Jumapili, 3 Novemba 2013

KESI YA BABU SEYA NA PAPII KOCHA YAFANYIWA MAREJEO MAHAKAMA YA RUFAA TANZANIA, VICHEKO AU VILIO TENA VINAKARIBIA. TUWAOMBEE MAMBO YAWE MAZURI.

Stori: Richard Bukos na Denis Mtima MWANAMUZIKI mkongwe wa muziki wa dansi, Nguza Viking maarufu kama Babu Seya na mwanaye Johnson Nguza ‘Papii Kocha’ pamoja na ndugu zao, Jumatano iliyopita walitoka kwa vicheko katika Mahakama ya Rufaa Tanzania baada ya kuridhishwa na utetezi uliotolewa na wakili wao, Mabere Marando, anayepinga hukumu ya kifungo cha maisha jela, waliyopewa wanamuziki hao.


Babu Seya na Papii Kocha wakiwa na furaha wakati wakitoka katika Mahakama ya Rufaa Tanzania.
Mbele ya majaji watatu wa Mahakama hiyo, Marando alikabiliana na timu ya mawakili watano waandamizi wa serikali ambao ni Jackson Brashi, Angaza Mwaipopo, Imaculate Banzi, Joseph Pande na Apimark Mabruk.


Babu Seya (wa pili kulia) na Papii Kocha (wa pili kushoto) wakiwa mahakamani kusikiliza rufaa yao.
Miongoni mwa hoja ambazo Marando alionekana kuwabana mawakili wa serikali ni jinsi Jamhuri ilivyowatia hatiani wateja wake kwa kutumia ushahidi uliotolewa na watoto katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu jijini Dar, akisema zipo taratibu za kuchukua katika ushahidi kwa mtoto ikiwemo kurekodiwa, jambo ambalo halikufanyika.


...Wakiwa na furaha wakati wakitoka katika mahakama baada ya kuridhishwa na utetezi uliotolewa na wakili wao, Mabere Marando.
Marando alizidi kuweka wazi kuwa katika ushahidi uliotolewa mahakamani hapo, ulionesha nyumba iliyodaiwa kufanyiwa uhalifu huo ilikuwa na mlango wa siri uliotumiwa na watoto hao kupenya hadi ndani pasipo kuonekana jambo ambalo baadaye lilidhihirika si kweli kwani nyumba hiyo haikuwa na mlango mwingine zaidi ya wa uani na barazani.


Wanahabari wakijaribu kupata matukio katika tukio hilo.
Hata hivyo, jopo la mawakili wa Jamhuri licha ya kukumbana na wakati mgumu kutoka kwa wakili Marando, liliendelea kusisitiza kuwa hukumu iliyotolewa dhidi ya washitakiwa hao ilikuwa sahihi.
Baada ya mawakili hao kusisitiza hivyo Marando alipewa nafasi nyingine ya kutoa utetezi wake, ambapo aliendelea kufafanua makosa mbalimbali yaliyofanyika kuwahukumu wateja wake kwa kutaja vifungu vya sheria ambavyo vilionekana kama kuwasafishia njia wateja wake hao hali iliyozua tabasamu na vicheko mahakamani hapo.


Watoto wawili wa Babu Seya, Nguza Mbangu (kulia) na Francis Nguza (kushoto) wakiwa na nyuso za furaha baada ya kuona kesi ya baba yao na ndugu yao inaelekea pazuri.
Baada ya kupitia marejeo ya kesi hiyo kwa pande hizo mbili, jopo la majaji akiwemo, Salum Masatti liliahirisha kesi hiyo na kusema litapanga siku ya hukumu huku wafungwa hao wakirejeshwa gerezani wakiwa na vicheko vya furaha huku ndugu na jamaa nao wakikumbatiana kwa shangwe.
Credits;globalpublishers.info

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni