Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo BUNGE. Onyesha machapisho yote
Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo BUNGE. Onyesha machapisho yote

Jumanne, 23 Agosti 2011

BUNGE LAHAIRISHWA BAADA YA KIFO CHA MBUNGE

MBUNGE wa Bunge la Tanzania kupitia Baraza la Wawakilishi, Mussa Khamis Silima (60), amefariki dunia leo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam.
Marehemu Hamis Mussa Silima.


Mbunge huyo wa jimbo la Msufini na familia yake walipata ajali ya gari juzi usiku Nzuguni mkoani Dodoma, mkewe, Mwanaheri Twalib (48) alikufa papo hapo, amezikwa jana Zanzibar.

Spika wa Bunge, Anne Makinda amewatangazia wabunge kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii , Blandina Nyoni amemuarifu kuwa Silima ameaga dunia.
Gari waliyokuwa wanasafiria.


Makinda ameahirisha shughuli za Bunge hadi kesho saa tatu asubuhi ili kutoa fursa kwa wabunge kuomboleza kifo cha mwenzao.

Leo asubuhi baada ya dua ya kuliombea Bunge na kuiombea nchi yetu, Makinda aliwaeleza wabunge kuwa, alizungumza na Silima, na kwamba alikuwa anaendelea vizuri.

Baada ya taarifa hiyo ya Spika kuhusu kifo cha Mbunge huyo, wabunge walisimama kwa dakika moja kumbuka marehemu Silima.

“Mwenyezi Mungu aipumzishe roho yake mahali pema peponi, amina” amesema Spika wa Bunge na kuitaka Kamati ya Uongozi ya Bunge na Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii wakutane kuzungumzia ushiriki wa Bunge katika msiba huo.

Makinda, jana aliwatangazia wabunge kuwa, Mbunge huyo na wenzake walipata ajali saa mbili kasorobo usiku, Silima aliumia, akalazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma. Kwa mujibu wa Makinda, Silima alipata majeraha makubwa.

Kwa mujibu wa Makinda, Mbunge na familia yake walikuwa wanarudi Dodoma wakitoka Zanzibar kumzika kaka wa mke wa Mbunge huyo.

Gari lililopata ajali aina ya Toyota Corolla liliharibika vibaya, lilivutwa juzi usiku likiwa halina baadhi ya matairi, lipo kwenye kituo kikuu cha Polisi Usalama Barabarani Mkoa wa Dodoma.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Zelothe Stephen, gari alilokuwa akisafiria Silima liligongana na magari mengine mawili saa 2.15 usiku katika barabara kuu ya Dodoma- Morogoro nje kidogo ya manispaa ya Dodoma.

Kamanda huyo amesema, gari hilo lenye namba za usajili T.509 AJC lilikuwa likitoka upande wa Morogoro kuelekea mjini Dodoma, kulikuwa na watu wanne ndani ya gari hilo akiwemo aliyekuwa akiliendesha, Chezard Sebunga (31), mkazi wa Chinangali Manispaa ya Dodoma, Silima, Mwanaheri mkazi wa Zanzibar, na Salama Juma (50) mkazi wa Area ‘D’ Manispaa ya Dodoma.

Gari hilo liligonga lori lenye namba T. 330 AYF aina ya Isuzu likiwa na tela lenye namba za usajli T. 673 ATS upande wa kulia kwenye gurudumu la nyuma kabisa kulia na kuyumba kisha kugonga lori linguine aina ya Scania lenye namba za usajili T. 497 ASW lililokuwa likitoka mjini Dodoma kuelekea Morogoro.

Kwa mujibu wa Polisi, chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa gari alilokuwa akisafiria Mbunge huyo kwa kuwa hakuwa mwangalifu wakati akitaka kulipita gari lililokuwa mbele yake akiwa katika mwendo kasi

Jumatano, 6 Julai 2011

KUMBE WATUHUMIWA WA RADAR YA TANZANIA SIO CHENGE NA DK. RASHID!!!!? NI HAWA HAPA; SAILESH VITHLAN-DALALI, JONATHAN CALLMAN-MENEJA BIASHARA BAE NA CHRISTOPHER-MENEJA MASOKO BAE SYSTEMS.


