Jumanne, 11 Novemba 2014

MBOWE AMCHANA SITTA MBELE YA WAPIGA KURA WAKE.

Mbowe ‘amwaga sumu’ nyumbani kwa Sitta

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akiwasili kwenye Uwanja wa Extended mjini Urambo, Tabora alikohutubia mkutano wa hadhara juzi. Na Mpigapicha Maalum
Urambo. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amefanya mkutano mkubwa Urambo Mashariki na kumshutumu Mbunge wa jimbo hilo, Samuel Sitta kwa kuchakachua maoni ya wananchi katika mchakato wa Katiba Mpya.
Katika mkutano huo ulifanyika katika Uwanja wa Extended mjini hapa takriban mita 100 kutoka nyumbani kwa Sitta aliyeongoza Bunge la Katiba, Mbowe alisema historia ya nchi hii itamhukumu mbunge huyo kwa maovu hayo.
Alisema kutokana na uovu huo wa Sitta ambaye amekuwa akiisifia Katiba Inayopendekezwa kuwa itakuwa nzuri Afrika Mashariki na Kati, vyama vya upinzani vitaendelea kuidai katiba ya wananchi hata kwa miaka 100 ijayo.
Aprili mwaka huu, wabunge wa vyama vya upinzani chini ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), walisusia Bunge la Katiba mjini Dodoma wakilalamikia kuvunjwa kwa kanuni na kutofuatwa kwa mapendekezo ya wananchi yaliyotolewa katika Rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.
Akihutubia mamia ya wafuasi wa chama hicho kwenye Operesheni Delete CCM, Mbowe ambaye pia ni mwenyekiti mwenza wa Ukawa, alisema ana uhakika Sitta ataipata hukumu hiyo ya historia kwa kile alichosema kudhulumu haki ya Watanzania milioni 45.
Mbowe anayetumia chopa katika ziara hiyo, alifika katika uwanja huo saa 11.45 na kuhutubia kwa dakika 30.
“Mzee Sitta najua upo nyumbani hapo na unanisikia, kama hunisikii basi mke wako Mama Margreth Sitta atakuwa ananisikia, lakini kama naye hayupo basi kutakuwa na wahudumu watanisikia na watakuja kukueleza,” alisema huku akiwaonyesha wafuasi wa chama hicho nyumba ya Sitta iliyopo jirani na uwanja huo.
Alisema Sitta alipuuza maoni ya wananchi waliyotoa katika mchakato wa Katiba Mpya na ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba badala yake akaweka maoni ya chama chake cha CCM.
“Tunasema kwamba historia ya nchi hii itamhukumu kwa maovu aliyoyafanya kukataa maoni ya wananchi na kuweka maoni ya chama chake,” alisema.
Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Hai, alisema baada ya maoni ya wananchi kuchakachuliwa... “Sasa tutaidai Katiba Mpya hata kwa miaka 100 ijayo.”
Alisema wabunge wa vyama vya upinzani walimwamini Sitta kwa kumpigia debe na baadaye walimpa kura  iliyomfanya awe Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba kutokana na rekodi yake alipokuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Tulifanya hivyo kwa kumwamini kutokana na rekodi zake akiwa spika, tunajuta kumchagua hatukufahamu kwamba atatusaliti na kudhulumu haki za Watanzania,” alisema Mbowe.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni