Jumapili, 6 Septemba 2015

CCM NA UKAWA WACHUANA KATIKA KUJAZA WASIKILIZA SERA VIWANJANI, KATI YA MAGUFULI AU LOWASSA KUCHUKUA DOLA 2015....

KAMPENI za uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu, sasa umepamba moto na kuonyesha upinzani mkali wa jino kwa jino baina ya wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wale wanaoungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Risasi Jumamosi linathibitisha.Habari zilizopatikana kutoka mikoani ambako kampeni zinaendelea, zinasema watu wamekuwa wakijitokeza kwa wingi katika mikutano ya wagombea wa vyama vyote, ili kusikiliza sera zinazotolewa, kitu kinachoonyesha kuwa kutakuwa na upinzani mkali kwani wingi wa watu hautoi picha ya mshindi.
“Ni ngumu kubashiri, ukienda kwenye mkutano wa CCM unaweza kudhani huyu ndiye mshindi, lakini kesho unapoenda kwenye mkutano wa Ukawa, hali ni kama kule tu, Magufuli (John-CCM) anajaza watu, Lowassa (Edward, Ukawa) anajaza nyomi, watu hawatabiri,” alisema Tiom Khane, aliyejitambulisha kuwa anatoka taasisi isiyo ya kiserikali inayozunguka kufuatilia mwenendo wa kampeni.
Alisema hadi sasa wamehudhuria mikutano ya kampeni ya wagombea wa Ukawa na CCM katika mikoa ya Mwanza, Mbeya, Rukwa na Mtwara na kugundua kuwa uchaguzi wa mwaka huu utakuwa na matokeo ya kushangaza, kwani hakuna dalili za ushindi wa kishindo kama ilivyopata kutokea miaka ya nyuma.
Katika nafasi ya urais, CCM inajivunia Dk. John Pombe Magufuli wakati Ukawa wanaye Edward Lowassa, watu wawili wanaosadikika kuwa mmoja wao ndiye atarithi mikoba ya Jakaya Kikwete baada ya kumalizika kwa uchaguzi huo unaosubiriwa kwa hamu nchini.
credits; masama blog

Maoni 1 :