Jumanne, 14 Julai 2015

PASTOR KALU ATANGAZA NIA MBIO ZA UBUNGE MBEYA VIJIJINI KUPITIA CCM...


MWANDISHI WA HABARI KALULUNGA AJITOSA MBIO ZA UBUNGE MBEYA VIJIJINI‏

Mwandishi wa Habari, Gordon Kalulunga akizungumza katika viwanja vya mahubiri alipokuwa akitangaza nia ya kugombea Ubunge jimbo la Mbeya vijijini.

Kalulunga akitaja vipaumbele vyake

Katibu wa Umoja wa Vijana Wilaya ya  Mbeya vijijini, Siulanga  akiwaasa Vijana kumuunga mkono kijana mwenzao.

Kalulunga akisalimiana na mmoja wa wazee waliojitokeza kumsikiliza alipokua akitangaza nia

Baadhi ya wanachama wapya wakikabidhiwa Kadi

Vijana wakiserebuka

Burudani zikiendelea
Wananchi wakimsikiliza Kalulunga

MWANDISHI wa habari wa gazeti la Mtanzania kutoka Mbeya, Gordon Kalulunga amejitosa kuingia kwenye kinyang’anyiro cha Ubunge katika Jimbo la Mbeya vijijini kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi(CCM).

Kalulunga alitangaza kuingia kwenye mchakato wa kugombea kuteuliwa na Chama ili aweze kupeperusha bendara katika uchaguzi mkuu ujao katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika jana kwenye viwanja vya mahubiri Mbalizi mkoani Mbeya.

Mtia nia huyo alisema endapo Chama chake kitampitisha na hatimaye kushinda Ubunge katika Jimbo hilo atahakikisha wananchi wote wanajiunga na mfuko wa bima ya afya kwa ajili ya matibabu kwa kila kaya kuchangia ili kupunguza adha na gharama kubwa za matibabu.

Aliongeza kuwa akifaniiwa kuukwaa Ubunge pia atasimamia kuhakikisha Jimbo hilo linapata Chuo cha aina yoyote kikiwemo Chuo cha ufundi kwa ajili ya vijana kupata elimu jambo lilatalopunguza wimbi la ukosefu wa ajira kwa vijana.

Kalulunga alisema kipaumbele kingine atakachoshughulikia ni pamoja na kupigania ujenzi wa ofisi za makao makuu ya Wilaya hiyo katika eneo husika ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi tofauti na ilivyosasa ambapo Ofisi za Wilaya ya Mbeya zipo katikati ya Jiji la Mbeya.

Awali Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Wilaya ya Mbeya vijijini, Japheti Siulanga aliwataka vijana wote kuungana ili kumuunga mkono kijana mwenzao aliyejitokeza na kuonesha nia ya kutaka kuongoza akiwa Mbunge wa jimbo hilo.

Aidha katika mkutano huo vijana zaidi ya 26 walijiunga na Chama cha mapinduzi na kukabidhiwa kadi za umoja wa Vijana.
CREDITS;MBEYA YETU BLOG

DR MAGUFULI- FAHAMU WASIFU WAKE HAPA


Mh. John Pombe Magufuli akiwa na mkewe Janeth ambaye ni Mwalimu wa Shule ya Msingi Mbuyuni Daresalaam. Ikumbukwe kuwa shule hii ya Mbuyuni ndiyo aliyokuwa akifundisha Mama Salma Kikwete mke wa Rais wa sasa Mh. Jakaya Mrisho Kikwete.


Dk. John Pombe Joseph Magufuli, alizaliwa Oktoba 29, 1959 wilayani Chato – wakati huo ikiwa Mkoa wa Kagera (sasa Mkoa wa Geita).
Ana Shahada ya Uzamivu ya Kemia (2006 – 2009) kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Mwaka 1991 – 1994, alisoma Shahada ya Uzamili (Kemia) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na baadaye Chuo Kikuu cha Salfordnchini Uingereza.
Mwaka 1985 – 1988, alisoma Shahada ya Kwanzaya Elimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akichukua masomo ya Kemia na Hisabati.
Mwaka 1981 – 1982, alisoma diploma katika Chuo cha Mkwawa akichukua masomo ya Kemia na Hisabati.
Mwaka 1979 – 1981, alipata elimu ya juu ya sekondari katika Shule ya Sekondari Mkwawa, Iringa.
Mwaka 1977 – 1978, alisoma elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari Lake, Mwanza.
Mwaka 1975 – 1977, alisoma Shule ya Msingi Katoke, Biharamulo mkoani Kagera.
Mwaka 1967 – 1974, alisoma Shule ya Msingi, Chato.
Mafunzo
Machi 1984 – Juni 1984 alihudhuria mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Mpwapwa mkoani Dodoma.
Januari 1984 – Machi 1984 alikuwa JKT Makuyuni, Arusha.
Julai 1983 – Desemba 1983 alikuwa JKT Makutupora, Dodoma.
Uzoefu wa kazi
Mwaka 2010 – hadi sasa: Waziri wa Ujenzi na Mbunge wa Chato.
Mwaka 2008 – 2010: Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Samaki; Mbunge wa Biharamulo Mashariki (Chato).
Mwaka 2005 – 2008: Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; na Mbunge wa Biharamulo Mashariki (Chato)
Mwaka 2000 – 2005: Waziri wa Ujenzi, na Mbunge wa Biharamulo Mashariki.
Mwaka 1995 – 2000: Naibu Waziri wa Ujenzi; na Mbunge wa Biharamulo Mashariki.
Mwaka 1989 – 1995: Mkemia Chama cha Ushirika cha Nyanza Cooperative Union (Ltd.), Mwanza.
Mwaka 1982 – 1983: Mwalimu Shule ya Sekondari Sengerema (akifundisha masomo ya Kemia na Hisabati).
Dk. Magufuli amepata tuzo mbalimbali za ndani na nje ya nchi.
Ameshiriki na kuongoza mikutano mingi ya kitaifa na kimataifa.
Ameandika vitabu na majarida mbalimbali. Ameoa na ana watoto kadhaa.

Alhamisi, 9 Julai 2015

KUTOKA GAZETI LA MWANANCHI; KISU KIKALI CHA KAMATI KUU YA CCM (CC) LEO KITAONDOKA NA VICHWA 33 KATI YA 38 VYA WATIA NIA UGOMBEA URAIS..


Dodoma. Kisu kikali cha Kamati Kuu ya CCM (CC) leo kitaondoka na vichwa 33 kati ya 38 vya walioomba kuteuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho kumrithi Rais Jakaya Kikwete anayemaliza ngwe yake.

Kikao hicho ni hatua ya pili baada ya kukamilika kwa kikao cha Kamati ya Maadili kilichokutana jana usiku chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete huku kikitawaliwa na usiri mkubwa, kuhama ukumbi na kila dalili za kubadili ratiba iliyopangwa awali ili kuvuruga mipango ya kambi za wagombea.

Habari zilizolifikia gazeti hili zilisema kulikuwa na uwezekano wa kubadili ratiba ili vikao vya Kamati ya Maadili na CC ama vifuatane au vifanyike usiku ili kuyanyima makundi nafasi ya kujipanga.

Alipoulizwa jana kuhusu vikao hivyo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alidai kuwa hata yeye hakuwa na uhakika wa lini na muda gani hasa kikao cha Kamati ya Maadili kingefanyika.

Awali, vifaa vya ukaguzi wa wajumbe vilikuwa vimewekwa katika Makao Makuu ya CCM, White House lakini baadaye jioni viliondolewa na hapakuwa na taarifa zozote zilizotolewa.

Habari zilizopatikana baadaye zilidai kuwa kikao hicho cha Maadili kilitarajiwa kufanyika Ikulu ya Dodoma kuanzia saa nne usiku wa jana.

Haya yanajitokeza wakati macho na masikio ya Watanzania yakiwa hapa Dodoma kusikiliza namna kazi ya kuchuja wagombea itakavyofanyika na kujua ni watu gani 33 watakaoanza kulambwa na kisu cha CC, hasa kwa majina makubwa yanayotazamwa na wengi, mara tu baada ya kujadiliwa na Kamati ya Maadili.

Kazi za Kamati Kuu leo

Kikao cha CC kina majukumu matatu leo ambayo ni kufikiria na kutoa mapendekezo kwa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), majina yasiyozidi matatu ya walioona kuwania urais wa Zanzibar ambayo imeombwa na Rais wa sasa, Dk Ali Mohamed Shein pekee, kufikiria na kutoa mapendekezo kwa NEC majina yasiyozidi matano ya walioomba kuwania urais wa Muungano na kuandaa mkutano wa NEC.