Sailesh Vithlan

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Mathias Chikawe amesema Mbunge wa Bariadi Magharibi, Endrew Chenge (CCM), hahusiki kwa namna yoyote na kashfa ya uuzaji wa rada liyoligharimu Taifa pauni milioni 28 ambazo sasa Serikali inataka zirejeshwe.

Mbali na Chenge ambaye pia anatakiwa kujivua gamba ndani ya chama chake kwa kashfa hiyo, Chikawe alisema bungeni jana kuwa, hakuna Mtanzania hata mmoja anayetuhumiwa kwa hilo ndio maana hawajamshitaki mtu.

Akitoa majumuisho ya hotubaya Ofisi ya Rais Utawala Bora, Chikawe alisema Serikali ililiita Shirika la Serious Fraud Office (SFO) la Uingereza kuja kumchunguza Chenge kwa kushirikiana na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) na katika uchunguzi
huo, Chenge hakukutwa na hatia.

Aliwataja wahusika kuwa ni Sailesh Vithlan, dalali wa rada hiyo Jonathan Callman, Meneja Biashara wa Kampuni ya BAE Systems ya Uingereza iliyouza rada hiyo na Meneja Masoko wa kampuni hiyo, aliyejulikana kwa jina moja la Christopher.

"Kama kuna mtu ana ushahidi dhidi ya Chenge au mtu mwingine atupe na tutampeleka mtuhumiwa huyo mahakamani kesho.

"Kama hakuna, basi tufanye kama kanisani (wakati wa kufunga ndoa) kuwa yeyote mwenye neno naye (Chenge), aseme sasa na kama hakuna basi kila mtu anyamaze," alisema Chikawe.

Alifafanua kuwa Serikali haijamshitaki Chenge wala mtu yeyote na kufafanua kuwa haiwezi kwenda mahakamani kwa hisia na hata wanasheria wanafahamu hilo.

Hii ni mara ya tatu kwa Chenge kusafishwa na tuhuma hizo; mara ya kwanza aliyekuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utawala Bora, Sophia Simba alikaririwa akisema kuwa Chenge alisafishwa na SFO.

Mara ya pili, Chenge mwenyewe alijitokeza mbele ya vyombo vya habari alipokuwa akigombea nafasi ya Spika wa Bunge na kufafanua kuwa SFO na Takukuru walimsafisha baada
ya kukosa ushahidi dhidi yake.

Lakini Ubalozi wa Uingereza ulitoa tamko kuwa suala hilo halijakamilika wala halijafikiwa muafaka na Chenge hakupaswa kudai kuwa hana hatia.

Hata hivyo wakati wa Kamati ya Matumizi Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lissu alisimama na kusema anayo barua inayoonesha kwamba Andrew Chenge na Dk.
Idris Rashid walihusika katika ununuzi wa rada hiyo na Chenge alipata dola milioni 1 alizopeleka katika akaunti iliyopo nje ya nchi na Dk. Rashid alipata pauni za Kiingereza
laki sita.

Hata hivyo Waziri Chikawe alisimama na kusema kwamba aliwaomba wabunge kama wana ushahidi dhidi ya Chenge waulete ili waende mahakamani hata kesho na akaomba Tundu Lissu ampatie ushahidi huo.

Lakini Lissu alisema ushahidi huo ni barua kutoka SFO kwenda kwa Mwanasheria Mkuu wa Tanzania na hivyo Serikali isiwahadae wananchi kwa sababu wanao ushahidi.

Kashfa hiyo hiyo, itakumbukwa kuwa ilichangia Chenge kujiuzulu nafasi yake kama Waziri wa Miundombinu baada ya kutuhumiwa kumiliki fedha zilizodaiwa kuwa mgawo wake katika uuzaji wa rada; dola milioni moja, zaidi ya Sh bilioni moja nje ya nchi.

Lakini jana kabla ya kutangazwa kuwa Chenge hana hatia, Serikali ilitupiwa zigo la kuwachukulia hatua za kisheria Watanzania waliohusika kupora fedha za umma katika ununuzi wa rada katika Mahakama ya Tanzania kwa kuwa katika Mahakama ya Uingereza, watuhumiwa hao hawatakuwa na hatia.

Ujumbe wa Bunge uliokwenda Uingereza kuwakilisha Watanzania kudai fedha hizo maarufu 'chenji' , umeweka wazi kuwa Kampuni ya BAE Systems inayotuhumiwa kushirikiana na watuhumiwa wa Tanzania katika uporaji huo na SFO, wameweka mazingira ya kutoshitakiwa kwa watuhumiwa hao huko Uingereza.

Wakizungumza baada ya kukabidhi ripoti ya kazi waliyoifanya huko Uingereza kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda, wajumbe hao walioongozwa na Naibu Spika, Job Ndugai, walisema wamefanikiwa kushawishi Waingereza kuona umuhimu wa fedha hizo pauni milioni 29.5, kurudishwa kupitia Serikali ya Tanzania.

Lakini pia waliituhumu kampuni hiyo na SFO kwa kupanga mazingira hayo ya kutoshitakiwa kwa watuhumiwa kwa kutumia mwanya wa mazungumzo nje ya Mahakama.

Ndugai alisema baada ya SFO kuishitaki kampuni hiyo, kampuni hiyo iliomba mazungumzo nje ya Mahakama na yalipokamilika, Mwanasheria wa kampuni hiyo, ambayo ndiyo mtuhumiwa, alitengeneza makubaliano ya mazungumzo hayo na kuzuia watuhumiwa wasishitakiwe na kuyasajili mahakamani.

Ndugai alisema kuwa mwanasheria huyo alihakikisha anailinda kampuni hiyo na watuhumiwa wengine.

"Kwa kweli jaji aliyetoa hukumu ile, alikuwa na 'moral pressure' msukumo wa kibinadamu, akaona gharama za kesi ni kubwa akasema nitapunguza gharama za kesi na kuongeza katika tuzo itakayopewa Watanzania," alisema Ndugai.
Mh. Andrew Chenge

Dk. Idris Rashid

Alifafanua kuwa katika hilo, badala ya kuamuru fedha nyingi ziwe gharama za kesi hizo ambazo zingetumiwa na SFO au kampuni hiyo; jaji huyo alitoa pauni laki tano tu kama
gharama za kesi na pauni milioni 29.5 akaamuru zirejeshwe kwa Watanzania walioibiwa.http://www.habarileo.co.tz/

MJUE MH. TUNDU LISSU


TUNDU LISSU: Mpambanaji aliyeuanza uanaharakati utotoni

Godfrey Dilunga Juni 8, 2011


Alimchachafya Mkapa kuhusu Rufiji Delta, Bulyanhulu

Asema historia yake na Tarime inaanzia mbali


Mpaka sasa amewasaidia wana Tarime 366 kutoka gerezani


JUNI 3, mwaka huu, Mwandishi Wetu, Godfrey Dilunga, alifanya mahojiano kuhusu masuala mbalimbali na Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA) ambaye pia ni mwanaharakati wa haki za binadamu, Tundu Lissu, jijini Dar es Salaam. Yafuatayo ndiyo yaliyojiri kwenye mahojiano hayo.


Raia Mwema: Tuanze na historia yako kwa muhtasari.

Lissu: Niliishi maisha ya furaha sana ya utoto. Tangu nikiwa shule ya msingi ni kama vile nilikuwa mwanaharakati. Unajua shuleni kuna shughuli nyingi sana kama kuchota maji kwa ajili ya walimu, kulima mashamba ya walimu na kupanda. Nilikuwa nikiona haya mambo hayako sawa, lakini pia kuna suala la kuwahi shuleni.

Sikumbuki kwa miaka saba ya shule ya msingi, kama kuna siku nimewahi zile namba. Siku zote nilikuwa mchelewaji na nimechapwa kweli.

Raia Mwema: Ni ukaidi wa makusudi?

Lissu: Siwezi kusema ni makusudi, lakini tatizo ni kuamka alfajiri saa 11 ili saa 12 niwe shuleni. Kwa hilo nilikuwa rebel (muasi). Pia sikumbuki mahali ambako sikuwahi kubishana na walimu iwe primary school, secondary school, iwe chuo kikuu, siku zote imekuwa hivyo.

Lakini vile vile nilizaliwa katika familia ambayo mijadala ya kisiasa ilikuwa sehemu yetu. Baba yangu alisoma hadi darasa la sita, mama yangu hakusoma kabisa.

Kila jioni tunasikiliza kwanza taarifa ya habari na idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani; baada ya hapo ni mjadala mpaka saa tano au sita, mjadala wa kisiasa kuhusu mwenendo wa mambo duniani. Nilikuwa mtoto mdogo sana, lakini nilikuwa na ufahamu.

Nafikiri nilikuwa miaka sita au saba hivi.

Wakati nikiwa darasa la kwanza (1976), nilikuwa nafahamu karibu viongozi wote duniani na miji mikuu mashuhuri.

Raia Mwema: Kutokana na ufahamu huo, ni viongozi gani hapa nchini walikuvutia wakati huo?

Lissu: Ni swali gumu kidogo. Si rahisi sana kusema nilivutiwa na Mwalimu Nyerere. Ukweli ni kwamba hapana, alikuwa sehemu ya mazungumzo ya kisiasa nchini. Siwezi nikasema nilivutiwa sana na Mwalimu.

Raia Mwema: Unaposikia jina la Julius Nyerere kwa sasa, unakumbuka nini?

Lissu: Ni hotuba za Mwalimu Nyerere kuhusu vita dhidi ya Uganda. Wakati huo nikiwa darasa la tatu mwaka 1978, nchi iko vitani tulichangishwa (familia) ng’ombe.

Baba yangu alitoa ng’ombe watatu kama sikosei ili kusaidia vita mpakani. Shuleni tuliimbishwa sana nyimbo kwamba Iddi Amini ni nyoka; ingawa baadaye nimekuja kugundua kwamba inawezekana kuna vitu vingine vingi hatukuambiwa kuhusu mgogoro wetu na Uganda.

Nakumbuka pia wakati huo tukiwa wadogo tulichimbishwa mahandaki. Nilikuwa na miaka 10, nilishangaa tunachimba (mahandaki) nje ya nyumba yetu halafu siyo marefu sana.

Lakini kuna kitu kingine kilichotafsiri mtazamo wangu kuhusu serikali ambao sio chanya sana. Nilipokuwa miaka kama sita hivi, nyumba yetu na wanavijiji wengine zilibomolewa halafu tukaachwa tu. Kina mama wanalia, kila mtu analia; halafu hawa watu wakavunja nyumba wakaondoka.

Raia Mwema: Hao wavunjaji walitumwa na nani?

Lissu: Unajua ukiwa na miaka 10 huulizi sana. Ni tukio ambalo haliwezi kuondoka katika kumbukumbu zangu kwamba; serikali inaweza kufanya vitu visivyo na akili (mantiki).

Sisi na wanakijiji wengine tumejenga nyumba, ingawa pengine hazikuwa nzuri sana wao (serikali) wametubomolea kwa jina la Operesheni Vijiji.

Baba yangu alikuwa Mwenyekiti wa Kijiji wakati huo, baadaye (watendaji wa serikali) wakaja na kamba za katani na wataalamu ili kupima namna ya kujenga nyumba za kisasa, wanaita maendeleo.

Kwa hiyo, wazee wanatembea na kamba ya katani wanapima namna ya kujenga nyumba za kisasa , zijengwe kwa mstari ulionyooka. Lakini hatimaye hawakutujengea wala kutusaidia chochote.

Hali hiyo ilinifanya niamini kwamba pengine serikali haina watu wenye akili sana kama nilivyokuwa nikifirikia mwanzoni.

Raia Mwema: Ukiwa katika umri wa utoto, unakumbuka nini enzi za nchi kufunga mikanda na baa la njaa lililowahi kutokea?

Lissu: Kuna njaa ya mwaka 1974 serikali ilileta chakula kudhibiti njaa hiyo, nakumbuka kuna kitu (chakula) kinaitwa burga ilikuwa sijaanza shule baadaye tukaletewa ugali wa muhogo. Sisi kwetu tunakula muhogo wa kuchemsha. Ilikuwa hali tofauti.

Raia Mwema: Tueleze safari yako kielimu, ilikuwaje...ngumu au nyepesi tu.

Lissu: Wakati wa Operesheni Vijiji ilitokea mvutano wa kuhama. Baba yangu pamoja na wazee wengine walisafiri kutoka kijijini Singida wakaja Dar es Salaam kulalamika.

Walilalamika kwamba tunatakiwa tuhame kwenye kijiji chenye mashamba makubwa. Wakaja kupiga kelele na serikali wakati huo iliwasilikiza.

Lakini ikaibuliwa hoja kwamba; tuhame (kijiji) kwa sababu hakuna shule. Wakati ule, hoja ya vijiji vya ujamaa ililazimisha kuwapo huduma za kijamii.

Sasa ili kukabili hoja hiyo na tusiweze kuhamishwa, kuna mzee mmoja alijenga nyumba yake mpya, akasema sitahamia ili iwe shule ya watoto. Kwa hiyo, tukaanza shule lakini shida walimu.

Mmoja wa wadogo zake baba yangu wakati huo alikuwa amemaliza darasa la saba, hana pa kwenda, wakasema atakuwa mwalimu. Kuna mama mwingine mjanja mjanja kijijini, naye wakamwambia atakuwa mwalimu.

Kwa hiyo, tukaanza darasa la kwanza Aprili 5, 1976. Shule za miaka ile zilikuwa zinaanza Januari, lakini ya kwetu tulianza Aprili, kwenye nyumba ya tembe sio ya bati, na walimu wasio na mafunzo yoyote.

Hatukuwa na vitabu, swali likawa tutaandikia nini? Wazee wakachanga hela wakamtuma mtu Dar es Salaam aende kumtafuta mtu anaitwa Abdallah Nungu, amueleze tatizo la vitabu shuleni.

Kwa hiyo, tukamsuburi kwa wiki mbili huyu bwana alete vitabu. Akarudi na boski kubwa la vitabu na vile vibao vya kuandikia, ingawa awali tulikuwa tukiandika chini (ardhini). Hivyo ndivyo tulivyoanza shule wengine.

Lakini hilo lilikuwa darasa la kwanza kwenye hiyo nyumba ya mzee. Tatizo likajitokeza ni darasa la pili litakaa wapi, kwa sababu ilibidi darasa la kwanza wengine waanze.

Nyumbani kwetu baba alijenga nyumba jirani na mdogo wake, lakini huyo mdogo wake hakuwa akiishi hapo kijijini alikuwa Moshi, nyumba yake haikuwa ikikaliwa.

Mzee akasema darasa la pili hilo hapo (nyumba ya mdogo wake). Kwa hiyo, darasa la pili tukahamia kwetu (nyumbani). Natoka mlango huu, naingia mlango wa pili niko darasani. Baada ya hapo, tukaanza ujenzi wa shule ambayo ikaitwa Shule ya Msingi Mahambe.

Raia Mwema: Serikali haikutoa mchango wowote katika hatua za awali za ujenzi?

Lissu: Hatukusaidiwa na serikali katika ujenzi. Ilikuwa asubuhi tunakwenda shule, saa nane tunaporudi (shule) tunabeba vibuyu na ndoo za maji pamoja na mama zetu kupeleka eneo la kufyatulia matofali; shughuli iliyokuwa ikifanywa na baba zetu.

Mwaka mzima tumefyatua matofali na baadaye kuanza ujenzi. Kule kwetu kuna Wakatoliki wengi, pale eneo la ujenzi (wa shule) kulikuwa na padre anapita kwenda kusalisha kijiji cha jirani kila Jumatano. Kila akipita anakuta ujenzi unaendelea na watoto wanasaidia.

Huyo padre anaitwa Charles ni mu-Irish, kila siku anapita pale anakuta watoto na wazazi wanafanya kazi, nadhani alikuwa akijiuliza kuna nini?

Siku hiyo akasimama. Alikuwa anatumia pikipiki kubwa....sijui ni kubwa (pikipiki) kweli au mimi ndiye nilikuwa mtoto na kuiona kubwa.

Akauliza, akaambiwa tunajenga shule. Akauliza serikali iko wapi? Akaahidi tukishamaliza ujenzi, ataleta mafundi kukamilisha kwa kuweka bati, ikaitwa Shule ya Wazazi.

Darasa la tatu tukaingia sasa kwenye darasa zuri na bora. Kuanzia hapo, kila mwaka nilipokaa pale shule ya msingi tulikuwa tunajenga darasa moja moja, hadi tulipomaliza mwaka 1979 tunaingia darasa la tano ndiyo kwa mara ya kwanza ikaitwa Shule ya Msingi Mahambe, na tutakaletewa mwalimu wa serikali.

Kwa hiyo, kati ya vyuo vikuu vyangu, chuo kikuu cha kwanza ni hicho....miaka minne ya kufundishwa na walimu wasio na mafunzo yoyote.

Siku hizi nikipita nikiwaambia watu shule niliyosomea na walimu walionifundisha, hawaamini. Tulifundishwa na wanakijiji kabisa wasio na mafunzo! Serikali ilipoanzisha mpango wa UPE wale walimu walijiendeleza, wakaenda vyuoni na wapo ambao wamekuwa waalimu wanataaluma.

Raia Mwema: Hayo ni ya shule ya msingi, tueleze ya sekondari, unakumbuka nini hasa?

Lissu: Cha kwanza nimetoka nje ya kwetu (Singida), nimeenda kusomea Ilboru Sekondari, Arusha. Pale (Ilboru) maisha yalikuwa mazuri na nilikuwa mdogo kuliko wengine wote (wanafunzi).

Sikuwahi kuwa kiongozi shuleni, na sikutaka uongozi. Viongozi wakati ule tuliwaita manyoka kwa sababu wanapeleka habari kwa walimu.

Lakini baadaye nilipoingia kidato cha tano na sita, Galanos Sekondari (Tanga), nilipewa uenyekiti wa Kamati ya Taaluma, lakini baada ya miezi sita hivi nikagombana vibaya sana na mwalimu wa taaluma, ikabidi nivuliwe madaraka.

Raia Mwema: Mlitofautiana katika jambo gani na mwalimu wa taaluma?

Lissu: Ni msimamo tu. Ilitokea kwamba mwaka 1988 niko kidato cha sita, sasa kidato cha nne na cha sita kila mwaka hufanya graduation (mahafali). Wakati huo, hasa Galanos na shule nyingi za sekondari, disko hazikuwa nyingi (mara kwa mara) kama sasa.

Kipindi cha kwenda kucheza disko ilikuwa wakati wa graduation. Sasa walimu wakaamua watoto wa kidato cha nne hawatakwenda kucheza disko. Mimi niko kidato cha sita, sasa tulipanga kwenda disko Korogwe Girls. Wakaamua (walimu) kidato cha nne hawatakwenda Korogwe Girls, badala yake waletewe taarabu.

Sikukubaliana, nikaandika makala inahoji uamuzi huo. Title yake naikumbuka hadi leo, inasema; “taarab for who’s benefit?” - taarabu kwa faida ya nani?

Halafu tukafanya mpango (wanafunzi) ikabandikwa kwenye mbao za matangazo shuleni, sikuandika jina langu halisi. Walimu wakauliza, wakapeleleza nani anaweza kuandika vitu kama hivi?....wakanikamata.

Nikatuhumiwa kuleta uchochezi, nikasimamishwa shule, baadaye walinirudisha. Lakini kwa ujumla miaka ya sekondari ilikuwa mizuri, hapakuwa na njaa kama wakati huu.

Raia Mwema: Baada ya kuhitimu kidato cha sita, nini kilichofuatia?

Lissu: Nikaenda JKT Mbeya, kwanza nilipelekwa Mafinga, lakini sikukaa tukapelekwa Mbeya operesheni yangu inaitwa; Operesheni ya Programu ya Chama, mwaka 1989.

Raia Mwema: Unakumbuka nini kuhusu enzi za JKT?

Lissu: Ninachokumbuka mjadala wa vyama vingi ulikuwa umeiva na CCM hawataki vyama vingi. Ilikuwa mwaka 1989/1990, kwa Katiba ya CCM wakati huo, kulikuwa kuna mkoa unaitwa Mkoa wa Majeshi, ulikuwa mkoa sawa na mingine katika chama.

Kwa hiyo, wakatuma wajumbe wao wa Mkoa wa Majeshi kutembelea kambi zote za jeshi na JKT Tanzania nzima, kueleza msimamo wa CCM.

Waliokuja Itende JKT kwetu nawakumbuka ni Omari Mahita wakati huo ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, Kanali Andrew Shija na mtu mwingine simkumbuki.

Nawakumbuka Kanali Shija na Omari Mahita kwa sababu walijenga hoja kwamba haya mageuzi (vyama vingi) hayatuhusu kwa hiyo tusishabikie yasiyotuhusu; eti yanayowahusu Wazungu, Ulaya Mashariki na kwingine.

Nakumbuka nilipambana vibaya sana na Omari Mahita kwenye huo mkutano. Nilisimama kuuliza maswali nikitambua kuwa kabla hawajaja, Mwalimu Nyerere alihutubia mkutano wa Baraza Kuu la Vijana wa CCM, Mwanza na akasema wanaodhani mageuzi ya Ulaya Mashariki hayatuhusu, ni wajinga.

Kwa hiyo, nikamuuliza RPC Omari Mahita nikamwambia kwamba Mwalimu Nyerere alisema wanaofikiri mageuzi ya Ulaya Mashariki hayatuhusu ni wajinga, na wewe umekuja na timu yako unatuambia haya mambo ni ya Wazungu hayatuhusu.

Sasa mjinga ni Mwalimu Nyerere aliyesema yanatuhusu au nyie ambao mnatuambia kwamba hayatuhusu?

Raia Mwema: Bila shaka ulitumbukia katika uhasama wa ghafla na meza kuu. Hali ilikuwaje?

Lissu: Omari Mahita ni mweupe sana, basi, ghafla akabadilika rangi akawa mwekundu. Ikawa makamanda kadhaa wakasimama tayari kumshughulikia huyu serviceman...maana nilishapita ukuruta. Wakasimama kutaka kumshughulikia anayetukana maofisa wa jeshi.

Lakini kanali Shija (marehemu sasa) akasimama akanitetea. Akasema; hoja ya serviceman ni sahihi kabisa, Mwalimu ndivyo alivyosema. Kwa hiyo, hatuwezi....kusema hayatuhusu. Maana yake tayari nilianza kusakamwa pale... akasema ni kweli hatuwezi kukwepa haya mawimbi na upepo. Shija akapiga siasa, na hatimaye akaniepushia kibano.

Raia Mwema: Kwa hiyo makamanda wenyewe kwa wenyewe walitofautiana mbele yenu?

Lissu: Walitofautiana na baada ya hapo, hakuna ofisa wa JKT aliyenigusa tena. Wengi baada ya hapo wakaamini mimi ni usalama wa taifa.

Maisha yakawa mazuri. Hakuna aliyenigusa kwa sababu kama nimezungumza vile na kanali wa jeshi, kwa sababu mkuu wa kambi mwenyewe hakuwa kanali, alikuwa luteni kanali, sasa mimi nimetetewa na Kanali Shija. Kwa hiyo nilikuwa nakula shushi (mambo mteremko).

Baada ya hapo nikaenda Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Miaka ile ulikuwa huendi chuo kikuu kama si mwanachama wa CCM na sehemu ya mafunzo unayopata JKT ni pamoja na itikadi ya CCM na mnapomaliza mafunzo mnakabidhiwa pia kadi za chama. Kwa hiyo, nilikuwa mwanachama wa CCM na hiyo ni muhimu watu wakafahamu.

Lakini nilikuwa mwanachama kwa sababu tu nilitaka kusoma. Ndivyo maisha yalivyokuwa na baada ya hapo. Nilipoingia chuoni kadi haikuwa na kazi sana kwangu. Siku ya kwanza chuo kikuu hadi naondoka, mijadala yote nilikuwa mstari wa mbele kabisa pamoja na kwamba sikuwahi kuwa kiongozi.

Raia Mwema: Katika mijadala yenu chuoni hasa ile mikubwa, hoja gani unakumbuka zilitikisa uongozi au hata nchi?

Lissu: Wakati huo, dunia na nchi ilikuwa ikibadilika, hatukuwa tayari tena kutawaliwa na mfumo wa chama kimoja, eti usipokuwa na kadi ya chama huendi chuo. Nikiwa mwanafunzi, uchangiaji wa gharama za shule ulianza wakati huo.

Nilikaa mwaka mzima nyumbani kabla ya kuingia chuo kikuu kwa sababu mwaka 1989 wanafunzi wa UDSM waligoma, chuo kikafungwa.

Pamoja na kwamba sikuwa sehemu ya huo mgomo wakati huo nilikuwa JKT, lakini madhara ya mgomo yalinigusa kwa kukaa nyumbani mwaka mzima. Nilipojiunga chuo mwaka 1991, tayari vuguvugu lilikuwa kubwa sana. Na upinzani dhidi ya uchangiaji gharama za elimu ulikuwa mkubwa sana.

Raia Mwema: Mliguswa vipi na tukio la kumdhalilisha Rais Mwinyi wakati ule chuoni UDSM?

Lissu: Chuo kilifungwa kutokana na tatizo hilo mwaka 1989. Ni tukio lililotugharimu ambao ndiyo tulitaraji kwenda kuanza masomo. Tulikaa nyumbani mwaka mzima.

Raia Mwema: Katika changamoto za mageuzi chuoni, baadaye ulijiunga na chama gani baada ya mfumo wa vyama vingi kuruhusiwa?Kwa hiasni ya http://www.raiamwema.co.tz/

PONGEZI SPIKA WA BUNGE MHESHIMIWA ANNA MAKINDA KWA KULISIMAMIA BUNGE KWA KANUNI ZAKE VIZURI.

Jana nilishuhudia mjadala wa bajeti ya Ofisi ya Rais Utumishi na idara zake ambapo shilingi zaidi ya mbili zilitolewa, pongezi kwa spika kwa kusimamia vizuri na kwa busara mjadala ule maana kazi ilikuwa nzito hasa pale Mnyika na kaka yake Tundu Lissu walipotoa shilingi zao. Pia pongezi ziende kwa waheshimiwa mawaziri Hawa Ghasia, Stephen Wasira na Chikawe kwa kujibu hoja kwa ueledi mkubwa. MUNGU IBARIKI TANZANIA.