Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo AJALI. Onyesha machapisho yote
Inaonyesha machapisho yaliyo na lebo AJALI. Onyesha machapisho yote

Jumamosi, 9 Novemba 2013

JAMANI TUNAKWISHA, AJALI ZA PIKIPIKI ZIMERIPOTIWA SANA JUMA HILI, TUELIMISHANE NA KUKUMBUSHANA KUCHUKUA TAHADHARI.

 
Toyota Land Cruiser linalodaiwa kumgonga muendesha pikipiki aliyetambulika kwa jina moja la Huweso.
 

...Askari wa usalama wa barabarani akichukua maelezo katika eneo la tukio, alielala chini ni Huweso baada ya kupata ajali.

Picha mbili za juu zinaonesha ajali iliyotokea juzi Ihumwa Dodoma ikisababisha vifo vya vijana wawili Ramadhan Lesso na George Lwandala ambao walikuwa wanafunzi wa CBE Dodoma, chanzo cha ajali ni mwendokasi na lori kupaki bila alama zozote kando ya barabara kuu ya Morogoro-Dodoma. Wanafunzi hao waliligonga lori kwa nyuma na kufariki papo hapo.


Ajali nyingine ya pikipiki imetokea juzi huko Geita ikihusisha mwendesha bodaboda na abiria wake wa kike ambao hawakufahamika majina yao kuanguka katikati ya barabara na baadae kukanyagwa na gari aina ya Noah waliyokuwa wanapishana nayo.
RAI
Kila mtu kwa nafasi yake ajaribu kufanya wajibu wake ikiwa ni kuelimisha waendesha bodaboda kwenda kwa mwendo wa tahadhari na wastani ili ikitokea tatizo la ghafla waweze kudhibiti, wenye magari waheshimu wenye vyombo vidogo barabarani kama bajaj na pikipiki pia abiria wajaribu kuwadhibiti madreva wao wanapoona wanaenda kwa kasi sana.

Jumatano, 10 Oktoba 2012

AJALI ZINATUMALIZA, MWENDESHA BODABODA NA ABIRIA WAKE WAFA KWA AJALI MAENEO YA MAKONGO.


Jamaa akijaribu kutambua mwili wa marehemu juzi asubuhi waliofariki baada ya pikipiki yao kugongwa juzi asubuhi maeneo ya Makongo shuleni, Dar es salaam. Eneo hili limekuwa zikitokea ajali za mara kwa mara hasa pikipiki, tuchukue tahadhari.(Picha na Sufiani Mafoto)

Jumatano, 18 Julai 2012

AJALI NYINGINE YA MELI KUZAMA IMETOKEA ZANZIBAR LEO MCHANA. NI MV SKAGIT SEAGUL, SMZ IMETANGAZA SIKU TATU ZA MAOMBOLEZO.

 

Wakazi wa Zanzibar wakiwa wamekusanyika katika Bandari ya Malindi mjini Unguja Zanzibar jioni ya leo wakati miili ya baadhi ya abiria wa Boti ya Kampuni ya Seagull "MV Skagit" wakitolewa baada ya boti hiyo kuzama na kupoteza maisha ya watu zaidi ya 200 hii leo ikitokea jijini Dar es Salaam.
Askari wa JWTZ wakiwa wamejipanga wakati wa zoezi la kupokea maiti.
Moja ya maiti ikiwa imebebwa na askari

Maiti ingine ikiwa imebebwa...
Ni hali ya huzuni Visiwani humo na jijini Dar es Salaam na Tanzania kwa ujumla. Ajali hii imetokea ikiwa imepita miezi kadhaa baada ya meli nyingine ya Abiria kupoteza uhai wa watu visiwani humo.
Meli ya Mv Skagit iliyokuwa safarini kutoka Dar kuelekea Zanzibar imezama majira ya saa nane mchana hii leo katika maeneo Pungume na Chumbe baada ya kukumbwa na upepo mkali.

Meli hiyo inayosadikiwa kuwa na abiria 250 inasemekana imepindukia upande mmoja na huku abiria wengi wakiweza kuokolewa kutokana na jitihada mbali mbali kupitia vile vile msaada wa boti za Mv Kilimanjaro, Tug ya Bandari na vyombo vyengine.

Mpaka tunaandika taarifa hizi ni maiti tatu zilikwishapatikana na kiasi cha abiria 150 wameokolewa na waliojeruhiwa wanatibiwa katika Hospitali ya Mnazimmoja.

Taarifa zinaeleza kwamba kulikuwa na watoto takriban 30 na Watalii kutoka nchi mbali mbali wafikao kumi.

Wazamiaji kutoka Kikosi cha KMKM pamoja na Jeshi tayari wapo eneo la ajali kusaidia kuokoa maisha ya wananchi waliokumbwa na maafa haya

Alhamisi, 24 Novemba 2011

AJALI MBAYA YA GARI YATOKEA ENEO LA RIVERSIDE JANA MCHANA.

Lori la mafuta likiwa limepanda juu ya magari mengine madogo.

Gari dogo jekundu likiondolewa eneo la tukio.

Shughuli za uokoaji zikiendelea.


SIMANZI na majonzi jana vilitawala eneo la River Side, Dar es Salaam baada ya ajali mbaya iliyohusisha lori la mafuta na magari mengine madogo saba kusababisha vifo vya wawili papo hapo na wengine wanne kujeruhiwa vibaya.  Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela alisema ajali hiyo ilitokea majira ya saa saba mchana na kwamba maiti na majeruhi wote walipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Ilala, Amana.


Lori la mafuta aina ya Marcedes Benz la Kampuni ya Dalbit lililokuwa likielekea Buguruni liliacha njia na kuyagonga magari saba yaliyokuwa kwenye foleni ya kuelekea Ubungo. Magari mengine yaliyohusika katika ajali hiyo ni Toyota Noah, BMW, Toyota Canter na Toyota Corolla nne.  Mmoja wa waliofariki dunia ni mama mmoja ambaye mwili wake ulitenganishwa kabisa na kichwa baada ya gari alilokuwemo kukandamizwa na lori hilo.


Habari kutoka eneo la tukio, zilieleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni lori hilo kuacha njia, baada ya dereva wake kutaka kumkwepa mtembea kwa miguu ambaye alielezwa kuwa ni mama mjamzito. Watu hao wawili waliofariki dunia walikuwa kwenye magari tofauti.


Hata hivyo, habari nyingine zinadai kwamba miongoni mwa waliofariki katika ajali hiyo ni mchuuzi kanda za video ambaye alikuwa akitembeza biashara yake katika eneo hilo.  Baadhi ya majeruhi walisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa lori hilo la mafuta baada ya dereva wake kushindwa kulimudu alipojaribu kumkwepa mtembea kwa miguu aliyekuwa anavuka barabara.


“Nilikuwa naelekea Ubungo nikiwa katika foleni, mara nikaona lori la mafuta likiwa linahama njia na kuja upande wetu. Baadaye kidogo, sikuelewa tena kilichokuwa kimetokea,” alisema Yahaya Makame.


Makame ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema licha ya kutokea kwa ajali hiyo mbaya, hakukuwa na msaada wowote wa haraka zaidi wa wakazi wa eneo hilo na wapita njia waliojitokeza kushuhudia.  “Ajali imetokea saa 7:00 mchana, lakini, waokoaji wanafika saa 8:00.

Muda wote huo watu walikuwa bado wako ndani ya magari hayo wakiwa wameminywa na lori! Kuna usalama hapo kama siyo neema ya Mungu?”  Gari la polisi liliwasili eneo la ajali majira ya saa nane mchana kusaidia uokoaji

Jumapili, 9 Oktoba 2011

AJALI MBAYA YA BASI KUPINDUKA YATOKEA LEO MCHANA HUKO KILWA, NG'ITU EXPRESS YAPINDUKA NA KUACHA MAJERUHI KIBAO.

Wananchi na abiria waliokuwa wakisafiri na magari mengine njia ya kusini leo hii wakisaidia kuinua gari lililopinduka ili kuwatoa abiria watatu walionasa humo. Ajali ilitokea baada ya dereva wa basi hilo kujaribu kuyapita magari mengine bila mafanikio eneo la kati ya kijiji cha Sinza na Ngong'otela huko Kilwa.
Baada ya saa moja na nusu zoezi lilikamilika na kuwanasua abiria hao walionasa wakiwa katika majeraha mabaya baada ya kubanwa na viti vya basi hilo, majeruhi walikimbizwa katika hospitali ya Wilaya ya KINYONGA huko Kilwa.
Baadhi ya waokoaji wakijaribu kuangalia kama kuna mtu yoyote aliyebakia ndani ya basi hilo.
Manusura mmoja wa ajali hiyo aliyetambulika kwa jina la Mansour akitokea Dar es salaam kwenda Mtwara akifanya mawasiliano ya simu kuwajulisha ndugu zake kuwa kapata ajali, wengi wa abiria wa basi hilo walikuwa ni wanafunzi wa shule ya sekondari ya wasichana ya Mtwara(Mtwara Girls High School) ambao walikuwa wakielekea shuleni. Mkuu wa mkoa wa Lindi na Dar es salaam pia na Mkuu wa Wilaya ya Kilwa walikuwepo kusaidia uokoaji. Tunawaombea majeruhi wapone haraka.