Jumapili, 4 Novemba 2012

MBUNGE WA ILALA AKAMATWA KWA RUSHWA

Mbunge Zungu wa Ilala Anaswa Akitoa Rushwa

NewsImages/6661242.jpg
Mbunge wa Ilala, Musa Zungu
Watu watano akiwemo mbunge wa Ilala Musa Zungu wamekamatwa na Taasisi ya kuzuia na Kupambana na Rushwa Mkoani Dodoma wakidaiwa kutoa rushwa kwa wajumbe wa Jumuiya ya wazazi ili wawachague.
Kamanda wa Taasisi hiyo Eunice Mmari alisema Zungu alikamatwa katika Hotel ya Golden Crown majuzi kati ya saa mbili na nusu na saa tatu usiku.

Eunice alisema baa ya taasisi yake kupata taarifa hizo walianza kumfuatilia kwa karibu mgombea huyo na ndipo walipomsikia akitoa maagizo kupitia simu ya mkononi kuagizia nani apewe kiasi gani.

Alisema baada ya hatua hiyo TAKUKURU walianza kumfatilia Zungu na ndipo waligundua kuwa yupo katika gari ndogo aina ya Toyota Mark –II huku akifuatana na gari jingine aina ya Prado ambalo ndiko fedha na wapambe wake walikuwa wamepanda.

Alisema baada ya kulisimamisha gari hilo alilokuwemo Zungu ghafla Prado hilo liliweza kutoroka na kumuacha Zungu na ndipo alipokamtwa na kuhojiwa.

Alisema hata hivyo TAKUKURU waliweza kufuatilia mitandao ya simu na kisha kubaini kuwa fedha hizo zilikuwa zikigawiwa na mmoja wa wakala wake ambaye naye kwa sasa amekamtwa.

Kamanda huyo aliwataja wengine waliokamatwa na Zungu ni pamoja na Yahya Khamis Danga , Busulo Mohamed Pazi na Famik Joseph Mang’ati.

Alisema kwa sasa watuhumiwa hao wote wameachiwa kwa dhamana huku uchunguzi zaidi ukiendelea na watafikishwa mahakamani mara baada ya kukamilika.

Aidha kamanda huyo alisema mwingine aliyekamtwa ni pamoja na Fatuma Kasenga ambaye ni mwenyekiti wa jumuiya ya Wazazi kutoka Mkoa wa Mbeya.

Alisema mwenyekiti huyo alikamatwa usiku wa kuamkia juzi, saa tisa usiku katika hoteli ya Kitoli mjini hapa akiwanunulia wajumbe wake chakula.

Kamanda huyo apia alisema kuna taarifa zaidi ambazo zinamtaja Alhaji Abdalah Bulembo kuwa naye amekuwa akitajwa sana katika utoaji huo wa rushwa.

Alisema hata hivyo wanaendelea na uchunguzi dhidi ya tuhuma za Bulembo na wamepata taarifa za awali kuwa anatoa rushwa hizo nyumbani.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni