fainali za kombe la Afrika (AFCON) tangu mwaka 1978 ilipomaliza mshindi wa pili nyuma ya wenyeji Ghana.
Timu hizo mbili zitarudiana nchini Uganda katikati ya mwezi Oktoba, mwaka huu

Jumapili, 13 Mei 2012

MANCHESTER CITY YACHUKUA UBINGWA WA ENGLAND LEO

Manchester City ikifunga mabao mawili zikiwa zimesalia dakika mbili za nyongeza mpira kumalizika, wamefanikiwa kuunyakua ubingwa wa Ligi Kuu ya Kandanda ya England kwa kuwalaza QPR waliocheza wakiwa 10 kwa mabao 3-2 katika mchezo uliomaliza msimu kwa mtindo wa kusisimua.
Wachezaji wa Manchester City wakishangilia ubingwa
Wachezaji wa Manchester City wakishangilia ubingwa
Pablo Zabaleta alikuwa wa kwanza kuipatia bao la kuongoza Manchester City kabla Joleon Lescott kufanya makosa na kumpatia nafasi Djibril Cisse kuisawazishia QPR.
Joey Barton alitolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kukwaruzana na Carlos Tevez lakini alikuwa Jamie Mackie aliyeipatia bao la pili QPR kipindi cha pili.
Huku Manchester United ikiwa imeshailaza Sunderland, Manchester City walionekana kama wangepoteza nafasi ya kuunyakua ubingwa lakini Edin Dzeko akafanikiwa kufunga bao la kusawazisha kwa kichwa na dakika moja baadae Sergio Aguero akapachika bao la ushindi lililoimaliza kabisa QPR.
Hili ni taji la kwanza la Manchester City tangu waliposhinda kombe la Ubingwa wa Ligi daraja la kwanza wakati huo mwaka 1968.
Manchester United imepoteza taji lake la Ligi Kuu ya England, licha ya kuilaza Sunderland baada ya mahasimu wao wakubwa Manchester City kuilaza Queens Park Rangers.
Bao la kichwa lililowekwa kimiani na Wayne Rooney lilioneka kama lingempatia Sir Alex Ferguson ubingwa wa Ligi Kuu ya Kandanda kwa mara ya 13 kwa kipindi chake cha umeneja kwa miaka 20.
Manchester United walikuwa wanadhani wameshinda ubingwa baada ya Manchester City kuwa nyuma kwa mabao 2-1 na zikiwa zinaelekea dakika za nyongeza kumalizika huku mashabiki wao wakianza sherehe za ubingwa.
Lakini taarifa zilizofika kwa mashabiki wa Manchester United kwamba Manchester City wamepachika mabao mawili ya haraka haraka dakika za mwisho ziliwanyamazisha mashabiki hao na wachezaji wao wakaonekana hawaamini wanachokisikia.
Arsenal imefanikiwa kupata nafasi ya tatu na watacheza Ligi ya Ubingwa wa Ulaya msimu ujao moja kwa moja baada ya kuilaza West Brom mabao 3-2, hasa kutokana na makosa ya mlinda mlango wa West Brom Marton Fulop.
Ushindi huo wa 3-2 ina maana kikosi cha Arsene Wenger kimemaliza msimu wakishika nafasi ya tatu.
Fulop alifanya makosa yaliyoipatia Arsenal bao la kuongoza dakika nne tu tangu mchezo ulipoanza kupitia kwa Yossi Benayoun lakini muda mfupi tu West Brom wakafanikiwa kusawazisha.
Lakini walikuwa Andre Santos na Laurent Koscielny waliopiatia Arsenal mabao ya ushindi kwa Arsenal.
Tottenham baada ya kuilaza Fulham mabao 2-0 imefanikiwa kumaliza ligi wakiwa nafasi ya nne lakini watajipatia nafasi ya kucheza Ligi ya Ubingwa wa Ulaya iwapo tu Chelsea itapoteza mchezo wa fainali ya Ubingwa wa Ulaya.
Emmanuel Adebayor alikuwa wa kwanza kuipatia Tottenham bao la kwanza ambapo Fulham nao walikosa nafasi nzuri ya kufunga kwa mkwaju wa Moussa Dembele kugonga mwamba.
Jermain Defoe aliithibitishia Tottenham ushindi baada ya kupachika bao la pili kutokana na mkwaju wa awali alioufumua Aaron Lennon kuwagonga wachezaji wa Fulham.

Jumamosi, 31 Machi 2012

ARSENAL YAFUNGWA 2-1 NA QPR, MAN CITY YATOKA SARE.

Arsenal hoi, Chelsea kidedea, City sare.

Manchester City walimaliza mchezo kwa mtindo wa aina yake baada ya kuwa nyuma kwa mabao 3-1 kipindi kirefu cha mchezo na kufanikiwa kusawazisha na kuwa mabao 3-3 dhidi ya Sunderland katika uwanja wa Etihad.
Mario Balotelli aliyefunga mabao mawili kwa Man City
Mario Balotelli aliyefunga mabao mawili kwa Man City

Sebastian Larsson alikuwa wa kwanza kuipatia bao Sunderland kabla Mario Balotelli hajasawazisha kwa mkwaju wa penalti kutokana na rafu aliyofanyiwa Dzeko.
Sunderland walijiimarisha kwa kupata bao la pili lililofungwa kwa kichwa na Nicklas Bendtner kabla ya mapumziko na walionekana dhahiri wangeibuka washindi baada ya bao la tatu la Larson.
Lakini Balotelli na Aleksandar Kolarov walibadili hali ya mchezo kwa kusawazsiha, ingawa Manchester City walikuwa wamepoteza rekodi yao ya kushinda uwanja wa nyumbani katika msimu huu.
Licha ya kucheza vizuri na kusawazisha, Man City wanafahamu fika iwapo Manchester United watailaza Blackburn siku ya Jumatatu, mabingwa hao mara 19 watasogea pointi tano nyuma ya City na kuendelea kushikilia usukani.
Lilikuwa pambano la kusisimua hasa dakika za mwisho ambapo Sunderland walionesha kandanda murua na kuweza kuwasumbua kwa muda mrefu wenyeji wao.
Lakini mara tu baada ya kutolewa mlinzi wa kati aliyecheza vizuri sana Matt Kilgallon na nafasi yake kuchukuliwa na Sotirios Krygiakos zikiwa zimesalia dakika 10 mpira kumalizika, wageni walionekana kuparaganyika.
QPR imefanikiwa kupata ushindi muhimu katika jitahada zao za kuepuka kushuka daraja baada ya Samba Diakite kufunga bao lake la kwanza tangu ahamie klabu hiyo na ndio lililoizamisha Arsenal na kupunguza kasi yake ya kushinda.
Adel Taarabt alikuwa wa kwanza kupata bao kwa upande wa QPR baada ya kumpita Thomas Vermaelen na kuachia mkwaju uliojaa wavuni.
Theo Walcott aliisawazishia Arsenal akiwa ndani ya sanduku la QPR na kuachia mkwaju baada ya jitahada zake za awali kugonga mwamba.
Mlinda mlango wa QPR Paddy Kenny alimnyima nafasi ya kufunga Robin van Persie wakati walipobakia wao wawili kabla ya Diakite kupachika bao la ushindi baada ya pasi kutoka kwa Jamie Mackie.
Aston Villa ikiwa nyumbani katika uwanja wao wa Villa Park ilishindwa kuhimili vishindo vya Chelsea baada ya nahodha wao Stiliyan Petrov kugundulika amekumbwa na maradhi ya saratani ya damu.
Mabao yaliyofungwa na Daniel Sturridge na Branislav Ivanovic yaliwasaidia wageni kupata ushindi wa mapema na kumiliki mpira kwa muda mrefu.
Dakika chache baadae zikawa za kuvutia baada ya James Collins kuipatia bao la kwanza Aston Villa, kabla ya Eric Lichaj kusawazisha na kufanya ubao usomeke 2-2.
Lakini sekunde 60 baadae, Ivanovic akafumua mkwaju wa karibu na kupata bao la tatu kabla Fernando Torres kumalizia kazi kwa kufunga bao la nne na la mwisho katika muda wa nyongeza.
Timu ya Everton ikiwa imeimarika ilifanikiwa kuichambua West Brom kwa mabao 2-0, kila bao likipatikana kila kipindi na hivyo kuweza kujinyanyua juu ya mahasimu wao wakubwa Liverpool katika msimamo wa Ligi Kuu ya England.
Leon Osman alikuwa wa kwanza kuifungia Everton kwa mkwaju wa yadi 20, baada ya kogongeana na Nikica Jelavic, na mpira ukamgonga Gareth McAuley wa West Bromich na kumzubaisha mlinda mlango Ben Foster.
Ni mkwaju wa chinichini wa Victor Anichebe ulizidisha furaha kwa Everton ambao wiki iliyopita waliweza kupata nafasi ya kucheza nusu fainali ya ya Kombe la FA Cup ambao kwa sasa wamejinyanyua hadi nafasi ya saba.
Nafasi nzuri waliyoipata West Brom Albion ilikuwa pale mkwaju wa chini uliopigwa na Paul Scharner ulipopanguliwa na mlinda mlango Tim Howard.
Fulham ilimaliza nuksi ya kupoteza michezo mitatu mfululizo ya ligi baada ya kujipatia ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Norwich City.
Alikuwa Clint Dempsey aliyeunasa mpira vizuri na kuutumukiza wavuni kabla mlinda mlango wa Norwich John Ruddy kushindwa kuzuia mkwaju wa Bryan Ruiz.
Hadi robo ya kwanza ya mchezo Fulham walikuwa tayari wameshaweka kibindoni mabao mawili.
Fulham mara mbili mikwaju yao iligonga mwamba kutokana na mashuti ya Dempsey na baadae Alex Kacaniklic - lakini mkwaju wa Aaron Wilbraham uliomgonga mchezaji wa Fulham kujaa wavuni na kuipatia Norwich bao la kufutia machozi.
Wigan imeendelea kuwa nafasi ya hatari ya kushuka daraja lakini imefanikiwa kusogea pointi tatu mbele na kuwa sawa na Blackburn nafasi ya 17 baada ya kuilaza Stoke City kwa mabao 2-0 kwenye uwanja wao wa DW Stadium.
Bao la kichwa kipindi cha pili la Antolin Alcaraz liliwapatia Wigan nafasi ya kuongoza.
Ryan Shawcross alipata nafasi nzuri ya kuifungia Stoke kwa kichwa lakini mlinda mlango wa Wigan Ali Al Habsi aliokoa.
Jean Beausejour aliipotezea nafasi nzuri Wigan, kabla Victor Moses kuifungia Wigan bao la pili dakika za mwisho za mchezo.
Matokeo hayo maana yake Wigan imekusanya pointi 28, sawa na QPR pamoja na Blackburn wakiwa juu yao.
Wolves imezidi kudhoofishwa baada ya kuongoza kwa bao moja ikajikuta ikipokea kichapo kutoka kwa Bolton na kujiongezea dhiki mkiani mwa ligi.
Michael Kightly aliipatia bao la kwanza Wolves wakiwa nyuma kwa pointi sita mkiani huku michezo iliyosalia ni sita kabla msimu haujamalizika.
Lakini Martin Petrov akaisawazishia Bolton kwa mkwaju wa penalti baada ya Roger Johnson kumchezea rafu Mark Davies na baadae Marcos Alonso akaipatia Bolton bao la pili na ubao kusomeka mabao 2-1 kwa Bolton.
Kevin Davies aliifungia Bolton bao la tatu kabla Wolves kupata bao la kufutia machozi dakika za mwisho kupitia kwa Matt Jarvis.
Muda unazidi kwenda kwa kikosi cha meneja wa Wolves Terry Connor ambacho hakijashinda katika mechi zake 10 zilizopita.
Connor, bado anahitaji ushindi wake wa kwanza tangu alipochukua hatamu za umeneja. Wolves waliongoza kipindi cha kwanza lakini iliwawia shida kutumbukiza mpira wavuni

Jumatano, 21 Machi 2012

MCHEZAJI WA BOLTON WONDERERS ALIYEZIMIA UWANJANI SASA APATA FAHAMU

Muamba anatambua familia


Fabrice Muamba
Fabrice Muamba sasa anaweza kutambua familia na jamaa zake na hata kuweza kujibu maswali. Hii ni kwa mujibu wa wakuu wa kilabu yake Bolton Wonderers pamoja na madaktari.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 23, pia anaweza kupumua bila usadizi wa mashine , lakini hali yake ingali mbaya kiasi cha kusalia katika chumba cha wagonjwa mahututi.
Mwamba alianguka uwanjani na kuzimia mnamo Jumamosi wakati wa mechi kati ya klabu hiyo na Spurs.
Moyo wake Ulisimama kwa masaa mawili lakini tangu hapo ameanza kuonyesha dalili za kuimarika kiafya.
Madaktari wamesisitiza kuwa hali ya Muamba sio mahututi lakini ni mbaya.
Muamba anaweza kuinua mikono yake na miguu, ingawa madaktari hawawezi kuelezea kuhusu hali yake ya baadaye kwa sasa.
Mchezaji huyo aliwahi kuchezea timu ya taifa ya Uingereza ya vijana walio chini ya umri wa miaka 21

Jumatano, 22 Februari 2012

TEVEZ AWAOMBA RADHI MANCHESTER CITY

Carlos Tevez, mshambulizi wa Manchester City, ameomba radhi kwa tabia yake isiyofaa hivi majuzi, na iliyoanza tangu alipogombana na meneja Roberto Mancini mwezi Septemba.
Carlos Tevez
Awaomba radhi Manchester City kwa makosa yake

Mchezaji huyo, mwenye umri wa miaka 28, alirudi katika klabu ya Man City wiki iliyopita, baada ya kuchukua hatua mikononi mwake, alipoamua kurudi nchini Argentina kwa kipindi cha miezi mitatu.
“Ningelipenda kuomba msamaha kwa dhati na pasipo kikwazo chochote kwa kila mtu, na kwa yoyote yule niliyemkosea kwa vitendo vyangu ikiwa nimemuudhi”, alielezea Tevez kupitia taarifa.
Wakati huohuo Tevez amefutilia mbali malalamiko aliyokuwa amewasilisha rasmi dhidi ya klabu ya Man City.
“Nia yangu sasa ni kuhusika zaidi katika kuichezea soka klabu ya Manchester City”, alisisitiza.
Baada ya kushindwa kujiunga na AC Milan ya Italia kama ilivyotazamiwa wakati wa usajili wa mwezi Januari, Tevez bila shaka alikuwa na uamuzi mgumu wa kuamua iwapo aendelee kupumzika na akicheza golf huko Argentina, ama arudi tena mjini Manchester na kujaribu kupigania nafasi yake katika timu yake.
Kuna uwezekano bado wa Tevez kuhama wakati wa msimu wa joto, lakini angalau inaelekea kwa hivi sasa uwanja wa Etihad umetulia, baada ya sokomoko iliyozushwa na mchezaji huyo.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Argentina hajawahi kuichezea City tangu mwezi Novemba, wakati meneja Roberto Mancini anadai alikataa kuingia uwanjani kama mchezaji wa zamu, na hatimaye timu kushindwa na Bayern Munich ugenini magoli 2-0 katika mechi ya klabu bingwa mwezi Septemba.
Tevez anadai kulikuwa na hali ya sintofahamu na mkorogano wa lugha, na akaeleweka vibaya.
Moja kwa moja baada ya ugomvi huo, Mancini alisema Tevez “amekwisha” kama mchezaji wa City, lakini baadaye alielezea kuna uwezekano wa mchezaji huyo kukaribishwa tena katika timu, ikiwa ataomba msamaha.

Alhamisi, 9 Februari 2012

ZAMBIA KUKUTANA NA IVORY COAST KWENYE FAINALI YA KOMBE LA MATAIFA YA AFRIKA.


Ivory Coast watakutana na Zambia kwenye fainali
Ivory Coast wameifunga Mali 1-0 na kufuzu fainali
Ivory Coast itakutana na Zambia kwenye fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya timu hizo mbili kushinda mechi zao za nusu fainali.
Ivory Coast imefuzu baada ya kuishinda Mali 1-0 katika nusu fainali yao mjini Libreville, nchini Gabon.
Bao la ushindi la Ivory Coast lilifungwa na mchezaji wa Arsenal Gervinho katika kipindi cha pili.
Awali katika mji wa Bata nchini Gabon Zambia iliibandua Ghana kutoka mashindano hayo kwa kuifunga 1-0.
Bao la Zambia lilifungwa katika dakika ya 78 na mshambuliaji Emmanuel Mayuka.
Katika kipindi cha kwanza mshambuliaji wa Ghana Asamoah Gyan alikosa kufunga penalti, mlinda mlango wa Zambia akautema nje mpira.
Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika itachezwa siku ya Jumapili mjini Libreville, nchini Gabon, mechi ambayo itatangazwa moja kwa moja kupitia Idhaa ya Kiswahili ya BBC

Jumatatu, 6 Februari 2012

GHANA NA MALI ZAINGIA NUSU FAINALI KOMBE LA MATAIFA HURU YA AFRIKA.

Ghana siku ya Jumapili ilifuzu kuingia nusu fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa kuishinda Tunisia magoli 2-1, katika muda wa ziada.

Kipindi cha kawaida cha dakika 90 kilipokwisha, timu hizo zilikuwa sare ya 1-1.
Wachezaji wa Ghana
Black Stars ya Ghana sasa kupambana na Zambia katika nusu fainali
Nahodha wa Black Stars ya Ghana, John Mensah, alifunga bao la kwanza katika mechi hiyo, katika dakika ya tisa, kabla Sabeur Khalifa kuisawazishia Tunisia kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika.
Bao la ushindi la Ghana lilifungwa na Andre 'Dede' Ayew.
Katika historia ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika, Tunisia haijawahi kuishinda Ghana.
Black Stars sasa wana matumaini ya kuendelea katika mashindano hayo na kupata ubingwa baada ya subira ya miaka 30, na watakutana na Zambia katika nusu fainali itakayochezwa uwanja wa Bata, siku ya Jumatano, tarehe 8 Februari, na ikiwa ni nusu fainali ya kwanza.
Mali na Ivory Coast nao watapambana katika nusu fainali ya pili siku ya Jumatano, katika uwanja wa Libreville.
Mali ilifuzu kuingia nusu fainali baada ya kuwashinda wenyeji Gabon 5-4 katika kupiga mikwaju ya penalti, baada ya mechi kumalizika kwa sare ya 1-1, na mabao kukosekana hata katika muda wa ziada.
Bao la Eric Mouloungui lilikuwa limewatia matumaini wenyeji Gabon, ambao mwaka huu wamekuwa wakishirikiana na Equatorial Guinea kuandaa mashindano ya mwaka huu.
Lakini kutangulia sio kufika, na Tidiane Diabate aliweza kuisawazishia Mali, zikiwa zimesalia dakika tano tu kabla ya mechi kumalizika.
Kwa kushindwa kufungana katika muda wa ziada, ilikuwa ni pigo kubwa wakati wa mikwaju ya penalti, Pierre-Emerick Aubameyang aliposhindwa kuifungia Gabon bao.
Gabon hawajawahi kufuzu kufika nusu fainali za mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika.
Idhaa ya Kiswahili ya BBC, ikishirikiana na redio washirika, itakutangazia nusu fainali kati ya Mali na Ivory Coast kutoka mjini Libreville, Gabon, katika matangazo maalum ya Ulimwengu wa Soka.
Charles Hilary vile vile atakutangazia mechi ya fainali ya mashindano hayo

Jumapili, 18 Desemba 2011

BARCELONA YATWAA UBINGWA WA VILABU DUNIANI, WAICHAPA SANTOS YA BRAZIL

Barcelona wameshinda kombe la dunia la Fifa kwa vilabu baada ya kuicharaza timu ya Santos ya Brazil kwa mabao 4-0 kwenye mchezo wa fainali uliyochezwa nchini Japan.
Barcelona mabingwa wa kandanda kwa vilabu duniani
Barcelona mabingwa wa kandanda kwa vilabu duniani


Ushindi huo umeendeleza rekodi nzuri ya klabu hiyo kwa mwaka huu ambapo wao ni mabingwa wa Ligi ya Hispania maarufu La Liga, wanashikilia ubingwa wa vilabu vya Ulaya na pia Kombe la Hispania maarufu Spanish Super Cup.
Mpachika mabao wa timu ya taifa ya Argentina Lionel Messi alifunga mabao mawili, huku mengine yakiwekwa kimiani na Xavi pamoja na nahodha na kiungo wa zamani wa Arsenal Cesc Fabregas.
Ushindi huo unathibitisha kwamba Barcelona inaendelea kusalia timu bora ya kusakata kandanda duniani.
"Tulicheza mchezo wetu kwa ukamilifu," alisema nahodha Carles Puyol. "Ulikuwa mchezo mzuri, mchezo mgumu sana na tumefurahi sana kwa matokeo haya."
Mchezo huo baina ya mabingwa wa kandanda wa Ulaya na wa Amerika Kusini mjini Yokohama ulikuwa ukitajwa kuwa kivutio kati ya Messi, anayeaminika ndiye mchezaji bora wa soka duniani na mshambuliaji hatari wa Brazil mwenye umri wa miaka 19 Neymar, ambaye anatajwatajwa huenda akajiunga na ama na Barca au Real Madrid.
Lakini haikuwa hivyo - Messi akionekana kushamiri katika mchezo huo na kutajwa mchezaji bora wa mechi hiyo na pia akapata tuzo ya mchezaji mwenye thamani kubwa katika michuano hiyo wakati Barcelena ikiweka kibindoni kombe la ubingwa wa dunia kwa mara ya pili mfululizo katika misimu mitatu.
Bao lake la kwanza alifunga kwa kuubetua mpira kama ilivyo kawaida yake na la pili alifunga kwa ustadi mkubwa baada ya kumzunguka mlinda mlango wa Santos Cabral.
Santos walibadilika na kucheza soka nzuri kipindi cha pili na Neymar nusura afunge baada ya kupatiwa pasi nzuri akiwa amebakia peke yake na mlinda mlando wa Barcelona Victor Valdes, lakini Valdes akafanikiwa kuokoa.
"Barcelona walistahili kushinda. Ni timu bora duniani na tumejifunza somo muhimu," alisema Neymar.
Timu ya Qatar ya Al Sadd, ambayo ililazwa mabao 4-0 na Barcelona katika hatua ya nusu fainali, iliwafunga mabingwa wa Japan Kashiwa Reysol mabao 5-3 kwa mikwaju ya penalti na kufanikiwa kushika nafasi ya tatu ya michuano hiyo inayofanyika kila mwaka kwa kushirikisha mabingwa wa soka wa mabara duniani