Vigezo vya maadili

Kulingana na kanuni za Uongozi na Maadili, toleo la 2012 kifungu cha 4(ii), kuhusu taratibu za kuomba uongozi, wanachama wanaogombea uongozi ambao uteuzi wao hufanywa na vikao vya kitaifa, watachunguzwa kwanza uadilifu wao na chombo cha maadili cha CCM kwa ushirikiano na vyanzo vingine.

Kanuni hizo zinasema mwanachama wa CCM anapoomba uongozi katika ngazi yoyote, itikadi na mwenendo wake vitachunguzwa kwanza na Kamati ya Usalama na Maadili inayohusika, ndipo maombi hayo yaliyoambatanishwa na mapendekezo ya kamati hiyo yatakapofikishwa mbele ya kikao chenye madaraka ya kutoa uamuzi.
Ikiwa mwanachama hakupendekezwa kwa sababu ya kukiuka Katiba ya CCM, Kanuni za CCM na sheria ya nchi, hatakuwa na haki ya kukata rufaa kwa mtu yeyote au kikao chochote. Lakini ikiwa mwanachama atakataliwa kugombea kwa sababu ya madhambi yake katika chama, basi ni wajibu wa Kamati ya Usalama na Maadili kumjulisha makosa yaliyomnyima haki ya kugombea, naye anaweza kukata rufaa kwa mujibu wa haki zake kikatiba.

Mtu yeyote anayetuhumiwa mbele ya Kamati ya Usalama na Maadili ya ngazi yoyote, kwa kosa lolote linalohusiana na maadili au nidhamu ya chama atasomewa na kutakiwa kuzijibu tuhuma hizo mbele ya wajumbe wa kamati hiyo ama kwa kauli yake mwenyewe au kwa maandishi, lakini hataambiwa nani aliyezileta tuhuma hizo, isipokuwa kama imekwishajulikana mapema kutokana na mijadala ya vikao, vyombo vya sheria au vyombo vya habari.

Kanuni ya maadili inaendelea kusema kuwa uchambuzi wa tuhuma hizo utafanywa kwa kutumia njia mbalimbali pamoja na mashahidi watakaopatikana.

Uchunguzi utakapokamilika na endapo itadhihirika kwamba tuhuma zina uzito, mtuhumiwa ataitwa mbele ya kikao cha Kamati ya Usalama na Maadili ya ngazi inayohusika, kama ni lazima, ili apate kuhojiwa ana kwa ana.

Pia, kanuni inasema Kamati ya Usalama na Maadili ya ngazi inayohusika itatoa mapendekezo yake kuhusu suala hilo kwenye kikao cha uamuzi kinachohusika. Mtuhumiwa atapewa nakala ya uamuzi kwa maandishi.

Wagombea wanne kukosa CC

Katika kikao cha CC kinachofanyika leo, wajumbe wanne ambao ni miongoni mwa majina 38 yatakayojadiliwa katika mchujo huo watalazimika kukaa kando ili kukwepa mgongano wa masilahi.

Wajumbe hao ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa Sheria na Katiba, Dk Asha-Rose Migiro, Makamu wa Rais, Dk Mohamed Ghalib Bilal na Waziri wa Kilimo na Chakula, Stephen Wasira.

Kwa mujibu wa Kanuni za Uteuzi wa Wagombea wa CCM katika Vyombo vya Dola, Toleo la Pili – Februari, 2005, ukurasa wa 25, kifungu cha 21 (3); wajumbe wa vikao vya uchujaji na uteuzi wa wagombea kwa ngazi inayohusika hawaruhusiwi kuendelea na kazi ya uchujaji na uteuzi iwapo wao ni wagombea katika ngazi hiyo.

Kanuni hiyo pia imetoa miiko ya shughuli za uchujaji na uteuzi wa wagombea na wajumbe wote wanatakiwa na kanuni kuzingatia maadili na nidhamu ya chama katika kusimamia na kutekeleza shughuli za uteuzi.

Kanuni hizo zinasema ni mwiko kwa kiongozi yeyote kwa maneno au vitendo kumpendelea au kumsaidia kupata kura nyingi mwombaji mmoja dhidi ya mwingine, kutumia au kuhusisha ukabila, dini, rushwa, rangi, hila na eneo analoishi au anakotoka katika shughuli yoyote ya uchaguzi.

Pia, ni mwiko kwa kiongozi yeyote au mwombaji yeyote wa nafasi ya uongozi au mwanachama yeyote aliyekabidhiwa dhamana ya usimamizi au uangalizi au uratibu wa kura za maoni, uchujaji na uteuzi, kufanya vitendo vya ukiukwaji wa kanuni.
Kuhusu misaada, kifungu cha tano (a) kinasema ni marufuku kwa mgombea yeyote mtarajiwa au wakala wake, kufanya vitendo vyovyote vinavyoonekana dhahiri kuwa ni sehemu ya kampeni za kuwania nafasi anayoitafuta kabla ya muda rasmi wa uongozi unaohusika haujamalizika.

Kanuni imetoa adhabu kwa watakaovunja miiko hiyo na kwa kiongozi atakayethibitika kuivunja atavuliwa uongozi na kwa mwanachama anayeomba kugombea nafasi yoyote atakayethibitika kuivunja hiyo hatateuliwa kugombea nafasi anayowania.
CHANZO: MWANANCHI

Jumatatu, 6 Julai 2015

WALUGULU WAPATA CHIFU MPYA, NI KUNGALU WA 15. NI BAADA YA KINGALU WA 14 KUFARIKI DUNIA TAREHE 1/7/2015 NA KUZIKWA TAREHE 2/7/2015 KIJIJINI KINOLE MOROGORO.


 Rais Jakaya Mrisho Kikwete akishuhudia kusimikwa kwa Kiongozi mpya wa kabila la Waluguru Chifu Kingalu wa 15 katika kijijini Kinole mkoani Morogoro Alhamisi Julai 3, 2015 kufuatia kifo cha Chifu Kingalu wa 14 aliyefariki Jumatano jijini Dar es salaam na kuzikwa siku ya pili kijijini hapo.
Kiongozi mpya wa kabila la Waluguru Chifu Kingalu wa 15 akitolewa nje baada ya kusimikwa rasmi kuwa kiongozi wa kabla hilo kijijini Kinole mkoani Morogoro Alhamisi Julai 3, 2015 kufuatia kifo cha Chifu Kingalu wa 14 aliyefariki  Jumatano jijini Dar es salaam na kuzikwa kijijini hapo.

Kiongozi mpya wa kabila la Waluguru Chifu Kingalu wa 15 akichomeka fimbo yake ya Uchifu kabla ya kuketi  meza Kuu na Rais Jakaya Mrisho Kikwete baada ya kusimikwa rasmi kuwa kiongozi wa kabila hilo kijijini Kinole mkoani Morogoro Alhamisi Julai 2, 2015 kufuatia kifo cha Chifu Kingalu wa 14 aliyefariki jana Jumatano jijini Dar es salaam na kuzikwa  kijijini hapo.Picha na IKULU

Alhamisi, 2 Julai 2015

TAMISEMI YATANGAZA MAJINA YA WANAFUNZI WALIOCHAGULIWA KUJIUNGA NA KIDATO CHA TANO 2015/2016.



OWM-TAMISEMI inawatangazia majina ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano na Vyuo vya Ufundi kwa mwaka 2015.Wanafunzi waliochaguliwa ni kutoka shule za Serikali na zisizo za Serikali.

Jumla ya wanafunzi 55,003 wakiwemo wasichana 23,303 na wavulana31,700 wamechaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano na Vyuo vya Ufundi.

  
Kati ya wanafunzi waliochaguliwa 29,744 wakiwemo wasichana 11,450 nawavulana 18,294 sawa na asilimia 54.08 watajiunga na masomo ya Sayansina Hisabati; na wanafunzi 25,259 wakiwemo wasichana 11,853 nawavulana 13,406 sawa na asilimia 45.92 wamechaguliwa kusoma masomoya Sanaa na Biashara.

Wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano mwaka 2015 wataanza muhula wa kwanza tarehe 18 Julai, 2015 na hakutakuwa nafursa ya mabadiliko yoyote ya shule. 

  
Wanafunzi wote wanatakiwa kuripoti katika shule walizopangwa kwa wakati. Endapo mwanafunzi atachelewa kuripoti kwa zaidi ya siku 14 kuanzia tarehe ya mwisho yakuripoti, nafasi yake itachukuliwa na mwanafunzi mwingine aliyekosa nafasi.

Orodha ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano naVyuo vya Ufundi mwaka 2015 inapatikana kwenye tovuti ya OWMTAMISEMI
ya www.pmoralg.go.tz BONYEZA HAPA