KAMA vituo 66 vya treni havitoshi katika safari nzima ya utalii, Teresa Williamson wa Australia na Annemarie Schuller wa Uholanzi wamesema Watanzania wanaishi katika mazingira magumu na wanastahili kubadilika.
Kauli hiyo wameitoa wakati wakizungumza na Mwandishi wa makala haya muda mfupi kabla ya kuondoka kurejea makwao baada ya ziara ya wiki mbili katika maeneo mbalimbali nchini.
Katika ziara yao ya kitalii walitumia treni, barabara na maji tena kwa kutumia jahazi wakitokea Pangani Tanga hadi Zanzibar.
Nilitaka kujua baada ya utalii wao wameona nini nchini Tanzania walisema pamoja na kufanikiwa kuwaona wanyama wakubwa watano kama walivyofikiria wakati wakiwa makwao wameshuhudia maisha masikini zaidi kuliko matarajio.
“Sijui inatokeaje watu wengi wana simu za mkono lakini ukiangalia maisha yao unayaona kuwa magumu sana,” alisema Teresa ambaye alifafanua kwamba ugumu wa maisha unaonekana katika miundombinu na usafirishaji, ulaji na utunzaji wa mazingira.
Wakiwa wamezaliwa mjini hawakuwa wanajua vijijini kukoje mpaka walipofika nchini Tanzania na kukumbana na hali ambayo hawakuitarajia hata kidogo.
Pamoja na kushuhudia matukio yasiyokuwa ya kawaida katika safari na mbugani ugumu wa maisha ambao wao wataendelea kuangalia ni mawasiliano, usafirishaji, na usalama.
Wamesema katika safari yao wamekumbana na tatizo kubwa la chakula, usahihi wa taarifa na tatizo la mawasiliano.
“Pamoja na wananchi kuwa marafiki tumeona tatizo kubwa la usafiri na aina ya chakula kinacholiwa na usafi,” alisema Schuller ambaye kitaalamu ni mganga wa meno.
Kwa mtazamo wa watalii hao taifa hili linahitaji kubadili wananchi wake kwa kuwapa elimu ya kutosha kuhusu mazingira yanayowazunguka hasa kwa kujali aina ya mlo wanaokula, usafi wa mazingira na kujali gharama kwa huduma wanazotoa kwa wageni.
Teresa alisema kwa kuwa na aina moja ya chakula Ugali na wali muda wote bila maziwa mboga za majini kunatengeneza aina ya udumavu ambao unachochea watu kukosa lishe bora.
“Tumekuwa tukikumbana na chakula cha aina ile ile kila mahali tunapoenda, chakula cha nafaka ambacho ni wanga lakini hukutani na matunda, mboga za kijani na maziwa,” alisema Teresa.
Pamoja na kuzungumzia mlo, wageni hao walizungumzia tatizo la rushwa na kusema walipokuwa Zanzibar pamoja na kuhisi kwamba ulinzi ni mkali kutokana na kusimamishwa kila mara katika gari, lakini waliona kuna kitu si sahihi wakati wa mazungumzo kati ya dereva na askari.
“Pale tuliona shida kidogo kwanini wanapenyeza mkono tena unaona kwa uangalifu mkubwa?” Alisema Annemarie ambaye alisema matendo waliyokumbana nayo yanatia wasiwasi hasa unaposimamishwa mara saba katika kipindi cha dakika 40 wakati wakiwa kisiwa cha Zanzibar.
Kwao wanaamini kwamba lipo tatizo la rushwa na pia tatizo la lugha kwani wengi wameshindwa kuwasiliana nao kutokana na shida ya lugha kiasi ya kwamba wapo watu walikuwa wanawakwepa kwa sababu hawaelewani na wakati mwingine walifanya maamuzi ambayo hayakuwa sahihi kutokana na lugha gongana.
Anasema walipofika Tanga waliambiwa wanaweza kufika Zanzibar kupitia Pangani.Walisema usafiri uliwachosha na hata walipofika Pangani wakagundua kwamba mawasiliano si sahihi lakini wakaingia katika boti na kuelekea Zanzibar.
