Jumanne, 11 Novemba 2014

MBOWE AMCHANA SITTA MBELE YA WAPIGA KURA WAKE.

Mbowe ‘amwaga sumu’ nyumbani kwa Sitta

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akiwasili kwenye Uwanja wa Extended mjini Urambo, Tabora alikohutubia mkutano wa hadhara juzi. Na Mpigapicha Maalum
Urambo. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amefanya mkutano mkubwa Urambo Mashariki na kumshutumu Mbunge wa jimbo hilo, Samuel Sitta kwa kuchakachua maoni ya wananchi katika mchakato wa Katiba Mpya.
Katika mkutano huo ulifanyika katika Uwanja wa Extended mjini hapa takriban mita 100 kutoka nyumbani kwa Sitta aliyeongoza Bunge la Katiba, Mbowe alisema historia ya nchi hii itamhukumu mbunge huyo kwa maovu hayo.
Alisema kutokana na uovu huo wa Sitta ambaye amekuwa akiisifia Katiba Inayopendekezwa kuwa itakuwa nzuri Afrika Mashariki na Kati, vyama vya upinzani vitaendelea kuidai katiba ya wananchi hata kwa miaka 100 ijayo.
Aprili mwaka huu, wabunge wa vyama vya upinzani chini ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), walisusia Bunge la Katiba mjini Dodoma wakilalamikia kuvunjwa kwa kanuni na kutofuatwa kwa mapendekezo ya wananchi yaliyotolewa katika Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.
Akihutubia mamia ya wafuasi wa chama hicho kwenye Operesheni Delete CCM, Mbowe ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa Ukawa, alisema ana uhakika Sitta ataipata hukumu hiyo ya historia kwa kile alichosema kudhulumu haki ya Watanzania milioni 45.
Mbowe anayetumia chopa katika ziara hiyo, alifika katika uwanja huo saa 11.45 na kuhutubia kwa dakika 30.
“Mzee Sitta najua upo nyumbani hapo na unanisikia, kama hunisikii basi mke wako Mama Margreth Sitta atakuwa ananisikia, lakini kama naye hayupo basi kutakuwa na wahudumu watanisikia na watakuja kukueleza,” alisema huku akiwaonyesha wafuasi wa chama hicho nyumba ya Sitta iliyopo jirani na uwanja huo.
Alisema Sitta alipuuza maoni ya wananchi waliyotoa katika mchakato wa Katiba Mpya na ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba badala yake akaweka maoni ya chama chake cha CCM.
“Tunasema kwamba historia ya nchi hii itamhukumu kwa maovu aliyoyafanya kukataa maoni ya wananchi na kuweka maoni ya chama chake,” alisema.
Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Hai, alisema baada ya maoni ya wananchi kuchakachuliwa... “Sasa tutaidai Katiba Mpya hata kwa miaka 100 ijayo.”
Alisema wabunge wa vyama vya upinzani walimwamini Sitta kwa kumpigia debe na baadaye walimpa kura  iliyomfanya awe Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba kutokana na rekodi yake alipokuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Tulifanya hivyo kwa kumwamini kutokana na rekodi zake akiwa spika, tunajuta kumchagua hatukufahamu kwamba atatusaliti na kudhulumu haki za Watanzania,” alisema Mbowe.

Alhamisi, 6 Novemba 2014

WATALII WALALAMIKIA RUSHWA KATIKA VIZUIZI VYA BARABARANI HUKO ZANZIBAR.



KAMA vituo 66 vya treni havitoshi katika safari nzima ya utalii, Teresa Williamson wa  Australia na Annemarie Schuller wa Uholanzi wamesema Watanzania wanaishi katika mazingira magumu na wanastahili kubadilika.
 Kauli hiyo wameitoa wakati wakizungumza na Mwandishi wa makala haya muda mfupi kabla ya kuondoka kurejea makwao baada ya ziara ya wiki mbili katika maeneo mbalimbali nchini.
Katika ziara yao ya kitalii walitumia treni, barabara na maji tena kwa kutumia jahazi wakitokea Pangani Tanga hadi Zanzibar.
Nilitaka kujua baada ya utalii wao wameona nini nchini Tanzania walisema pamoja na kufanikiwa kuwaona wanyama wakubwa watano kama walivyofikiria wakati wakiwa makwao wameshuhudia maisha masikini zaidi kuliko matarajio.
“Sijui inatokeaje watu wengi wana simu za mkono lakini ukiangalia maisha yao unayaona kuwa magumu sana,” alisema Teresa ambaye alifafanua kwamba ugumu wa maisha unaonekana katika miundombinu na usafirishaji, ulaji na utunzaji wa mazingira.
Wakiwa wamezaliwa mjini hawakuwa wanajua vijijini kukoje mpaka walipofika nchini Tanzania na kukumbana na hali ambayo hawakuitarajia  hata kidogo.
Pamoja na kushuhudia matukio yasiyokuwa ya kawaida katika safari na mbugani ugumu wa maisha ambao wao wataendelea kuangalia ni mawasiliano, usafirishaji, na usalama.
Wamesema katika safari yao wamekumbana na tatizo  kubwa la chakula, usahihi wa taarifa na tatizo la mawasiliano.
“Pamoja na wananchi kuwa marafiki tumeona tatizo kubwa la usafiri na aina ya chakula kinacholiwa na usafi,” alisema Schuller ambaye kitaalamu ni mganga wa meno.
Kwa mtazamo wa watalii hao taifa hili linahitaji kubadili wananchi wake kwa kuwapa elimu ya kutosha kuhusu mazingira yanayowazunguka hasa kwa kujali aina ya mlo wanaokula, usafi wa mazingira na kujali gharama kwa huduma wanazotoa kwa wageni.
Teresa alisema kwa kuwa na aina moja ya chakula Ugali na wali muda wote bila maziwa mboga za majini kunatengeneza aina ya udumavu ambao unachochea watu kukosa lishe bora.
“Tumekuwa tukikumbana na chakula cha aina ile ile kila mahali tunapoenda, chakula cha nafaka ambacho ni wanga lakini hukutani na matunda, mboga za kijani na maziwa,” alisema Teresa.
Pamoja na kuzungumzia mlo, wageni hao walizungumzia  tatizo la rushwa na kusema walipokuwa Zanzibar pamoja na kuhisi kwamba ulinzi ni mkali kutokana na kusimamishwa kila mara katika gari, lakini waliona kuna kitu si sahihi wakati wa mazungumzo kati ya dereva na askari.
“Pale tuliona shida kidogo kwanini wanapenyeza mkono tena unaona kwa uangalifu mkubwa?” Alisema  Annemarie ambaye alisema matendo waliyokumbana nayo yanatia wasiwasi hasa unaposimamishwa mara saba katika kipindi cha dakika 40 wakati wakiwa kisiwa cha Zanzibar.
Kwao wanaamini kwamba lipo tatizo la rushwa na pia tatizo la lugha kwani wengi wameshindwa kuwasiliana nao kutokana na shida ya lugha kiasi ya kwamba wapo watu walikuwa wanawakwepa kwa sababu hawaelewani na wakati mwingine walifanya maamuzi ambayo hayakuwa sahihi kutokana na lugha gongana.
Anasema walipofika Tanga waliambiwa wanaweza kufika Zanzibar kupitia Pangani.Walisema usafiri uliwachosha na hata walipofika Pangani wakagundua kwamba mawasiliano si sahihi lakini wakaingia katika boti na kuelekea Zanzibar.
Boti hiyo ambayo ilikuwa kila mara inatolewa maji, iliwaogopesha sana lakini hata walipokuwa wakitaka kujua wanajiokoaje walijikuta wakiambulia kuambiwa kwamba njia za kujiokolea ni palepale walipo.
Hata hivyo walifarijika baada ya kugundua maboya ya kujiokolea ndio waliyoyakalia.
Pamoja na kufurahishwa na matembezi yao hasa kwa kuona kwamba wameweza kuwaona wanyama wakubwa kama tembo, chui, simba, faru,twiga na nyati walisema ipo haja ya kupunguzwa kwa kiingilio kwani kwa sasa wanakiona kama ghali.
Nilipomuuliza kuhusu Serengeti kama itakufa, alisema kwamba hadhani kwani anaona kwamba bado haijavurugwa sana na kama Watanzania watakubali kwamba ile ni mali yao haitakufa.
“Ni suala la kuelimika na kuhakikisha kwamba utamaduni unajali mazingira, unajali afya na wajibu,” alisema Teresa ambaye katika miaka yake 55 alisema Afrika bado ni bara la kutembelea.
Alisema walifika Sumve kuwaona jamaa zao na marafiki, lakini walishangazwa na wingi wa vituo ambapo treni inasimama japo waliona kwamba hali ile inaweza kuwa inasaidia mzunguko sahihi wa uchumi  wa eneo hilo.
“Njiani tuliona mengi lakini nadhani baya kabisa ni watu kutokujali mazingira yao. Uchafu unatupwa kila mahali na hata maeneo mengine hayakuwa na vyoo na yale yaliyokuwa na vyoo hata karatasi laini za chooni zilikosekana,” alisema Teresa.
Kwa maneno yao watu wanatakiwa kubadilika kupitia elimu ili kutambua kwamba kuna haja ya kuwa na mazingira safi kwa manufaa yao na kizazi kijacho.
“Unakosaje mahali pa kujisaidia? Umelipa fedha ili ufurahi inakuaje unapokosa huduma,” aliuliza Teresa.
Kwa maneno yao wenyewe ugumu wa kupata huduma inayoridhisha kwa fedha halisi  si tu katika maeneo waliyofikia bali hata katika usafiri.
“Ukiwa peke yako huwezi kufanikiwa,” alisema Teresa na kuungwa mkono na Annemarie ambaye yeye kuja Afrika ilikuwa mara yake ya kwanza. Moja ya tatizo ni kukosekana kwa uaminifu miongoni mwa watu wanaoandaa usafiri ambao wamekuwa wakiwatoza ada kubwa kuliko wanayokuja kujua baadaye.
Yalikuwa ni maoni ya mwandishi wa makala haya kwamba tatizo hilo linatokana na kutumia wakala katika masuala ya utalii na badala yake watu  ambao wamejitangaza kujua Tanzania na kwamba watawapokea.
Watu hao ambao unaweza kulinganisha na vishoka wanachojali wao ni kuongeza cha juu na kuwafikisha watalii wao katika maeneo ambayo ni rahisi na wakati mwingine bila kuwa na muunganisho mwema.
Pamoja na udhaifu katika masuala ya utalii hasa mawasiliano na upashanaji wa taarifa elimu inayotakiwa miongoni mwa wananchi ni kubadili masuala yao yanayowafanya wawe na maisha magumu.
Kwa watalii hao wamesema hawajawahi kuona ardhi yenye rutuba kubwa kama Tanzania na kinachotakiwa kufanywa ni watu wake kutumia fursa zilizopo kujikwamua katika dhiki ya umasikini na kuboresha maisha yao.
Walielezea kufurahishwa na ukarimu uliofanywa na Wapare walipoenda kutembelea eneo la Mbagha ambako walilala Tona Lodge na kupata maelezo kuhusu kijiji na kutembelea vivutio mbalimbali likiwemo jiwe lililotumika kuua watoto waliokuwa wanafikiriwa wana mikosi.
Naam, mpaka mwisho wa mazungumzo wageni hao walilalamikia usafi, utunzaji wa mazingira, mfumo wa lishe na mawasiliano hafifu pamoja na lugha gongana unaleta utata wa uaminifu.
Credits; Lukwangule