Boti hiyo ambayo ilikuwa kila mara inatolewa maji, iliwaogopesha sana lakini hata walipokuwa wakitaka kujua wanajiokoaje walijikuta wakiambulia kuambiwa kwamba njia za kujiokolea ni palepale walipo.
Hata hivyo walifarijika baada ya kugundua maboya ya kujiokolea ndio waliyoyakalia.
Pamoja na kufurahishwa na matembezi yao hasa kwa kuona kwamba wameweza kuwaona wanyama wakubwa kama tembo, chui, simba, faru,twiga na nyati walisema ipo haja ya kupunguzwa kwa kiingilio kwani kwa sasa wanakiona kama ghali.
Nilipomuuliza kuhusu Serengeti kama itakufa, alisema kwamba hadhani kwani anaona kwamba bado haijavurugwa sana na kama Watanzania watakubali kwamba ile ni mali yao haitakufa.
“Ni suala la kuelimika na kuhakikisha kwamba utamaduni unajali mazingira, unajali afya na wajibu,” alisema Teresa ambaye katika miaka yake 55 alisema Afrika bado ni bara la kutembelea.
Alisema walifika Sumve kuwaona jamaa zao na marafiki, lakini walishangazwa na wingi wa vituo ambapo treni inasimama japo waliona kwamba hali ile inaweza kuwa inasaidia mzunguko sahihi wa uchumi wa eneo hilo.
“Njiani tuliona mengi lakini nadhani baya kabisa ni watu kutokujali mazingira yao. Uchafu unatupwa kila mahali na hata maeneo mengine hayakuwa na vyoo na yale yaliyokuwa na vyoo hata karatasi laini za chooni zilikosekana,” alisema Teresa.
Kwa maneno yao watu wanatakiwa kubadilika kupitia elimu ili kutambua kwamba kuna haja ya kuwa na mazingira safi kwa manufaa yao na kizazi kijacho.
“Unakosaje mahali pa kujisaidia? Umelipa fedha ili ufurahi inakuaje unapokosa huduma,” aliuliza Teresa.
Kwa maneno yao wenyewe ugumu wa kupata huduma inayoridhisha kwa fedha halisi si tu katika maeneo waliyofikia bali hata katika usafiri.
“Ukiwa peke yako huwezi kufanikiwa,” alisema Teresa na kuungwa mkono na Annemarie ambaye yeye kuja Afrika ilikuwa mara yake ya kwanza. Moja ya tatizo ni kukosekana kwa uaminifu miongoni mwa watu wanaoandaa usafiri ambao wamekuwa wakiwatoza ada kubwa kuliko wanayokuja kujua baadaye.
Yalikuwa ni maoni ya mwandishi wa makala haya kwamba tatizo hilo linatokana na kutumia wakala katika masuala ya utalii na badala yake watu ambao wamejitangaza kujua Tanzania na kwamba watawapokea.
Watu hao ambao unaweza kulinganisha na vishoka wanachojali wao ni kuongeza cha juu na kuwafikisha watalii wao katika maeneo ambayo ni rahisi na wakati mwingine bila kuwa na muunganisho mwema.
Pamoja na udhaifu katika masuala ya utalii hasa mawasiliano na upashanaji wa taarifa elimu inayotakiwa miongoni mwa wananchi ni kubadili masuala yao yanayowafanya wawe na maisha magumu.
Kwa watalii hao wamesema hawajawahi kuona ardhi yenye rutuba kubwa kama Tanzania na kinachotakiwa kufanywa ni watu wake kutumia fursa zilizopo kujikwamua katika dhiki ya umasikini na kuboresha maisha yao.
Walielezea kufurahishwa na ukarimu uliofanywa na Wapare walipoenda kutembelea eneo la Mbagha ambako walilala Tona Lodge na kupata maelezo kuhusu kijiji na kutembelea vivutio mbalimbali likiwemo jiwe lililotumika kuua watoto waliokuwa wanafikiriwa wana mikosi.
Naam, mpaka mwisho wa mazungumzo wageni hao walilalamikia usafi, utunzaji wa mazingira, mfumo wa lishe na mawasiliano hafifu pamoja na lugha gongana unaleta utata wa uaminifu.