Jumatatu, 3 Novemba 2014

JAJI WARIOBA APIGWA KIBAO KWENYE MKUTANO UBUNGO PLAZA. ULIITISHWA NA MWALIMU NYERERE FOUNDATION.

TAARIFA YA TUKIO LILILOTOKEA UBUNGO PLAZA  JANA.

IMG-20141102-WA0021
 Mkutano ulifanyika kuanzia saa 1520hrs ukiwa chini ya uenyekiti wa Jaji Mstaafu mh. Joseph Sinde Warioba. Mkutano ulihudhuriwa na watu wa kada mbalimbali sambamba na itikadi tofauti za kisiasa. Mkutano ulirushwa moja kwa moja na ITV na maudhui yake kimtazamo ulilenga kuoanisha mapendekezo ya marekebisho ya Katiba ya tume ya Warioba na ile ya Mh. Sitta na tume yake. Baada ya Mh. Warioba kuelezea kwamba Muungano sio tunu ila
ni urithi ndipo wakereketwa wa upande wa Mh. Sitta walipoinua mabango yasemayo pamoja na mambo mengine kwamba iweje wajadili mapendekezo ya katiba ya Mh. Sitta ambayo wao wameshaikubali? Baada ya mabango yale kuinuliwa yakazua tafrani ambapo walishauriwa kutoyainua kwa sababu haukuwa mkutano wa kisiasa na wakanyang’anywa na kuyachana ndipo vurugu/kashfa/matusi yakaanza kutolewa dhidi ya meza kuu. Hali hii ilisababisha kushikana, kusukumana na kurushiana viti. Katika tafrani hiyo mh. Warioba alipigwa kibao na Mh. Paulo Makonda- ambaye ni katibu wa UVCCM TAIFA. Mtuhumiwa huyu pamoja na wengine wanne wamekamatwa kwa mahojiano. Upelelezi unaendelea na juhudi za kuwapata wengine zinaendelea.

IGP MSTAAFU PHILEMON MGAYA ASHEREHEKEA MIAKA 85 YA KUZALIWA


WAZIRI Mkuu Mstaafu Cleopa Msuya amewaomba Watanzania kuwa na tabia ya utii wa sheria, uaminifu na uadilifu katika nafasi zao wanazozitumukia katika Taifa la Tanzania.
Msuya aliyasema hayo katika sherehe ye kuadhimisha miaka 85 ya kuzaliwa ya aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Philemon Mgaya iliyofanyika katika Hotel ya Protea , Court Yard jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu Mstaafu alieleza kuwa tabia aliyoionyesha Mgaya wakati wa utumishi wake serikalini inapaswa kuigwa na watanzania wote.
“Huyu ndiye Mtanzania halisi aliyelelewa vizuri kuitumikia nchi yake. Hana makuu, ni mkweli na mwadilifu. Akiahidi kufanya jambo fulani analitekeleza bila kuchelewa. Tunahitaji uwajibikaji wa namna hii,” Msuya alisisitiza.
Alisema kuwa Mgaya alikuwa kiongozi hodari ambaye alisimamia vyema kiapo na kazi zake na kipindi chake cha uongozi alikuwa akitoa amri zinatekelezwa mara moja.
Naye Mshauri wa kimataifa wa Kujitegemea wa Kampuni ya Mabibo Beer Wines and Spirits Limited James Rugemalira alitoa wito kwa watanzania kuendele kuunga mkono jitihada za kuendeleza maeneo mbalimbali ya kiuchumi ikiwemo viwanda.
Aliwasihi wadau kutoa ushirikiano kwa kampuni yake inayosambaza bia aina ya Windhoek Larger na Windhoek Draught ambayo inadhamira ya kujenga kiwanda cha kuzalisha bia hizo hapa nchini.
“Tunatafuta maeneo Kilimanjaro, Tanga na Bukoba ili tuweze kujenga kiwanda hapa nchini. Tumedhamilia kufanya hivyo na tutafanya,” Rugemalira alisisitiza.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo Benedicta Rugemalira aliwashukuru wananchi kwa kukubali kujumuika pamoja katika hafla hiyo na kumwomba Mzee Mgaya aendelee kuwapa mwongozo wa namna ya kuenenda katika maisha.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Kilutheli Tanzania (KKKT) Dkt. Alex Malasusa aliwaomba watanzania kuwa na moyo wa unyenyekevu na kujitolea kulitumikia taifa katika utumishi wao kama ilivyokuwa kwa IGP mstaaafu Mzee Mgaya.
Wageni wengine waliohudhuria hafla hiyo ni Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dkt. Fenella Mukangara, Katibu Mkuu Msaaafu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Balozi Bakari Mwapachu, Balozi Anthony Nyaki na wazee wengine maarufu kama Timothy Msangi, Mzee James Rugemalira na wengineo.
Mara Baada ya Ibada katika Kanisa la Azania Front wakati wa kuadhimisha miaka 85 ya kuzaliwa ya aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Mzee Philemon Mgaya.
Baadhi ya waumini mbalimbali wakiwa nje baada ya Ibada.
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Mstaafu Philemoni Mgaya akiwa katika siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwake.
Keki.
Waziri Mkuu Mstaafu Mhe Cleopa David Msuya akimpongeza aliyekuwa IGP Philemoni Mgaya.
Mzee Timothy Msangi akieleza Historia fupi ya IGP Mstaafu Mzee Philemon Mgaya.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Kilutheli Tanzania (KKKT) Alex Malasusa akitoa salam za Pongezi kwa IGP mstaafu.
Mshauri wa kimataifa wa Kujitegemea wa Kampuni ya Mabibo Beer Wines and Spirits Limited James Rugemalira akitoa pongezi zake kwa IGP Mstaafu na kuelezea Kampuni ya Mabibo Beer Wines and Spirits Limited.
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni Mabibo Beer and Wines Mama Benedicta Rugemalira akitoa salam za Pongezi kwa IGP mstaafu.
Mshereheshaji Joe Mgaya ambaye ni Mtoto wa IGP Mstaafu Philemon Mgaya akisherehesha.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Kilutheli Tanzania (KKKT) Dkt. Alex Malasusa akimpongeza Mzee Mgaya.
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dkt. Fenella Mukangara akimpa mkono wa Pongezi IGP mstaafu.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Kilutheli Tanzania (KKKT) Dkt. Alex Malasusa na Mzee Mgaya wakiwa katika Furaha.
IGP Mstaafu akipokea zawadi.
IGP Mstaafu Philemoni Mgaya akikata keki huku amezungukwa na wajukuu wake.
Mzee Mgaya akipongezwa na Mzee James Rugemalira.
Haya wajukuu na tule keki sasa.
Balozi Juma Mwapachu na Mwenyekiti Mstaafu wa Gymkhana Club Mzee George Kritsos wakipozi na Mzee Mgaya.
Mzee Mgaya akipozi na baadhi ya watu mashuhuri waliohudhuria sherehe hizo.
Waziri Mkuu Mstaafu Mzee Cleopa David Msuya akiwa na mabinti wa Mzee Msangi.
Watu mbalimbali wakiwa katika Sherehe hiyo.
Burudani ya nguvu.
Credits Sondacom